Sheria Leo. Maeneo ambayo watu hupenda Kujichukulia Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunaangalia maeneo ambayo watu hupenda kujichukulia sheria mkononi. Karibu tujifunze.

Dhana ya kuchukua sheria mkononi

Tumeeleza kwa muda mrefu kutokana na mfululizo wa makala hizi juu ya watu kujichukulia sheria mkononi kama jambo ambalo halipaswi kukubalika wala kushabikiwa na jamii bali kukemewa kwa nguvu zote.

Kujichukulia sheria mkononi ni ile hali ya kufanya maamuzi na kuyatekeleza dhidi ya mtu mwengine au kitu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa kisheria.

Tumeweza kuzichambua sababu mbalimbali zinazochangia tabia hii kukithiri ndani ya jamii na pia kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua katika kila sababu iliyojadiliwa.

Katika makala hii tunakwenda kuangalia kwa uchache maeneo ya kimgogoro ambayo mara nyingi tunashuhudia watu au jamii wakichukua sheria mkononi.

Maeneo ya kisheria ambayo watu hujichukulia sheria mkononi

Katika maisha yetu wanadamu jambo la migogoro ni suala ambalo haliepukiki. Hii ni kwa sababu tu sisi sote hatufanani wala maamuzi yetu au mtazamo wetu hauwezi kufanana. Kutokana na hali hii migogoro mingi huzaliwa kila siku. Hatahivyo, umewekwa utaratibu wa kuitatua kwa kufuata sheria. Kwa bahati mbaya watu hawapendi kuifuata sheria katika kufikia suluhu ya migogoro yao. Hapa tunaangalia baadhi ya maeneo ya kisheria ambayo inazua migogoro mingi na watu hupenda kujichukulia sheria mkononi.

  1. Migogoro ya ardhi

Hili ni eneo ambalo linazalisha migogoro mingi kila siku. Kuhusiana na ardhi tunashuhudia migogoro baina ya mtu na jirani, ndugu wa familia, jamii na wawekezaji na hata migogoro katika ya jamii ya wakulima na wafugaji. Migogoro hii imekuwa na madhara makubwa kwa jamii yote kwa ujumla na kuzorotesha mahusiano.

Katika maeneo ya kisheria suala la ardhi ndilo linaongoza kuwa na mashauri mengi mahakamani ambayo yanachukua muda mrefu sana kukamilika.

Serikali kwa kuona kuwa migogoro ya ardhi imekuwa mingi, ikaanzisha mahakama maalum za kusikiliza migogoro ya ardhi na kutatua kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya na mahakama kuu kama ngazi ya kitaifa. Mfumo wa mahakama hizi ulianza kazi mnano mwaka 2002. Bado changamoto ya migogoro ya ardhi imekuwa kubwa na zinahitajika juhudi kubwa zaidi kutafuta mfumo bora wa kuboresha utatuzi kwa haraka zaidi.

Ni kwa sababu hii inaweza kuwa mojawapo ya eneo ambalo jamii inapata mtazamo wa kuwa na maamuzi ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuona mlolongo wa kufuata hatua za kisheria unaweza kuchukua muda mrefu sana.

Madhara ya kuchukua sheria mkononi kwenye migogoro ya ardhi

Yapo madhara mengi yanayojitokeza kwa mtu au jamii kuchukua hatua za kisheria mkononi katika migogoro ya ardhi. Hapa nitaeleza baadhi ya madhara hayo;

  • Kusababisha mauaji ya mtu au watu katika jamii ambazo zinapambana katika ardhi. Tumekuwa tukishuhudia kila siku juu ya madhila yanayojitokeza katika migogoro ya ardhi kwa watu kuuwawa na kujeruhiwa katika mapambano. Mfano ni migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imeshamiri katika nchi yetu.

 

  • Uharibifu wa mali na mifugo. Sehemu nyingine ya madhara ya migogoro ya ardhi ni uharibifu wa mali na mifugo katika migogoro ya ardhi. Watu wameharibiwa nyumba zao, majengo yao na hata kuuwawa kwa mifugo yao kutokana na mgogoro wa ardhi.

 

  • Kupoteza nafasi ya uzalishaji. Sikuzote mahali ambapo kuna migogoro ya ardhi basi hakuna uzalishaji wowote wa kuleta tija kwenye jamii. Wale wanaogombana wanajikuta wote hawapati nafasi ya kufanya maendeleo katika ardhi husika.

 

  • Kupoteza rasilimali muda. Muda mrefu sana unapotea katika kuingia kwenye migogoro ya ardhi. Watu wanapoingia kwenye mgogoro wa ardhi muda mwingi hupotea endapo mgogoro ule hautapatiwa suluhu ya mapema.

 

Hatua za kuchukua kuepusha watu kuchukua sheria mkononi katika migogoro ya ardhi

  • Kuboresha mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa kuongeza vyombo vya utatuzi kwa kuwa na mabaraza mengi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, watumishi.

 

  • Kuanzisha mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi. Mingi ya migogoro ya ardhi haikupaswa kuwa migogoro endapo njia bora za utatuzi zitatumika. Mfumo ukiboreshwa na kutoa nafasi ya usuluhishi basi migogoro mingi itaishia katika ngazi hiyo.

 

  • Kila mtu anayemiliki ardhi kuhakikisha anaweka alama za mipaka yake na wakati wa kuuza au kununua majirani husika wanakuwa na taarifa.

 

  • Wananchi wanapaswa kuwa na hali au tabia ya kupenda kufuata utaratibu ili kuokoa muda mwingi unaopotezwa katika migogoro.

 

Ndugu msomaji ni vyema kutambua kwamba masuala ya ardhi ni ya muhimu sana kuzingatia katika suala la umiliki na uhalali wa matumizi ya eneo husika ili kuepuka madhara ya muda mrefu. Kama una uhakika juu ya ardhi husika basi ni ruksa kufanya shughuli zako bali kama huna uhakika fuatilia upate uhakika huo. Muhimu zaidi maeneo yetu yakawa na vipimo ambapo tunapatiwa hati za umiliki kupitia Halmashauri za Manispaa za maeneo tuliyopo.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili