6. Wadau wa Sheria za Barabarani – Wanaochunga wanyama

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Barabara kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Ukurasa huu maalum unakuletea uchambuzi wa Sheria mbalimbali zinazohusiana na barabara. Kila siku kuna matukio mengi sana yanaendelea barabarani, lakini si watu wengi wanaojua taratibu zinazopaswa kuchukuliwa ili kushughulikia matukio hayo. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Waendesha Baiskeli kuhusu wajibu wao wa kuzingatia sheria za barabarani. Leo tunaendelea  kuangalia  kama wadau wa Sheria za Barabarani kwa wanaochunga wanyama. Karibu tujifunze.

Wadau wa Sheria za Barabara: Wanaochunga wanyama

Kama walivyo makundi mengine ya watumiaji wa barabara, wanaochunga wanyama pia ni wadau ambao wamekuwa na matumizi makubwa ya barabara. Tumeshuhudia sehemu nyingi mifugo imekuwa ikitumia barabara aidha kuvuka au kuzagaa maeneo ya barabara.

Pamoja na kuwa wanaochunga mifugo  haubanwi na masharti mengi ya matumizi ya barabara, bado watumiaji hao wanao wajibu mkubwa katika matumizi ya barabara ili waweze kujilinda wao na watumiaji wengine wa barabara.

Changamoto inayowakumba wanaochunga mifugo maeneo ya vijijini na hata mijini endapo mifugo hiyo kwa njia moja ama nyingine itahusika na kuvuka barabara au kuwa kando ya barabara ni ukosefu wa udhibiti wa mifugo husika

Mambo ya msingi kuzingatia

  • Udhibiti wa mifugo; ni lazima Yule anayehusika kuchunga mifugo awe na udhibiti wa wanyama hao, mfano: ng’ombe, mbuzi, kondoo, nk haijalishi idadi ya wanyama muhimu sana ni lazima kuwe na udhibiti
  • Idadi ya wadhibiti; pindi wanyama watakapokuwa wengi basi inapendekezwa kuwa na wadhibiti wanyama zaidi ya mmoja ili kufanya kazi hiyo kwa usahihi zaidi.
  • Taadhari; kwenye kona kali mmoja awe mbele zaidi ili kuonya watumiaji wengine wa barabara waweze kuitumia kwa taadhari
  • Kibali cha Polisi; lazima uwe na kibali cha Polisi kama unataka kuchunga wanyama zaidi ya 50 kwenye barabara yoyote au mtaa.

Hitimisho

Wachunga wanyama ni wadau wengine katika utekelezaji wa matakwa ya sheria za barabarani. Wadau hawa kama wengine wengi wanalo jukumu muhimu sana katika kuzifahamu sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali pindi wanapokuwa wakitumia barabara. Kila mmoja anao wajibu wa kufahamu ni nini anapaswa kukifanya anapokuwa barabarani ili kuepusha ajali na matumizi mabaya ya barabara.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya barua pepe info@ulizasheria.co.tz

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili