Sheria Leo. Ujinga ni sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi

 

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika mfululizo wa makala hizi za sheria kwa ujumla tunakwena kuangalia mambo kadhaa ya kijinai katika jamii. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Ujinga. Karibi tujifunze.

Ujinga kama sababu ya watu kuchukua sheria mkononi

Katika makala iliyopita tumeweza kuzianisha na kueleza kwa kifupi sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia watu kujichukulia sheria mkononi. Mojawapo ya sababu hiyo ni ujinga.

Ujinga sio tusi kama watu wengine wanavyodhani. Ujinga ni hali ya kutokujua kitu Fulani au kutokuwa na taarifa sahihi juu ya jambo Fulani. Wanadamu wote tunazaliwa tukiwa wajinga na kwa kadri tunavyokuwa tunaendelea kutambua na kujifunza mambo mbalimbali kutokana na mazingira yetu. Mifumo ya elimu ipo katika nchi mbalimbali kwa lengo la kuondoa ujinga.

Katika matatizo ambayo Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kuainisha pamoja na mengine ni ujinga, maradhi na umasikini.

Ujinga ni tatizo kubwa sana ndani ya jamii yaani hali ya kutokufahamu au kuwa na maarifa juu ya jambo fulani. Kama vile sheria inavyoelekeza kuwa watu wote wanapaswa kuishi kwa mujibu wa sheria ndani ya nchi. Hatahivyo, changamoto kubwa iliyopo ni namna ya watu kuijua hiyo sheria ambayo wanapaswa kuishi kwa kuifuata kila siku.

Katika mfumo wa elimu ya nchi hii msisitizo umewekwa kwa wananchi wote angalau wawe na elimu ya msingi. Si watu wote wanapata elimu ya msingi ambayo msisitizo wake ni maeneo makuu matatu yaani kusoma, kuandika na kuhesabu yaani KKK. Jitihada za nchi zinaonekana pia wakati huu kuhakikisha walau wale wanaopata elimu waweze kufika kiwango cha kidato cha nne.

Hatahivyo, katika mfumo rasmi wa elimu ya nchi hii masomo ya sheria hayajapewa kipaombele katika kufundishwa kwenye ngazi za msingi na sekondari. Sheria imebaki kuwa masomo ya taaluma na ni watu wachache sana wanaopata nafasi ya kusoma sheria na kuwa wanataaluma wa sheria. Hawa ndio majaji wetu, mahakimu, wakufunzi na mawakili wanaofanya kazi katika taasisi mbalimbali kuongoza mfumo wa sheria.

Changamoto nyingine inayowakabili watu wengi ni aina ya mfumo wa sheria zetu ambazo nyingi zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza. Pia lugha hiyo ya kiingereza ina lahaja ya kisheria yaani si kiingereza cha kawaida. Hii si tu changamoto kwa wananchi bali pia kwa wanataaluma wa sheria.

 

Kwa mfumo na mtazamo huu ambao upo sasa ni wazi jamii kubwa ya watu zaidi ya milioni 50 hawana taarifa sahihi juu ya kuishi kwa mujibu wa sheria. Hivyo kazi kubwa inatakiwa kufanywa na mamlaka husika kuona ni kwa namna gani elimu ya sheria inatolewa kwa jamii pana kwa lugha rahisi inayoeleweka.

Wengi wetu hatufahamu masuala ya sheria na mchakato wake katika kushughulikia makosa na uhalifu. Ujinga katika masuala la kisheria katika taifa unapaswa kufutwa kwa kutengeneza misingi tangu shule za awali na kuendelea. Pia ni vyema kuwa na mfumo huru kwa jamii kupata maarifa ya kisheria kupitia wataalam mbalimbali wa kisheria.

Hatua za kuchukua

  • Wanasheria wanapaswa kuchukua hatua za mbele zaidi kama wanataaluma kuhakikisha jamii yetu inapata elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya kuishi kwa mujibu wa sheria.
  • Serikali kupitia mfumo wa elimu na kuweka uzito wa masomo kuanzia elimu ya awali na msingi kujifunza misingi ya kuishi kwa mujibu wa sheria.
  • Bunge la Tanzania kuhakikisha linatunga sheria ya kuweza kusaidia wananchi kupata elimu ya kisheria kupitia tafsiri za sheria kutoka lugha ya kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili.

Ni wazi kwamba tunahitaji jamii yetu kuwa na taarifa sahihi na kupambana na adui ujinga katika maeneo yote. Eneo mojawapo la msingi ambalo tunapaswa kuweka nguvu zetu kama taifa ni eneo la sheria. Kwa kuwa sheria ni muhimu kwa kila mtu basi tunao wajibu wa kuhakikisha kila mmoja wetu anaijua sheria. Wadau wote tunapaswa kutekeleza wajibu wetu kwa kuielimisha jamii. Jamii ikipata elimu sahihi na kuondokana na ujinga wa sheria basi kwa sehemu kubwa tutakuwa tumepunguza tabia ya wanajamii kuchukua sheria mkononi yaani kutenda pasipo kufuata sheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema na mwanzo mwema wa 2018.

Wako

Isaack Zake, Wakili