60. Ufanye nini endapo umekatwa mshahara bila utaratibu?


Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeweza kujibu swali juu ya mamlaka ya mwajiri kumkata mfanyakazi mshahara pasipo utaratibu. Leo tunakweda kujibu swali ya kwamba nini mfanyakazi anaweza kufanya endapo atakatwa mshahara pasipo utaratibu. Karibu tujifunze.

Hali ya Wafanyakazi

Wafanyakazi wengi wanaokutwa katika adha ya kukatwa mishahara au kuzuiliwa mishahara yao na waajiri wanabaki na hali ya kulalamika tu pasipo kuchukua hatua mapema. Uzoefu unaonesha mfanyakazi anaweza kuendelea kufanya kazi katika mazingira hayo ya mapunjo au kukosa kabisa mshahara ili mradi tu aendelee kuwa kazini. Wapo wafanyakazi wanadai mishahara hadi ya mwaka mzima na zaidi kwa mwajiri na hawajachukua hatua yoyote.

Ni muhimu mfanyakazi kufahamu ya kuwa mshahara ni haki yake endapo amefanya kazi katika kipindi husika. Mfanyakazi anapaswa kujua hatua za kuchukua ili kuweza kudai haki yake ndani ya muda wa kisheria.

Mambo ya Msingi ya Mfanyakazi kufanya ili kudai mishahara

  1. Kutambua muda wa ukomo wa madai ya mishahara

Sheria ya Ajira imeweka ukomo juu ya madai ya haki mbalimbali zinazopatikana ndani ya sheria. Upande wowote hauwezi kwenda mbele ya Tume kwa muda unaotaka wenyewe bali unaongozwa na sheria. Sheria ya ajira inaeleza wazi kuwa ukomo wa madai juu ya mishahara ni siku 60. Mfanyakazi anapaswa kuchukua hatua za kudai mwajiri ndani ya siku 60 endapo mshahara wake umekatwa au kutokulipwa. Wafanyakazi wengi hawachukui hatua mapema na wanaacha madeni dhidi ya mwajiri kulimbikizwa kitu ambacho kinaweza kusababisha kukosa kwa haki yao. Ni muhimu sana kuzingatia muda wa kisheria ili uweze kudai madai ya mishahara ndani ya muda.

2. Kuchukua hatua za kudai kwa maandishi

Ni wafanyakazi wachache sana wenye ujasiri wa kuweza kuwaandikia waajiri wao madai yao. Wafanyakazi wengi ni waoga au hawana ujasiri wa kueleza kwa maandishi kile wanachomdai mwajiri. Endapo mshahara wako au malipo yako yoyote yatapunguzwa au utayakosa basi chukua hatua ya kuandika kwa mwajiri ili aweze kutoa ufafanuzi au kulipa madai hayo mapema. Wafanyakazi wengi wana hofu ya kwamba wakichukua hatua hiyo basi kuna uwezekano wa ajira yao kusitishwa. Mwajiri makini hawezi kusitisha ajira yako kwa kigezo cha kuulizia haki zako. Ni muhimu kutumia njia hiyo kwani itakuwa sababu na ushahidi kuwa ulichukua hatua mapema.

3. Kufungua shauri Tume

Endapo mwajiri anaonesha hana nia ya kukulipa madai yako ya mshahara basi hatua nyingine unayoweza kuchukua ni kufungua mgogoro mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi. Mgogoro huu wa madai ya mshahara ni lazima ufunguliwe ndani ya siku 60 tangu mwajiri kuvunja haki yako. Tume itasikiliza mgogoro huo na kutoa uamuzi kama inavyostahili. Eneo hili pia wafanyakazi wanakuwa waoga kumfungulia shauri mwajiri ili hali bado yupo kazini. Ni muhimu kufahamu kuwa mwajiri anaporuhusiwa kuvunja haki yako kidogo kidogo basi unaweza kujikuta hata unasitishwa ajira yako pasipo kufuata utaratibu wa kisheria.

4. Kujiuzulu kazi

Hii ni hatua ngumu sana kwa mfanyakazi kuichukua lakini hana budi kuichukua inapobidi kufanya hivyo. Endapo mwajiri atakataa kwa muda mrefu kukulipa mishahara yako basi unaweza kuandika barua ya kuacha kazi na kisha kufungua shauri mbele ya Tume. Aina hii ya kujiuzulu si kwa hiyari yako bali mazingira yaliyotengenezwa na mwajiri kwa kutokukulipa mishahara na madai yako imepelekea wewe kujiuzulu. Unaweza kufungua shauri husika na kudai fidia dhidi ya mwajiri kwa kusababisha ujiuzulu kazi.

Hitimisho

Kama tulivyoona katika mfululizo wa makala hizi mbili ya kwamba si haki kwa mwajiri kuzuia mshahara au kufanya makato ya mshahara wa mfanyakazi pasipo sababu za msingi za kisheria. Pia mfanyakazi hupaswi kusubiri haki hii endapo itavunjwa unapaswa kuchukua hatua mapema ili kuepusha hasara kubwa utakayopata endapo utachelewa kuwasilisha malalamiko yako mbele ya Tume ndani ya muda.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com