Biashara Sheria.10. Je, Mkataba ni muhimu kwenye Biashara?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Ukurasa huu umekuwa mahsusi kwa ajili ya uchambuzi wa mambo mbalilmbali yanayomwezesha mtu au kikundi kuwa na namna bora ya kuanzisha na kuendesha shughuli zao za kibiashara kwa mujibu wa sheria. Leo tunakwenda kujifunza juu ya Umuhimu wa Mkataba wa kwenye Biashara. Karibu tujifunze.

Kisa cha Biashara ya mashine kuwa rehani

Nianze makala hii kwa kusimulia kisa cha kweli kilichomkuta mtu kuhusiana na biashara ya mashine kugeuka rehani. Katika kueleza kisa hiki nitatumia majina yasiyo halisi ingawa ni kisa cha kweli. Ndugu Juma alikuwa na mashine ya kukoboa nafaka akamuuzia kwa ‘maneno ya mdomo’ ndugu John kwa ahadi ya kulipa jumla ya Tsh.5,000,000/-. Wakati John anapokea ile mashine na kuondoka nayo alitoa kiasi cha Tsh.1,000,000/- kama malipo ya awali kwa ahadi ndani ya miezi 6 atamaliza kiasi kilichobaki. Haya yote waliyafanya wawili tu kwa maneno ya mdomo. John pamoja kuwa na mashine hakuanza uzalishaji wowote katika kipindi chote hicho cha miezi 6.

Ndugu Juma akaanza kudai fedha zake kiasi kilichobaki cha Tsh.4,000,000/- lakini John akagoma kulipa naye akabadili maneno kuwa yeye ndiye anamdai Juma kiasi cha Tsh.1,000,000/- aliyomkopesha na kuwa ile mashine ya kukoboa nafaka ilikuwa ni dhamana Juma ya kurudisha huo mkopo.

Mambo ya Kujifunza katika kisa hiki

Yapo makosa yaliyofanyika katika biashara hii ilivyofanyika kati ya Juma na John kuhusiana na uuzaji wa mashine ya kukoboa. Ndugu hawa kwa kuaminiana na kuishi kwa muda mrefu wakadhani kuwa si lazima sana kuandikisha mkataba juu ya kile wanachofanya biashara. Hii ni hali ya watu wengi sana katika kubadilishana vitu vya thamani.

Makosa

  • Juma kuamini kuwa katika makubaliano haya ya mdomo John atakuwa mwaminifu kutimiza ahadi yake kutokana na uhusiano wao
  • Pande zote kutokutumia mashahidi hata wa kusikia juu ya biashara waliyoifanya.
  • Kutokujali umuhimu wa kuandikishana juu ya msingi wa makubaliano yao

 

Umuhimu wa Mkataba

Kwa kusoma kisa hiki na kukielewa nandani tunaona juu ya umuhimu wa mkataba wa maandishi. Tusipuuze kabisa suala la kuandika katika makubaliano yetu yanayohusisha mbadilishano wa thamani. Tunaweza kudhani tunaaminiana lakini maisha hayako hivyo. Yapo hata mazingira ya mtu kutumia mashahidi wa kusikia, lakini hata hao mashahidi nyakati hizi si waaminifu wananunulika kwa ajili ya kudhulumu haki ya mtu.

Usidharau fedha yako au thamani ya kitu chako unachouza hata kama ni kwa fedha kidogo hakikisha una maandishi ambayo yatakusaidia endapo mambo hayataenda kama ulivyotarajia.

Hatua za kufanya

  • Kama unatarajia kuingia kwenye makubaliano ya kibiashara, hakikisha yanafanyika kwa maandishi
  • Kama umeshaingia kwenye makubaliano ya kibiashara ‘kwa mdomo’ basi wasiliana na mwenzako myaweke kwenye maandishi
  • Hakikisha una nakala zaidi ya moja zinazohusu makubaliano hayo ‘photocopy’
  • Tunza nyaraka zako za makubaliano sehemu salama ikiwezekana sehemu zaidi ya moja

‘Fanya biashara kisheria, hakikisha una makubaliano kwa maandishi’

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

1 reply

Comments are closed.