48. Makosa ya Utovu wa Nidhamu – Utoro Kazini

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika eneo mojawapo linalopelekea usitishwaji wa ajira ni Utovu wa Nidhamu yaani ‘misconduct’. Katika makala zilizopita tuliweza kuona nini maana ya utovu wa nidhamu na utaratibu unaoweza kutumika kuachisha kazi kwa utuvu wa nidhamu. Leo tunaanza kuangalia baadhi ya makosa yanayoweza kupelekea kusitishwa kwa ajira kutokana na utovu wa nidhamu. Karibu tujifunze.

Utovu wa Nidhamu

Utovu wa nidhamu maana yake ni kufanya mambo kinyume na mwongozo au tararibu za ajira sehemu ya kazi. Katika mahusiano ya kiajira baina ya mfanyakazi na mwajiri kuna mfumo wa mwenendo ambao unatarajiwa mfanyakazi auishi katika kutekeleza majukumu yake. Kutoka nje ya mfumo huo wa kimatendo kunasababisha makosa ambayo yanaonekana ni utovu wa nidhamu ‘misconduct’. Utovu wa nidhamu ni sababu mojawapo ambayo inakubalika kwa mujibu wa Sheria ya Kazi na Ajira kupelekea usitishwaji wa ajira endapo itathibitishwa na kufuata utaratibu wa haki.

Leo tunaanza kuangalia baadhi ya makosa ya utovu wa nidhamu yanayoweza kusababisha usitishwaji wa ajira ya mfanyakazi.

  1. Utoro kazini

Kumekuwa na tabia ya utoro kazini kwa wafanyakazi wengi sana. Wafanyakazi hawaji kazini pasipo na sababu au kutoa sababu za uongo za kuwafanya wasije kazini. Sheria ya Kazi na Ajira kupitia Kanuni za Utendaji Bora ‘Employment and Labour Relations (Code of Good Prictice)’ inaeleza kuwa

‘kutokuwepo kazini pasipo ruhusa au sababu ya msingi kwa zaidi ya siku 5 za kazi ni kosa linaloweza kusababisha kusitishwa ajira kwa utovu wa nidhamu’

Endapo mfanyakazi atashindwa kufika kazini kwa siku 5 basi mwajiri anayo haki ya kuanzisha mashtaka ya kinidhamu na ikithibitika kuwa mfanyakazi ametenda kosa hilo, mwajiri anaweza kusitisha ajira ya mfanyakazi husika.

Wapo wafanyakazi kwa visingizio vingi mara kwa mara wanashindwa kufika kazini au wanashindwa kutoa sababu za msingi za kuwafanya wasifike kazini.

Ni muhimu kufahamu kuwa suala la utoro kwa siku 5 za kazi si lazima ziwe mfululizo kama jumatatu – ijumaa inawezekana utoro huo ukawa wa vipindi vifupi vifupi kwa siku 2 au 3 kwa wiki kisha utoro wa siku nyingine 2 au 3. Tafsiri hii ilitolewa na Mahakama ya Kazi kwenye shauri la marejeo Na.48/2015 kati ya Bulyanhulu Gold Mine Ltd dhidi ya George Allen Gwabo, ambapo Mheshimiwa Jaji Mipawa aliona kuwa Mjibu Maombi  (George Allen) japo hakuwa mtoro wa siku 5 mfululizo lakini alikuwa na mtoro aliyejenga tabia ya utoro uliokithiri na hivyo ni sahihi kwa mwajiri kumwachisha kazi kwa sababu ya utoro.

Ili kuepuka changamoto hizi za utoro kazini inapaswa kuwepo na utaratibu  mahali pa kazi wa namna mfanyakazi anaweza kuufuata ili kupata ruhusa ya kutokufika kazini endapo kuna tatizo limejitokeza.

  • Uwepo wa daftari maalum la kuthibitisha uwepo wa mfanyakazi kazini. Siku hizi teknolojia imesaidia vipo vyombo vya kielekroniki vinavyoweza kutumiwa kuonesha ‘attendance’ ya mfanyakazi.

 

  • Uwepo wa kanuni zinazoweza kuongoza juu ya sababu za msingi ambazo mfanyakazi anaweza kuomba ruhusa ya kutokufika kazini.

 

  • Uwepo wa fomu maalum ambayo mfanyakazi anapaswa kuijaza ili kuomba ruhusa ya kutokufika kazini.

 

 

  • Kuthibitishwa kwa fomu husika na mwajiri au kiongozi wa eneo la kazi kwamba sababu inayotolewa ni ya msingi.

 

  • Mfanyakazi kuleta uthibitisho kulingana na sababu aliyoomba ruhusa. Mfano anaomba ruhusa ya kwenda hospital basi alete cheti cha daktari kikionesha mahali alipoenda kutibiwa, au anaenda safari basi alete tiketi zinazoonesha safari aliyoenda.

Hitimisho

Wafanyakazi wengi wanapenda kutumia mifumo dhaifu ya mwajiri na kusababisha tabia ya utoro wa kazi kukithiri sana. Ni dhahiri kwamba wafanyakazi wengi hawapendi kufanya kazi kwa uaminifu, kila wakati zipo sababu nyingi za kuwafanya wasifanye kazi au wasije kazini huku wakitaka kupata malipo pasipo kuzalisha. Ni muhimu sana kwa waajiri kuweka mfumo mzuri wa kudhibiti mwenendo wa wafanyakazi hasa tabia ya utoro kazini.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.