Sheria Leo. Usijichukulie Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Leo ni siku njema kabisa katika kuanza mwaka huu mpya wa 2018. Lengo la ukurasa huu ni kuendelea kutoa maarifa ya kisheria yanayokusaidia wewe msomaji kila siku. Tunapenda kukualika tena katika mwaka huu kuendelea kuwa nasi katika mtandao wako wa Uliza sheria. Karibi tujifunze.

Maisha kwa Mujibu wa Sheria

Tangu kuanzishwa kwa mtandao huu wa uliza sheria kupitia ukurasa wa Sheria Leo tumekuwa tukijifunza na kuweka msisitizo katika maisha kwa mujibu wa sheria. Kama tunavyofahamu sheria ni kanuni ambazo zinatawala mwenendo wa maisha ya mwanadamu katika eneo Fulani. Mfumo huu wa sheria upo duniani kote kila nchi ina utaratibu wake wa kutawala wananchi na watu wote wanaofanya shughuli katika nchi husika.

Tanzania ni miungoni mwa nchi hizo ambazo zina mfumo wa sheria ambao unaweka mamlaka mbalimbali za nchi na kutawala shughuli zote za wananchi na wakaazi wa nchi hii.

Ni muhimu kufahamu kuwa wananchi wote na wakaazi wote walio raia au sio raia wa nchi hii wanao wajibu mkubwa wa kuishi kwa mujibu wa sheria za nchi. Wajibu huu unapaswa kutekelezwa na watu wote pasipo kujali jinsia, kabila, dini, rangi, asili au nasaba au tofauti yoyote ile inayoonekana katika jamii. Sisi zote tupo chini ya utawala wa sheria na tunao wajibu wa kuishi kwa mujibu wa sheria.

Dhana ya Kujichukulia Sheria Mkononi

Katika siku za hivi karibuni kumeongezeka wimbi kubwa la wananchi kujichukulia sheria mkononi yaani kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuadhibu watu wengine pasipo kufuata sheria.

Maana ya kujichukulia sheria mkononi ni ile hali ya mtu kuchukua hatua fulani ikiwa ni kuadhibu au kutekeleza vitendo fulani dhidi ya mtu au kitu cha mtu mwengine pasipo kufuata taratibu za kisheria.

Dhana hii imeshika kasi sana katika siku hizi yaani watu hawako tayari kufuata utaratibu wa kisheria kushughulikia changamoto kadhaa ndani ya jamii.

Mfano mkubwa ambao umekuwa ukijirudia kila kukicha ni hatua zinazochukuliwa na wananchi ‘wenye hasira kali’ dhidi ya wahalifu kwenye matukio ya uhalifu. Imezoeleka sasa ndani ya jamii kwamba mwizi akikamatwa basi adhabu yake ni kifo tena kwa kuchomwa moto. Suala hili limeshika kasi si katika maeneo ya miji tu bali hata maeneo ya vijijini.

Labda nieleze wazi kuwa sina maslahi wala sishawishi vitendo viovu katika jamii yetu kwani hakuna anayependa uhalifu, lakini tabia hii inatupa kujua kuwa jamii yetu inalo tatizo kubwa si tu la wahalifu hao ambao wanakamatwa na kuadhibiwa na wananchi ‘wenye hasira kali’ bali jamii nzima yetu ina tatizo kubwa la kihalifu kwani hakuna mahali dhana ya kukomesha uhalifu kwa kufanya uhalifu mwengine dhidi ya mhalifu imeweza kufanikiwa duniani.

 

Hitimisho

Hivyobasi, nipende tu kusisitiza katika kuuanza mwaka huu wa 2018 ndugu yangu kama mwananchi na raia mwema wa taifa hili anza kutafakari maisha yako yaliyopita endapo kuchukua sheria mkononi mwako kumeleta faida yoyote katika kutatua matatizo tuliyonayo katika jamii.

Nikuache na swali hili ndugu yangu ambalo ni wewe pekee unaweza kujijibu kwa dhamiri yako ikikushuhudia

‘Je, ni kitu gani ungestahili kufanyiwa na jamii endapo ungebainika leo uhalifu ambao umekuwa ukiufanya katika maisha yako?

Naamini unalo jibu muafaka juu ya kile ambacho jamii ingekufanyia, pengine tusingekuwa nawe leo au msingekuwa nami leo kwa adhabu ambayo tungeipata kwa jamii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema na mwanzo mwema wa 2018.

Wako

Isaack Zake, Wakili