Sheria Leo. Hatua za Kuchukua dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Tumejifunza kwa muda mrefu juu ya makosa mbali mbali na namna ya kisheria kosa linavyotokea kwa kitendo na dhamira. Katika makala iliyopita tuliangalia ‘Kwa nini watu husita kuchukua hatua dhidi ya ukatili kwenye mahusiano?. Leo tutaangalia ‘Hatua za Kuchukua dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano’

Karibu tujifunze.

 Ukatili/Vipigo kwenye Mahusiano ni Kosa Kisheria

Ni muhimu kufahamu kuwa vitendo vyovyote vya kuonesha ukatili au kumpiga mwenzi katika mahusiano ni kosa la kijinai. Tumeeleza wazi mwanzo kuwa jinai ni makosa yanayoshtakiwa na Jamhuri dhidi ya mtuhumiwa na ukipatikana na hatia basi unaweza kufungwa jela. Hivyo ni vyema pande zote zikatambua kuwa vitendo vya kupiga mwengine au ukatili katika mahusiano ni makosa ambayo pande zote yaani mwathiriwa na mtendaji ukatili wanapaswa kufahamu.

‘Kifungu cha 66 cha Sheria ya Ndoa ya 1971 kinaeleza wazi kuwa hakuna mwenye haki ya kumwadhibu mwenzi wake kwa vipigo au adhabu ya viboko bila kujali tamaduni au mila za eneo husika au asili ya wanandoa hao’

Kuna wengine wanachukulia suala la kumwadhibu mume au mke ni jambo la kimila au kitamaduni, Sheria hii imeweka wazi kuwa kitendo hicho hakiruhusiwi na ni kosa kisheria.

Katika makala hii ya leo tunaenda kuangalia baadhi ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na mwathiriwa au jamii kwa lengo la kupunguza au kukomesha vitendo hivi vya ukatili au vipigo kwenye mahusiano.

Kumekuwa na changamoto kubwa kwa waathiriwa wa vitendo vya unyanyasaji kutokujua hatua za kuchukua au wapi pa kupeleka malalamiko yao. Wengi huishia kuumia au kuwaambia ndugu, jamaa na marafiki ambao hawatoi msaada wowote zaidi ya kuwaambia ‘wavumilie’. Katika makala ya leo tutakuonesha baadhi ya maeneo yanayoweza kushughulikia masuala haya na kupata suluhu ya kudumu.

  1. Kutoa taarifa katika baraza la usuluhishi la ndoa la Kata

Sheria ya Ndoa ya 1971 inaeleza juu ya uundwaji wa mabaraza ya usuluhishi ya masuala ya ndoa katika kila Kata. Wanandoa wengi hawafahamu uwepo wa mabaraza haya. Ni muhimu linapojitokeza tatizo lolote kuchukua hatua na kutoa taarifa kwenye baraza la usuluhishi wa ndoa nao watachukua hatua za kumwita mwenzi huyo kuweza kupata suluhu. Hii itasaidia hata kwa baadae na kukulinda dhidi ya mashambulizi mengine.

  1. Kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kidini

Hili ni eneo lingine ambalo kutokana na changamoto hizi unaweza kutumia kwa ajili ya kutafuta suluhu. Tunafahamu ndoa nyingi zinafungwa na viongozi wa kidini. Ni dhahiri wana mchango mkubwa wa kuweza kuleta amani na ustawi wa ndoa au mahusiano husika endapo kutajitokeza tofauti baina ya pande mbili. Tumia fursa hii vizuri ya kuweza kutafuta suluhu baina yako na mwenzi wako endapo kutaanza kujionesha matukio ya ukatili au vipigo.

  1. Ofisi ya Ustawi wa Jamii

Ofisi za ustawi wa jamii zipo katika kila Kata, hivyo ni nafasi nzuri ya kuweza kuwasilisha malalamiko yoyote yanayohusiana na manyanyaso kwenye uhusiano wako na mwenzi wako. Ofisa wa ustawi atachukua hatua za kumwita mwenzi wako ili kuweza kuzungumza tofauti zilizopo na kufikia mwafaka wa tatizo lenu.

  1. Dawati la Jinsia katika Vituo vya Polisi

Kutokana na wingi wa matukio ya unyanyasaji unaoendelea katika familia, Serikali kupitia Jeshi la Polisi lilianzisha dawati maalum la jinsia. Dawati hili lnajishughulisha na maswala yanayojitokeza katika familia kama ya unyanyasaji, vipigo n.k. kama hali katika mahusiano yenu imezidi kuwa mbaya na mwenzi wako haonekani kubadili mwenendo wake basi chukua hatua ya kutoa taarifa katika kituo cha Polisi nao watakuelekeza kufuata utaratibu wa kushughulikia malalamiko hayo kupitia dawati la jinsia.

Linapokuja suala la mtu kumshtaki mwenzi wake kituo cha Polisi linahamsha ukakasi sana kwenye jamii na kuona kama vile anayeshtaki hamtakii mema mwenzi wake, hatahivyo jamii yetu imekuwa nzito sana kuchukua hatua kumsaidia mwathiriwa kabla hali yake kuwa mbaya. Hivyo kama tungependa hali hii isiendelee basi ni muhimu kuwasaidia mapema.

Hitimisho

Hofu kubwa inatawala jamii yetu kwa kufumbia macho vitendo hivi hasa wale wanaoathiriwa na ukatili huu na unyanyasaji katika mahusiano. Wengine wanahofu kuwa wakieleza yanayowasibu basi mateso yataongezeka. Hatuna sababu ya kuwa na hofu kwani hata watesi hao wana hofu kubwa kuliko wewe mwathiriwa kwamba ikitokea amejulikana na jamii kile anachokitenda hatokuwa na ujasiri wa kufanya hivyo mbele ya jamii. Tuchukue hatua kuepusha majanga na mauaji ya kutisha yanayotokea kila leo, kukaa kwetu kimywa kunaweza hali hii kututokea na sisi pia. Hakuna aliye salama kwa kukaa kimya.

Usikubali kuwa sehemu ya jamii inayonyamazia vitendo vya ukatili katika mahusiano bali chukua hatua sahihi ndani ya wakati

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili