Biashara Sheria.9. Usajili wa Biashara

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Ukurasa huu umekuwa mahsusi kwa ajili ya uchambuzi wa mambo mbalilmbali yanayomwezesha mtu au kikundi kuwa na namna bora ya kuanzisha na kuendesha shughuli zao za kibiashara kwa mujibu wa sheria. Leo tunakwenda kuangalia utaratibu wa kisheria wa kusajili biashara. Karibu tujifunze.

Usajili wa Majina ya Biashara

Majina ya biashara ili yawe halali na mtu au biashara iweze kuyatumia katika shughuli au biashara ni lazima yasajiliwe kwa mujibu wa sheria. Kuna biashara nyingi zinaendeshwa pasipo majina ya biashara au zina majina lakini majina hayo hayajasajiliwa.

Bunge la Tanzania lilitunga sheria maalum ya usajili wa majina ya biashara inayotambulika kama ‘The Business Names (Registration) Act, sura ya 213’. Katika sheria hii zimeainishwa taratibu za kisheria zinazomwezesha mtu, au wabia au kampuni kuweza kupata jina la biashara na kulisajili kisheria.

Sheria imeunda mamlaka maalum inayoshughulikia usajili wa majina ya biashara yaani ‘Business Registrations and Licensing Agency – BRELA’. Wakala huyu wa usajili anahusika na usajili wa majina ya biashara na kazi mbali mbali za kibiashara kwa Tanzania.

Sheria ya usajili wa majina ya biashara unazitaka biashara zote ili zitambuliwe kisheria kuwa ni halali lazima zisajiliwe.

Sheria hii inazitaka biashara kusajili majina ya biashara ndani ya siku 28 tangu kuanza kufanya biashara zao kwa kutumia majina hayo.

Utaratibu wa Usajili

Kabla ya maboresho ya mfumo wa TEHAMA usajili wa majina ya biashara ulimtaka muhusika kufika ofisi za BRELA na kujaza fomu maalum za usajili. Hatahivyo, kutokana na mabadiko ya mfumo wa kiteknolojia usajili wote kwa sasa unafanyika kwa njia ya mtandao.

BRELA kupitia website yake ya www.brela.go.tz inatoa maelekezo ya namna ya kupata au kusajili jina la biashara.

 

 

Faida za usajili wa jina la biashara

Zipo faida kadhaa za usajili wa jina la biashara ambazo mtu, wabia au kampuni unaweza kuzipata kutokana na usajili huo. Baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo;

  • Usajili wa jina la biashara unasaidia kuitambua biashara yako na kuitofautisha na biashara nyingine
  • Usajili unakusaidia uaminifu kwa wale unaofanya nao biashara kwamba hata mamlaka za kiserikali zinatambua biashara yako
  • Usajili wa jina la biashara inakusaidia katika mchakato wa kuifanya biashara yako itambulike kisheria na kuwa halali
  • Usajili unasaidia kuitangaza biashara yako

Hitimisho

Ni muhimu kwa mtu au wabia au kampuni kujua hatua na matakwa ya sheria ya usajili wa jina la biashara kwani ni kinyume cha sheria kutumia jina la biashara ambalo halijasajiliwa. Biashara itakayokutwa inaendeshwa pasipo usajili inaweza kushtakiwa na kulipa faini. Lazima tufahamu kuwa gharama za usajili wa biashara si kubwa bali gharama ya kutokusajili ni kubwa na inaweza kukuondolea imani kwa wale unaofanya nao biashara.

‘Sajili sasa jina la biashara yako upate uhalali wa kutoa huduma na kufanya biashara kisheria’

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili