Mauzo ya Mali za Mirathi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunajifunza juu ya mauzo ya mali za mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Mali za Mirathi

Katika masuala ya usimamizi wa mirathi, eneo la mali ndilo linaibua changamoto kubwa sana ndani ya familia na jamii kwa ujumla. Iwapo marehemu aliacha mali basi wanaohusika na wasiohusika watajitahidi kuweka mazingira ya kunufaika na mali za marehemu huku wakiacha majonzi na kilio kwa warithi halali.

Katika makala ya leo tungependa kuangazia mojawapo ya swali ambalo tumelipokea kutoka kwa wasomaji wetu linalosema

Nini kinaweza kufanyika kisheria, endapo mmojawapo wa warithi au ndugu wa marehemu anauza mali za marehemu pasipo kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi?

Hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kwenye familia zetu za kiafrika ambazo nyingi hazina utaratibu wa kuandika wosia au kuweka mambo ya mali kisheria ili warithi wasije kubugudhiwa na ndugu au jamaa au marafiki.

Ipo mifano mingi kwenye jamii zetu mara baada ya mtu kufariki, ghafla mali zake zinaanza kuuzwa na wengine wanaanza kujichukulia kwa kadri wanavyoweza.

Ni muhimu kufahamu msimamo wa kisheria juu ya mali zilizoachwa na marehemu kuwa haziwezi kugawiwa au kuuzwa au kukodishwa  isipokuwa msimamizi wa mirathi amependekezwa na familia na kudhibitishwa na mahakama.

Hivyobasi, mauzo au namna yoyote ambayo mtu au mrithi anayofanya na mali ya marehemu bila kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ni BATILI.

Maana ya ubatili wa mauzo haya ni kama vile hayajawahi kufanyika kabisa.

Hatua za kuchukua

Endapo wewe ni mrithi au mwathiriwa wa vitendo vya ndugu au mrithi mwenzako kuuza mali za marehemu pasipo kuwa na usimamizi wa mirathi basi chukua hatua zifuatazo;

  1. Itisha kikao cha familia au ukoo mara moja

Hii ni hatua ya kwanza ambayo unaweza kufanya endapo marehemu aliacha mali pasipo wosia. Itisha kikao cha wanandungu na kupendekeza majina ya wasimamizi wa mali ya marehemu. Katika kikao hicho kitaonesha wajumbe na hata mali za marehemu na uandaliwe muhtasari wa kikao husika.

  1. Fungua shauri la mirathi

Mara baada ya kuitishwa kikao cha wanandugu, fungua shauri la kuteuliwa msimamizi wa mirathi katika mahakama ya mwanzo mahali alipokuwa akiishi marehemu. Sheria za Mirathi zinataka utaratibu wa mtu kuteuliwa usimamizi wa mirathi udhibitishwe na mahakama kisheria. Wengi wanaishia kuteuliwa na kikao cha kifamilia na kuanza majukumu ya usimamizi wa mirathi, hii ni kinyume cha sheria na yote anayofanya msimamizi pasipo kuidhinishwa na mahakama ni batili kisheria.

Unapofungua shauri la mirathi utaorodhesha mali zote za marehemu ikiwa ni pamoja na zile ambazo zimeuzwa au zimekodishwa mara baada ya marehemu kufariki na kabla ya uteuzi wa usimamizi wa mirathi.

  1. Fungua shauri dhidi ya muuzaji na wanunuzi wa mali ya mirathi kwenye mahakama husika

Mara baada ya kuteuliwa usimamizi wa mirathi, na kuidhinishwa na mahakama, msimamizi anakuwa na uhalali wa kisheria kuhusiana na mali zote za marehemu. Msimamizi anaweza kufungua mashauri ya madai dhidi ya mtu aliyeuza mali za marehemu pamoja na walionunua. Lazima ifahamike kuwa wajibu mkubwa alionao msimamizi wa mirathi ni kukusanya mali za marehemu, kulipa madeni na kugawa kwa warithi halali. Katika kukusanya mali za marehemu, msimamizi anao wajibu wa kufuatilia kila mali ya marehemu ikiwezekana kufungua mashauri ya kisheria dhidi ya mtu yeyote au taasisi yoyote iliyouza mali au kununua mali ya marehemu.

  1. Fungua shitaka la jinai dhidi ya muuzaji

Msimamizi anayo haki na wajibu wa kufungua hata mashitaka ya kijinai dhidi ya muuzaji au mtu aliyejipatia mali za marehemu kwa njia za udanganyifu. Kisheria msimamizi wa mirathi anasimama katika miguu ya marehemu hivyo matendo yake yanahesabika kama ni matendo ya marehemu yaani anafanya kwa niaba yake. Hivyo anatarajiwa kuilinda mali ya marehemu kama vile marehemu angefanya mwenyewe.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa watu wote na jamii kuzingatia na kujiepusha kujinufaisha na mali za marehemu pasipo kuzingatia utaratibu wa kisheria. Ni rai yangu kwa wanunuzi wa viwanja, mashamba, au magari au mashine mbalimbali zinazohusishwa na mirathi kuwa makini. Ni lazima ujiridhishe uhalali wa muuzaji endapo ni msimamizi halali na anacho kibali cha kisheria kufanya mauzo au kuingia makubaliano ambayo mnataka kuingia, kinyume na hapo ni hasara mbele endapo sheria itachukua mkondo wake.

Nitoe rai kwa wale waathiriwa wa matendo ya watu wasio waaminifu katika mali za marehemu, kuchukua hatua kama nilivyopendekeza katika makala hii. Hatahivyo, ni vyema kwetu wote kwa kuwa ni ‘marehemu watarajiwa’ kuchukua hatua ya kuandika wosia ili warithi wetu wasikumbwe na changamoto husika.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

 ‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na uwakilishi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com