Maeneo ya Kutunza Wosia

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo tunaendelea kujifunza na mfululizo wa makala zinazohusu masuala ya mirathi. Karibu tujifunze kwa pamoja.

Uandishi wa Wosia

Kama tulivyozungumza katika makala mbalimbali ambazo tumeangalia masuala ya mirathi, wosia umejitokeza kama hitaji muhimu kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua na kuandaa.

Wosia inahusisha tamko au andiko la mwosia juu ya mali zake, madeni na namna ambavyo angependa maziko yake yafanyike mara baada ya kifo chake.

Kwa hatua mbali mbali na mada ambazo tumezijadili, tumeweza kuona kwa sehemu kubwa jamii yetu ya Kiafrika, hususani watanzania hatuna kawaida ya kuandaa wosia juu ya mali zetu. Hii imeibua changamoto na mashindano yasiyoisha kwenye koo na familia kila kukicha.

Ni muhimu tu kusisitiza kwamba ukitaka familia yako waweze kunufaika na jasho lako yaani mali ulizochuma mara baada ya wewe kuondoka hapa duniani basi huna budi kuandaa wosia. Andishi la wosia ni jambo rahisi linaweza kufanywa na mtu yeyote. Hata hivyo kwa ushauri na namna bora wasiliana na wanasheria ili wakuongoze kuandaa wosia vizuri.

Mahali pa kutunza wosia

Kama ilivyo muhimu kuandaa wosia ni vyema pia kujua namna ya kuutunza wosia. Kwa kuwa wosia ni nyaraka muhimu sana katika maisha ya mtu na inabeba sauti ya muhusika baada ya kifo chake ni vyema ukatunzwa vizuri na mahali ambapo itakuwa rahisi kupatikana mara baada ya kifo cha muhusika.

Wapo watu ambao waliandika wosia wao lakini kwa kutokujua mahali pa kuifadhi hata walipofariki wosia wao haukuonekana au haukupatikana. Ni wazi kufahamu mwosia mara baada ya kifo chake hawezi kuelekeza mahali wosia ulipo bali wale waliokabidhiwa ndio wana wajibu wa kuutoa wosia ili warithi waweze kufahamu juu ya kile mwosia alichowausia.

Yapo maeneo kadhaa yanafahamika kisheria kuwa sehemu salama ya kutunza wosia wa marehemu.

  1. Ndugu au rafiki ambaye mwosia anamwamini

Mwosia mara baada ya kuandaa wosia wake wa mwisho anaweza kuutunza kwa rafiki yake au ndugu yake anayemwamini. Katika mahusiano na watu wapo wale ambao tunajua kuwa wanatutakia mema hata baada ya sisi kuondoka wanaweza kuchukua wajibu wa kuiangalia familia. Ni muhimu kuwa na mtu unayeweza kumwamini na kumwachia nakala halisi ya wosia wako. Hii haimaanishi mtu huyo awe mtekeleza wosia bali anaweza tu kuitunza nakala na mara baada ya kifo chako kuiwasilisha kwa warithi.

  1. Nyumba ya ibada ya mwosia

Eneo lingine ambalo mwosia anaweza kuacha wosia wake ni eneo ambalo anashiriki imani yake. Hii kwa tamaduni inaweza kuwa kanisani au msikitini pale ambapo mwosia anashiriki ibada. Zipo taratibu za nyumba za ibada katika namna ya kuhifadhi nyaraka muhimu kama hizi ambapo zitatunzwa kwa usalama na mara baada ya kifo cha mwosia basi wosia huo unaweza kupelekwa kwa warithi husika.

  1. Mwanasheria

Mwosia anaweza kuacha wosia wake pia kwa mwanasheria wake kulingana na makubaliano yao. Hii itasaidia pia endapo mwosia anafariki basi warithi wataweza kupokea wosia huo kutoka kwa mwanasheria wa mwosia.

  1. Mahakama

Pia wapo ambao wanaandaa wosia wao na kuuweka mahakamani katika eneo ambalo wanaishi. Hii ni sehemu nyingine kwa kufuata taratibu mwosia anaweze kuifadhi wosia wake na kuwa na uhakika kwamba wosia wake utafikishwa kwa warithi wakati mwafaka mara baada ya kifo chake.

  1. Wakala wa Usajili

Sote tunafahamu kuwa nchi yetu ina wakala wa usajili juu ya masuala mbali mbali mfano vizazi, ndoa, talaka, na vifo. Wakala wa usajili yaani RITA ina ofisi katika kila wilaya nchini. Mwosia anayo fursa ya kuandaa waraka wake juu ya mali zake na kuutunza kwa wakala wa usajili.

Haya ni maeneo ambayo mwosia anaweza kutunza wosia wake na ukapatikana mara baada ya kifo chake. Kila mwosia anaweza kutumia kati ya njia hizo angalau tatu kwa pamoja ili kuondoa tashwishi kwa warithi endapo wosia husika ni halali au la.

Mwosia ni vyema kuepuka kuacha wosia kwa mmoja wa warithi kwani mara nyingi huibua changamoto ya kuonekana kuwa labla wosia husika umechezewa.

Hitimisho

Ndugu msomaji katika mfululizo huu wa makala hizi za mirathi naamini umejifunza mambo mengi ya msingi ambayo yatakupa mwanga wa kuchukua hatua zinazostahili. Mfululizo wa makala hizi ni kukuonesha japo kwa uchache matatizo yanayowakumba wengi katika familia na jamaa kwa kutokuchukua hatua zinazostahili kabla ya kifo yaani kuandika wosia.

Ni rai yangu tena kwako sasa kuchukua hatua mapema ili kuepuka warithi wako kuingia katika mgogoro ambayo mingi ya hiyo imesababisha mauaji, utengano na chuki dhidi ya ndugu wa kuzaliwa kwa sababu ya mali zilizoachwa na marehemu.

Katika kumalizia makala hii ambayo inahitimisha mwaka huu 2017 na kufikisha makala 100 za ukurasa wa Sheria Leo nimekumbuka wimbo mmoja wenye kionjo kinachosema ‘tunatoana roho, yarabi kwa mali alizoacha baba’ huu ni ujumbe madhubuti wa kuufanyia kazi. Nakutakia mwisho mwema wa mwaka 2017 na maandalizi bora ya 2018.

‘Andika wosia sasa, maadam unaishi leo’

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Karibu darasa la sheria DARASA LA ULIZA SHERIA 2018 

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Edward Scynia Makaranga
    Edward Scynia Makaranga says:

    Hii Makala ninzuri sana. Pia nimuhimu sana Watanzania tunapaswa kujijengea utamadani wakuandaa wosia pindi tungali hai ili tutakapokua tuondoka hapa duniani tuache mazingira mazuri wanandugu wasije kugombana.

Comments are closed.