5. Wadau wa Sheria za Barabarani – Waendesha Baiskeli

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Barabara kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Ukurasa huu maalum unakuletea uchambuzi wa Sheria mbalimbali zinazohusiana na barabara. Kila siku kuna matukio mengi sana yanaendelea barabarani, lakini si watu wengi wanaojua taratibu zinazopaswa kuchukuliwa ili kushughulikia matukio hayo. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Waenda kwa Miguu kuhusu wajibu wao wa kuzingatia sheria za barabarani. Leo tunaendelea  kuangalia Waendesha Baiskeli kama wadau wa Sheria za Barabarani. Karibu tujifunze.

Wadau wa Sheria za Barabara: Waendesha Baiskeli

Kama walivyo makundi mengine ya watumiaji wa barabara, waendesha baiskeli pia ni wadau ambao wamekuwa na matumizi makubwa ya barabara. Tumeshuhudia sehemu nyingi usafiri wa baiskeli umekuwa ukitumiwa na watu wengi katika kusafiri au kusafirisha mizigo na bidhaa mbalimbali.

Pamoja na kuwa usafiri wa baiskeli hauna haubanwi na masharti ya usajili kama yalivyo magari au pikipiki, bado watumiaji wa baiskeli wanao wajibu mkubwa katika matumizi ya barabara ili waweze kujilinda wao na watumiaji wengine wa barabara.

Changamoto nyingine ambayo inawakumba waendesha baiskeli, ni kutokuwepo mfumo wa kuthibitisha uwezo au umahiri wa uendeshaji wa baiskeli. Kila mmoja anajifunza kwa namna yake na hatimaye huendesha baiskeli hiyo kwenye maeneo ya barabara. Hali hii inasababisha ukosefu maarifa sahihi na kuzingatia sheria za msingi za barabarani.

Mambo ya msingi kuzingatia

  • Fuata sheria za barabarani; mwendesha baiskeli anapaswa kuwa na ufahamu wa sheria za barabarani zinazofuatwa na madereva wengine kama gari au pikipiki. Mwendesha baiskeli anapaswa kufahamu ishara za barabara, michoro na maelekezo yaliyopo barabarani ili kuweza kuwa na matumizi sahihi.
  • Baiskeli iwe katika hali nzuri; ile kwamba chombo hiki hakikaguliwi na askari barabarani haimaanishi kiwe na upungufu. Baiskeli inatakiwa iwe na taa zinazofanya kazi, matairi yenye upepo, breki na gea zinazofanya kazi, mnyororo uliowekwa vizuri, kengele n.k
  • Matumizi ya Kengele; namna ambayo mwendesha baiskeli anaweza kuwasiliana na watumiaji wengine wa barabara ni kuwa na matumizi sahihi ya kengele. Inatarajiwa kila baiskeli iwe na kengele ili kutoa ishara kwa watumiaji wengine wa barabara.
  • Vifaa vya usalama na mavazi; mwendesha baiskeli anapaswa kutumia helmet na mavazi ya kujikinga mwili wake vizuri. Mwendesha baiskeli anawajibika kuwa na mavazi ambayo yatasaidia kuonekana kwake kwa urahisi endapo anatumia baiskeli.

Mambo ya kuzingatia Unapoendesha baiskeli

  • Weka mikono yote miwili kwenye usukani isipokuwa wakati wa kutoa ishara
  • Weka miguu yote miwili kwenye pedeli
  • Usijishikilie kwenye magari au au pikipiki au baiskeli nyingine
  • Usiendeshe ukiwa karibu nyuma ya gari
  • Usibebe abiria isipokuwa kama baiskeli yako imetengenezwa kubeba abiria mmoja
  • Usibebe kitu chochote kitakachokupa ugumu wa kuendesha baiskeli
  • Endesha upande wa kushoto wa barabara karibu na ukingo

Mambo ambayo hutakiwi kufanya uwapo barabarani

  • Kuendesha kwa speed kali; mara nyingine waendesha baiskeli wanaenda mwendo mkali sana na kuhatarisha maisha yao na watumiaji wengine wa barabara. Inatakiwa kuwa na mwendo wa wastani ambao unaweza kumudu.
  • Kuendesha kwa kelele;  watumiaji wengine wa baiskeli wanatumia kengele vibaya au wanapokosa kengele hupika kelele nyingi barabarani. Hii ni hatari kwa watumiaji wengine wa barabara ambao hushindwa kutafsiri ishara zinazotolewa nao.
  • Kutokuendesha eneo la waenda kwa miguu; imekuwa ni utamaduni kwa waendesha baiskeli kuona wana haki ya kuendesha baiskeli kila mahali hata maeneo yaliyotengwa kwa waenda kwa miguu. Hali hii imekuwa ikisababisha ajali mbalimbali. Kama unaendesha baiskeli basi hakikisha unaendesha katika eneo la barabara au eneo maalum la baiskeli na si maeneo ya waenda kwa miguu.

Hitimisho

Waendesha baiskeli ni wadau muhimu sana katika utekelezaji wa matakwa ya sheria za barabarani. Wadau hawa kama wengine wengi wanalo jukumu muhimu sana katika kuzifahamu sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali pindi wanapokuwa wakitumia barabara. Kila mmoja anao wajibu wa kufahamu ni nini anapaswa kukifanya anapokuwa barabarani ili kuepusha ajali na matumizi mabaya ya barabara.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e- mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040. Tafadhali tuma ujumbe wa sms au watsup au ujumbe wa sauti.

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako              

Isaack Zake, Wakili