Sheria Leo. Kwa Nini watu Hujichukulia Sheria Mkononi?

 

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika mfululizo wa makala hizi za sheria kwa ujumla tunakwena kuangalia mambo kadhaa ya kijinai katika jamii. Karibi tujifunze.

Kujichukulia Sheria Mkononi

Katika makala iliyopita tumeweza kuona kwa utangulizi juu ya dhana ya mtu au watu kujichukulia sheria mkononi. Hii ina maana watu wanachukua hatua dhidi ya mtu au jambo Fulani pasipo kufuata mkondo wa sheria kama inavyoanishwa katika Katiba au sheria za nchi.

Tumeona kuwa suala la kujichulia sheria mkononi si suala jema kwa jamii yoyote ile ingawa kwa walio wengi kwenye jamii kutokana na vitendo vinavyoendelea ndani ya jamii wanaona ni sawa na kuwa sehemu ya kukomesha au kupunguza vitendo vya uhalifu.

Tumeona kuwa tatizo halipo kwa wahalifu au watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu peke yao ndani ya jamii lakini tatizo kubwa tunalo sisi wenyewe ndani ya jamii. Hivyo ni muhimu sana kwetu kama jamii kuchukua muda wa kujitathmini na kutafakari namna bora ambayo tunaweza kuitumia ili kusaidia nchi yetu kuondokana na matatizo haya ya uhalifu wa mtu mmoja mmoja na uhalifu wa jamii nzima.

Kwa nini watu hujichukulia Sheria Mkononi

Hili ni swali muhimu sana kujiuliza kama jamii na mtu mmoja mmoja. Ni kweli kwamba wengi wanachukua hatua dhidi ya uhalifu au dhidi ya mtu mwengine hata pasipo uhalifu kutendeka na mtu huyo huku wakiona jambo hilo wanalofanya ni sahihi. Lakini lazima zipo sababu zinazosukuma watu wachukue sheria mkononi pasipo kufuata utaratibu. Katika makala hii tunakwenda kuzitaja sababu kadhaa na kuanza uchambuzi wa kila sababu moja moja katika makala zinazofuata.

  1. Ujinga

Hii ni miongoni mwa sababu kubwa ndani ya jamii kukosa ufahamu juu ya madhara ya kuchukua sheria mkononi. Wengi wetu hatufahamu masuala ya sheria na mchakato wake katika kushughulikia makosa na uhalifu. Kwa kutokujua huku kunatufikisha kuchukua maamuzi ambayo mwisho wake si mzuri kwetu na kwa wale ambao maamuzi hayo yanatekelezwa dhidi yao.

 

  1. Kufuata mkumbo

Kumekuwa na tabia ndani ya jamii ya kufuata mkumbo yaani watu kukosa maamuzi binafsi na kufanya kila jambo kwa mazoea. Watu wakisikia kuwa jambo fulani limefanyika mahali nao wanahamasika kufanya pasipo kuchukua taadhari na kufanya tathmini juu ya madhara ya maamuzi hayo.

  1. Nafasi ya kulipa kisasi

Wanajamii wameumizwa kwa namna mbalimbali na vitendo vya uhalifu au migogoro ya mara kwa mara ndani ya jamii. Mara inapojitokeza fursa ya kuchukua hatua dhidi ya mtu au kitu ambacho kimekuwa kikiwaumiza, watu hawasiti kuchukua hatua ya kulipa kisasi.

  1. Kuepuka mchakato mrefu wa kisheria

Hii pia ni mojawapo ya sababu ambayo wanajamii wanaichukua ili kutimiza azma yao ya kuchukua sheria mkononi. Wenye uzoefu na masuala ya sheria wanafahamu kuwa mchakato wa kisheria hasa kwenye kushughulikia masuala ya kijinai huchukua muda mrefu sana na mara nyingine haathiri kazi na shughuli za kimaendeleo za kijamii. Njia bora inayoonekana inafaa ni kumaliza suala hilo mara moja kwa kufanya maamuzi pasipo kufuata mkondo wa kisheria.

  1. Kutokuwa na imani na vyombo vya upelelezi

Hii imekuwa moja ya sababu inayotolewa mara kwa mara na wananchi endapo wameamua kuchukua hatua mikononi mwao. Unaweza kusikia kuwa wahalifu hata wakikamatwa haichukui muda utawaona tena mtaani kuja kutishia maisha na ustawi wa jamii. Hivyo wananchi wanachukua hatua za kijamii na kukamilisha matakwa yao dhidi ya mtu au kitu kinachowasumbua.

  1. Kutokuwa na imani na mfumo wa mahakama

Pia mchakato wa kimahakama mara baada ya shauri kupelekwa mahakamani umekuwa mojawapo ya sababu ya watu kuchukua sheria mkononi. Wengi hawana imani na mahakma katika utendaji wa shughuli zake. Kuna tuhuma juu ya rushwa mahakamani na aina mbali mbali za upendeleo. Hii inaondoa imani na matarajio kwa watu kutokana na uhalifu unavyozidi kuongezeka.

  1. Hofu ya wanajamii kujihusisha na mchakato wa kisheria katika kushughulikia uhalifu

Ipo dhana ndani ya jamii kuwa endapo raia au mwananchi utajihusisha sana na mchakato wa kisheria katika kusaidia kutokomeza uhalifu basi utakuwa shabaha ya wahalifu wakati wowote. Hali hii inajenga hofu kubwa ndani ya jamii na hivyo kusababisha watu kuamua kumaliza kabisa matatizo wakati wa tukio.

  1. Mtu au jamii kujiahami dhidi ya mkondo wa sheria

Yapo mazingira ambayo yanamsukuma mtu kujichukulia sheria mkononi kwa sababu anajua kuwa endapo suala husika litafuta mkondo wa sheria basi itabainika kuwa hana haki ile ambayo anadhani anayo. Hivyo njia pekee ni kutumia nguvu, ubabe na fujo dhidi ya mtu mwengine au taasisi ambaye anazo haki zote endapo sheria itafuata mkondo wake.

Ndugu msomaji hizi ni baadhi tu ya sababu ambazo zinamsukuma mtu au jamii kwa ujumla kuchukua sheria mkononi dhidi ya mtu mwengine au kitu fulani. Sababu hizi na nyingine nyingi kwa sehemu kubwa zimeweza kujenga tabia hii ndani ya jamii ambayo inahatarisha mfumo wa usalama na ustawi kwa jamii nzima. Tuendelee kuwa pamoja katika kufuatilia kila sababu na namna bora ya kuweza kuchukua hatua ili kupunguza au kuondoa tabia hii ndani ya jamii.

 

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili