3.Kujichukulia Sheria Mkononi kwenye Makosa ya Sheria za Barabarani.

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Barabara kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Ukurasa huu maalum unakuletea uchambuzi wa Sheria mbalimbali zinazohusiana na barabara. Kila siku kuna matukio mengi sana yanaendelea barabarani, lakini si watu wengi wanaojua taratibu zinazopaswa kuchukuliwa ili kushughulikia matukio hayo. Leo tunaangalia tabia za watu kujichukulia sheria mkononi kwenye makosa ya sheria za barabarani. Karibu tujifunze.

Makosa yatokanayo na Sheria za Barabarani

Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 ndiyo inaongoza kwa masuala yote ya watumizi wa barabara kuzingatia pindi wanapokuwa wakitumia barabara siku kwa siku.

Sheria hii inaainisha kanuni na taratibu za watumiaji wa barabara ambazo wanapaswa kuzizingatia. Katika sheria hii imeanisha haki na wajibu wa kila mmoja anayetumia barabara. Pia yapo makosa ambayo yameanishwa na adhabu zake kupitia kanuni za sheria hii na miongozo mbalimbali.

Changamoto kubwa inayoibuka katika matumizi ya sheria hii ni hali mbaya ya matukio mabaya yanayozidi kutokea barabarani kwa watumizi wake kutokuzingatia sheria. Matokeo yake mfumo mzima wa utekelezaji wa sheria za barabara umekuwa mgumu na kulemewa na uhalifu au makosa ya barabarani yanayofanywa na madereva au watumiaji wengine wa barabara.

Matukio mabaya, ajali na makosa mengine ya barabarani imefanya jamii kutafuta njia mbadala ya kukomesha au kupunguza athari za matukio haya kwa njia isiyofaa ya kuchukua sheria mkononi kwa kuadhibu madereva au watu wengine wanaojikuta wapo katika kadhia ya makosa ya barabarani. Imekuwa si jambo geni kusikia magari yamechomwa moto au watu wamefunga barabara kutokana na ajali katika eneo fulani huku wakishindikiza vyombo vinavyo husika kuchukua hatua stahiki.

Hii yote ni kutokana na kuchoshwa na mwendelezo wa matukio na kupoteza ndugu, wapendwa, jamaa na marafiki wa maamuzi mabovu yanayofanywa na watumiaji wa barabara hasa madereva wa vyombo vya moto.

Hata hivyo yapo madhara ya uamuzi wa kuchukua sheria mkononi katika makosa ya barabarani

Hapa nitaeleza baadhi ya madhara hayo;

  • Kusababisha mauaji ya mtu au watu waliohusika katika makosa ya barabarani. Mara kwa mara tumesikia na kupata ushuhuda juu ya madereva kuuwawa au kuumizwa kutokana na ajali zinazotokea barabarani. Wananchi wanaamua kuchukua hatua na kutoa adhabu pasipo kuwa na utaalam wa kujua nini hasa chanzo cha ajali husika. Ni rahisi sana wananchi kupima kuwa kwa kuwa dereva muhusika alikuwa na gari kubwa na mwathiriwa alikuwa na gari dogo au boda boda basi yule wa gari kubwa kwa vyovyote ndiye mwenye makosa. Jambo hili si sahihi hata kidogo, vyanzo vya ajali vinatokea kwa sababu mbalimbali.
  • Uharibifu wa vyombo vya usafiri. Mara nyingi tunaona wananchi ‘wenye hasira kali’ wakichukua hatua ya kuchoma moto magari au boda boda kutokana na ajali zilizojitokeza. Pasipo kuwa na muda wa kutafakari watu wanaamua kuharibu mali husika bila kutoa nafasi ya uchunguzi makini kujua nani mwenye makosa.
  • Kupoteza nafasi nzuri ya uchunguzi na hatua sahihi za kisheria kuchukuliwa. Kitendo cha kuchukua sheria mkononi kinawakosesha waathiriwa nafasi ya kupata haki yao kwani mazingira ya eneo la ajali yanapoharibiwa vyombo vinavyohusika haviwezi kufanya uchunguzi ipasavyo.
  • Kupoteza nafasi ya Serikali kuboresha mbinu za kupunguza makosa au kurekebisha sheria kukidhi matakwa ya sasa. Kupitia uchunguzi na takwimu sahihi, Serikali inapata sababu ya kuweza kufanyia kazi changamoto za makosa ya ajali kwa kurekebisha sheria au kubuni mbinu nyingine za kusaidia utendaji bora wa sheria. Kitendo cha kuchukua sheria mkononi kinapoteza fursa hiyo.
  • Upotevu wa mali au wizi wa mali unaotokea baada ya ajali. Kumekuwa na tabia mbaya ya wananchi kuvamia na kupora mali mara baada ya ajali kutokea. Tabia hii tumeona ikisababisha maafa makubwa hasa ajali inapohusu magari ya mafuta. Uungwana unatutaka kuwa waangalifu wa hali za wale waliopata ajali katika kuhakikisha usalama wao na mali zao.

Hatua za kuchukua kuepusha watu kuchukua sheria mkononi katika makosa ya sheria za barabarani

  • Kuboresha utendaji na ufanisi wa vyombo vinavyoisimamia sheria ya barabara. Katika usimamizi wa sheria hii lipo Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani, LATRA pia wakala wa barabara TANROADS. Vyombo hivi vinapaswa kuboreshwa ili kuongeza ufanisi unaoendana na kasi ya sayansi na teknolojia.
  • Kurekebisha sheria kulingana na matakwa ya muda. Yapo makosa mengine yanachangiwa na matumizi ya simu za mkononi kwa madereva wakati wa kuendesha gari. Hali hii imeongezeka sana maeneo ya mjini. Ni muhimu sheria ikarekebishwa kutoa adhabu kwa wale wote wanaotumia simu aidha kwa kuongea au kutuma jumbe wakiwa wanaendesha barabarani. Busara inatutaka tufanye hivyo mahali pa utulivu ukihitaji kuwasiliana weka gari pembeni.
  • Kuongeza ukaguzi wa mara kwa mara kwa vyombo vya usafiri ili kuona endapo vinakidhi vigezo vya kuweza kutumika barabarani. Kwa sasa tumeshuhudia vyombo vya usalama vikifanya ukaguzi hasa kwenye mabasi ya abiria ya mikoani. Ni muhimu zoezi hili likawa endelevu vya vyombo vingine.
  • Kuweka mfumo wa kisasa katika barabara ili kukagua mwenendo wa shughuli na matumizi ya barabara kwa kutumia kamera. Watu wengi wanazingatia sheria pale wanapoona uwepo wa askari, hivyo njia nzuri ya kuboresha ni kuwa na kamera ambazo zitaangalia masaa 24 kwa siku kusaidia vyombo vya usalama barabarani kubaini makosa na kuchukua hatua mapema.
  • Kuanzisha baraza au vyombo maalum kwa ajili ya kusikiliza mashauri na makosa ya barabarani tofauti na mashauri haya kuwa katika mfumo wa mahakama za kawaida. Watu hawaridhiki na mwenendo wa pole pole katika mashauri ya usalama barabarani ndio msingi wa wao kuchukua maamuzi ya kujichukulia sheria mkononi.
  • Kuota elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya masuala ya kuzingatia sheria katika barabara na kuacha mkondo wa sheria kuchukua hatamu kwani kwa jinsi hiyo waathiriwa wanaweza kupata haki zao endapo makosa yatadhibitika. Unakuta gari limechomwa na waathirika wanakosa hata mtu wa kushitaki ili kulipwa na Bima.

Kumekuwa na jitihada za makusudi za kuboresha mifumo ya matumizi bora ya barabara. Vikosi vya usalama barabarani vimekuwa mara kwa mara vikifanya ukaguzi. Hatahivyo, mara nyingine nia ya ukaguzi imekuwa ikitumiwa vibaya na kusababisha usumbufu kwa madereva na wenye vyombo vya usafiri. Majukumu ya vyombo hivi ni kusaidia kuboresa usalama barabarani kwa kutoa maelekezo, kutoa elimu na ushauri bora kwa watumizi wa barabara. Kinyume na baadhi yao kwa sasa kila kitu ni faini tu hata wanaenda mbali zaidi na wengine kuonewa kwenye makosa ambayo hawakufanya. Tuwatendee haki wote yaani madereva na watumizi wengine wa barabara. Msingi wa kutenda haki ni muhimu sana na itaondoa dhana ya watu waliokosana barabarani kuamua ‘kumalizana wenyewe’ kwa namna wao wanayoona inafaa bila kufuata sheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili