49. Hatua za kuchukua kushughulikia Utoro Kazini

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tuliona juu ya mojawapo ya sababu ya mfanyakazi kuweza kuachishwa kazi ni suala la Utoro Kazini. Leo tunaangalia ‘Hatua za Kuchukua kushughulikia Utoro Kazini’. Karibu tujifunze.

Namna ya kushughulikia Utoro kazini

Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya uwezekano wa kusitishwa ajira ya mfanyakazi kwa kosa la utoro kazini. Tumeona kuwa kukosekana mfanyakazi kufika kazini kwa siku 5 kunaweza kusababisha kusitishwa kwa ajira yake kwa utovu wa nidhamu. Siku hizo 5 si lazima ziwe mfululizo bali zinaweza kuwa zimejikusanya kutoka wiki kadhaa au miezi.

Sheria ya Kazi na Ajira kupitia Kanuni za Utendaji Bora ‘Employment and Labour Relations (Code of Good Prictice)’ inaeleza kuwa

‘kutokuwepo kazini pasipo ruhusa au sababu ya msingi kwa zaidi ya siku 5 za kazi ni kosa linaloweza kusababisha kusitishwa ajira kwa utovu wa nidhamu’

Hivyobasi, katika makala hii tunakwenda kuona njia au mbinu mwajiri anazoweza kutumia kushughulikia suala la utoro kazini.

  1. Uwepo wa mkataba wa maandishi

Ili mwajiri awe na nafasi nzuri ya kushughulikia suala la utovu wa nidhamu katika utoro kazini ni vyema akawa na mkataba wa maandishi. Ndani ya mkataba huo, mojawapo ya vipengele vitakavyoainishwa kwa pande zote kuzingatia ni suala la muda wa kuanza kazi na muda wa kumaliza kazi. Pia mkataba ni lazima uoneshe siku za kazi ni ngapi katika juma. Hii itamsaidia mwajiri kama rejea endapo tabia ya utoro kazini kwa mfanyakazi itakithiri.

  1. Uwepo wa daftari maalum la kuthibitisha uwepo wa mfanyakazi kazini.

Kama tulivyoeleza katika makala iliyopita njia moja wapo ya kudhibiti utoro kazini ni uwepo wa daftari maalum. Katika nyakati hizi zilizoendelea siku hizi wafanyakazi wanajisajili kila siku kwa kutumia alama za vidole kwenye mashine za kielektroniki. Hii inasaidia kupunguza udanganyifu wa wafanyakazi kuweka saini kwa niaba ya wengine.

  1. Anza kuchukua hatua za kuonya kwa mdomo na kisha kwa maandishi.

Ni lazima mwajiri atambue kuwa jukumu la kudhibitisha endapo mfanyakazi ni mtoro au la lipo upande wake. Hivyo panapojitokeza utoro basi ni vyema mwajiri kuchukua hatua za awali za kumwonya mfanyakazi kwa mdomo na endapo tabia hiyo itaendelea basi amwandikie barua ya onyo ikiwa ni onyo la kwanza, la pili hata la tatu. Muhimu kuandika ili kutunza kumbukumbu za tabia za wafanyakazi.

  1. Sitisha ajira ya mfanyakazi baada ya kikao cha kinidhamu

Sheria ya Ajira inataka kuwa mashitaka dhidi ya mfanyakazi juu ya utovu wa nidhamu yafanyike kwanza kabla ya mfanyakazi kusitishiwa ajira yake. Endapo tabia hii itakithiri, mwajiri anao wajibu wa kuandaa mashtaka ya kinidhamu dhidi ya mfanyakazi kwa kosa la utoro na mfanyakazi atapewa nafasi ya kujitetea kama mwongozo wa kisheria juu ya mashtaka ya kinidhamu yanavyotaka. Ikidhibitika kuwa tabia hiyo imekithiri mwajiri anayo haki ya kusitisha ajira ya mfanyakazi.

Hitimisho

Ni jukumu la mwajiri kuwa na kumbukumbu zote zinazohusiana na mfanyakazi ikiwa ni mkataba, utendaji wake na mwenendo wa tabia yake mahali pa kazi. Waajiri wengi wanashindwa kuchukua hatua dhidi ya wafanyakazi au wanachukua hatua kinyume cha sheria kwa sababu ya kukosa umakini wa kuwa na kumbukumbu sahihi kuhusiana na mfanyakazi husika. Ni dhahiri kuwa endapo mfanyakazi atapinga kusitishwa ajira yake mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, ni jukumu la mwajiri kuthibitisha kuwa usitishaji wa ajira ulikuwa na sababu za msingi na ulifuata utaratibu wa haki kama sheria ya ajira inavyoelekeza.

Ni rai yangu kwa waajiri kuweka kumbukumbu sahihi za wafanyakazi ili waweze kuchukua hatua zinazostahili endapo suala la kinidhamu litajitokeza.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com