47.B. Madai Mengine Muhimu katika Usitishaji wa Ajira
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeanza kuchambua hoja na swali linalohusu aina na dai au madai ambayo mfanyakazi anaweza kudai endapo ataachishwa kazi isivyo kihalali. Leo tunaendelea kuangalia juu ya Madai Mengine Muhimu wakati wa Usitishaji wa Ajira
Nini unaweza kudai endapo umeachishwa kazi isivyo kihalali?
Karibu sana tujifunze kwa pamoja.
Msingi wa Madai
Katika sehemu ya kwanza ya madai mengine muhimu wakati wa usitishaji wa ajira tumeona juu ya mfanyakazi kudai malimbikizo ya mishahara, mshahara badala ya notisi na malipo ya kiinua mgongo. Leo tunaendelea na sehemu nyingine ya madai ambayo mfanyakazi anaweza kudai wakati wa usitishaji wa ajira.
- Likizo
Mfanyakazi ni anaweza kudai likizo endapo muda anaositisishwa ajira yake tayari likizo yake ya mwaka ilikuwa imeiva. Hii ina maana kuwa kipindi anachositishiwa ajira yake kama alikuwa hajaenda likizo basi atapata haki hiyo ya kulipwa likizo husika.
Mfano
Mfanyakazi anasitishwa ajira mwezi wa April 2018 na kwamba alipaswa kwenda likizo yake mwezi huo April au mwezi May 2018, basi kipindi cha kusitishwa ajira anayo haki ya kudai likizo husika.
- Gharama za Usafiri
Endapo mwajiri atasitisha ajira ya mfanyakazi ambaye alimwajiri eneo mbali na lile ambalo anamwachisha kazi basi anawajibika kumlipa gharama za usafiri na kusafirisha mizigo yake mpaka eneo aliloajiriwa. Upo uwezekano wa mfanyakazi kuwa sehemu nyingine mbali na kituo alichoajiriwa. Inapojitokeza hali hii mfanyakazi anayo haki ya kudai gharama za usafiri na usafirishwaji wa mizigo yake.
Mfano
Mfanyakazi ameajiriwa Dar es Salaam na kufanya kazi kwa muda kisha akahamishwa kituo cha kazi na mwajiri wake kupelekwa Mbeya. Akiwa Mbeya, mwajiri anamwachisha kazi. Hapa mfanyakazi ana haki ya kudai gharama za usafiri kutoka Mbeya kurudi Dar es Salaam.
- Haki nyingine ndani ya Mkataba
Zipo haki nyingine ambazo mfanyakazi anaweza kuwa nazo kwenye mkataba wake wa ajira. Haki hizi zinaweza zisiainishwe na sheria ya ajira lakini zinaonekana katika mkataba wa ajira. Mfanyakazi anayo haki ya kudai haki hizo ndani ya madai yake endapo litajitokeza zoezi la kusitishwa ajira.
Mfano
Katika mkataba wa ajira imeaishwa kuwa endapo kutatokea usitishaji wa ajira basi mwajiri atamlipa mfanyakazi ‘Mkono wa Heri’. Endapo kuna kipengele hiki au kingine chenye maslahi kwa mfanyakazi basi anayo haki ya kudai maslahi hayo.
Hitimisho
Ni muhimu sana kwa wafanyakazi kufahamu juu ya madai wanayoweza kudai linapojitokeza suala la kusitishwa kwa ajira yao. Ni muhimu kuzingatia aina ya madai ili kuepuka makosa au kuandika madai madogo kulinganisha na haki wanazostahili. Waajiri wazingatie juu ya haki wanazopaswa kuwalipa wafanyakazi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahali pa kazi
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.