Kisa Mkasa.1: Emmanuel Didas vs MOI

Utangulizi

Visa na Mikasa Mahakamani ni ukurasa mpya na maalum kwa wasomaji wetu wa Uliza Sheria mtandao unaokupa fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya kisheria na namna ya kukabiliana na changamoto za kisheria. Visa na Mikasa Mahakamani ni ukurasa maalum unaokuletea matukio ya kweli kabisa ambayo yametokea katika mashauri mbalimbali yaliyofikishwa mahakamani kupata utatuzi wa kisheria. Watu wengi wamekuwa na matukio ambayo wangeweza kudai haki zao na kuzipata lakini kutokufahamu au uwezo wa kuchukua hatua unakuwa hafifu. Hapa utapata fursa ya kujifunza kwa mifano halisi kwa matukio halisi yaliyojitokeza. Karibu sana ufuatane nasi katika Visa na Mikasa Mahakamani.

Uzembe: Operesheni ya kichwa badala ya mguu – Kisa cha Emmanuel Didas

Tarehe 1 mwezi Novemba 2007 tasnia ya matibabu ilikumbwa na tukio kubwa lililotikisa nchi nzima kwa kisa cha raia wawili ambao walifanyiwa upasuaji kitengo cha mifupa MOI (Muhimbili) tofauti na mahitaji yao ya kimatibabu. Hiki ni kisa kilichowahusu ndugu Emmanuel Didas na Emmanuel Mgaya. Kisa hiki kinaeleza kuwa Emmanuel Didas alifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha Mifupa (Muhimbili Orthopedic Institute –MOI) kutokana na kupata ajali ya pikipiki mnamo tarehe 26 Oktoba 2007 ambayo ilimletea shida kwenye mguu kwa upande mwengine Emmanuel Mgaya alifikishwa hospitali hiyo kwa sababu ya uvimbe kichwani. Changamoto kwa wagonjwa hawa ilijitokeza pale kwenye chumba cha upasuaji ambapo Emmanuel Didas aliyekuwa na tatizo la mguu akafanyiwa upasuaji wa kichwa na Emmanuel Mgaya aliyekuwa na tatizo la kichwa akapasuliwa mguu.

Kutokana na tatizo hili wagonjwa hawa walipata madhara kiasi kilichopelekea uongozi kuunda Tume ya kitaaluma kuchunguza endapo kulikuwa na uzembe katika kushughulikia matibabu yao. Pia katika kurekebisha hilo uongozi ulifanya mpango wa kumsafirisha mgonjwa huyo nchini India kwa matibabu zaidi. Tarehe 22/11/2007 mgonjwa Emmanuel Mgaya alifariki wakati Emmanuel Didas aliendelea na matibabu lakini changamoto za kiafya ziliendelea. Emmanuel Didas aliendelea na matibabu MOI baada ya kutoka Hospital ya Appollo India mpaka mwaka 2009 alipopewa ruhusa ya kutoka hospitali.

Ndugu Emmanuel Didas baada ya kumaliza matibabu alijaribu kuwasilisha madai yake kwa Uongozi wa Hospital ya Muhimbili lakini hakufanikiwa hivyo rasmi aliamua kufungua kesi ya madai ya madhara aliyopata kutokana na uzembe uliojitokeza wakati wa matibabu yake.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam ndiyo ilikuwa na jukumu la kuamua kwenye shauri hili la Madai Na.129/2012 kati ya Emmanuel Didas dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya MOI na wenzake 2. Katika shauri hili kutokana na hali ya kiafya ya Emmanuel Didas utaratibu wa kisheria ulitumika kwa ndugu yake kufungua shauri kwa niaba yake ambaye anaitwa Sisti Marishay.

Ndugu msomaji taarifa hizi za uzembe uliojitokeza katika kitengo cha MOI mnamo mwaka 2007 zilikuwa taarifa zilizoshtua sana watu wengi na kutilia mashaka juu ya huduma ambazo zilikuwa zinatolewa. Hatahivyo, si watu wengi waliopata fursa ya kufahamu nini kiliendelea baada ya tukio lile.

Endelea kufuatilia Kisa na Mkasa huu Mahakamani ili uweze kujifunza zaidi na kufahamu haki za kisheria unazoweza kuzidai pindi zinapojitokeza changamoto kama hizi au nyinginezo.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili wa dunia (Global Advocate)