27.B. Matokeo ya Ugonjwa au Kuumia kwa Mfanyakazi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa sababu ya uwezo mdogo wa kazi kutokana na Ugonjwa au Kuumia.

Vigezo vya Uchunguzi juu ya ugonjwa au kuumia

Kama tulivyoona katika makala iliyotangulia kuwa ugonjwa au kuumia kunaweza kuwa sababu ya kusitisha ajira ya mfanyakazi kwani ugonjwa au kuumia kunaweza kuchangia kupungua ufanisi wa mfanyakazi mahali pa kazi.

Pia tuliangalia kwa kirefu juu ya namna ya kuchunguza sababu zinazoweza kupelekea hatua mbalimbali kwa mwajiri kuchukua kuhusiana na hali ya ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi. Katika uchambuzi wa leo tunakwenda kuona athari zinazoweza kujitokeza mara baada ya mwajiri kufanya uchunguzi kuhusiana na suala la ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi.

Hata hivyo ni muhimu kufahamu kwamba mwajiri pindi anapochukua hatua za uchunguzi juu ya hali ya mfanyakazi wake ni vyema kuzingatia mambo yafuatayo;

 • Aina ya kazi
 • Muda ambao mfanyakazi atakosekana kazini
 • Kiwango cha ugonjwa au kuumia
 • Uwezekano wa kumbadilisha kazi mfanyakazi kwa muda au kumsaidia mfanyakazi kufanya kazi katika hali aliyonayo.

Vigezo hivi ni muhimu sana kuvizingatia kwani vinaweza kutoa dira na mwelekeo kwa mwajiri kuchukua hatua zinazostahili pasipo kuhatarisha mahusiano yake na mfanyakazi husika.

Athari za ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi

Baada ya uchunguzi mwajiri anakuwa katika nafasi nzuri ya kutambua ni kwa kiwango gani cha ugonjwa au hali ya kuumia kwa mfanyakazi kunaweza kuleta athari kwa ajira au mfanyakazi mwenyewe. Athari hizi zinaweza kutazamwa kama ifuatavyo.

 

 1. Athari endapo ugojwa au kuumia ni kwa kudumu

Endapo uchunguzi utabainisha kuwa matokeo ya ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi ni ya kudumu yaani hatoweza kurudi katika hali yake ya awali kabla ya kuumia au kupata ugonjwa. Basi mwajiri anaweza kuchukua hatua zifuatazo.

 • Kumbadilisha mfanyakazi kazi na kumpangia majukumu yatakayoweza kuendana na hali aliyonayo kwa sasa.
 • Kumsaidia mfanyakazi kufanya kazi katika hali ya ugonjwa au ulemavu alionao kwa sasa. Hii ni kumwekea miundombinu na mazingira bora zaidi ya kuweza kutekeleza wajibu wake alionao. Zipo aina za kazi haziwezi kuathiriwa sana kutokana na hali ya ugonjwa au ulemavu, hivyo ni wajibu wa mwajiri kuweka mazingira yatakayosababisha mfanyakazi kuendelea kutimiza wajibu wake.

Kama uwezekano huo wa kutimiza wajibu husika kwa mfanyakazi haupo basi hatua ya mwisho kabisa kwa mwajiri ni kusitisha ajira ya mfanyakazi kutokana kwa kuumia au ugonjwa.

 

 1. Athari endapo ugonjwa au kuumia ni kwa muda

Endapo uchunguzi utabainisha kuwa matokeo ya ugonjwa au kuumia kwa mfanyakazi ni hali ya muda yaani baada ya kipindi Fulani mfanyakazi ataweza kuridi katika hali yake ya awali. Basi mwajiri anaweza kuchukua hatua zifuatazo;

 • Kumbadilishia mfanyakazi kazi kwa muda
 • Kumpa mfanyakazi kazi nyepesi
 • Kumpa mfanyakazi kazi mbadala
 • Kumpa mfanyakazi nafasi ya kustaafu mapema

Hitimisho

Leo tumeona vigezo ambavyo mwajiri anapaswa kuzingatia wakati wa uchunguzi wa hali ya mfanyakazi aliyepata ugonjwa au kuumia. Pia athari ambazo zinaweza kujitokeza mara baada ya uchunguzi huo. Kimsingi sheria inaelekeza mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri yaweze kutunzwa kwa muda mrefu kwa kadri inavyowezekana ndio maana suala la kusitisha ajira halipaswi kuwa kipaombele kwa mwajiri bali ni suluhu ya mwisho kabisa baada ya kukosekana mbadala wa aina yoyote. Waajiri wengi wamekuwa wakikimbilia kusitisha ajira mara baada ya kuona mfanyakazi ana hali ya ugonjwa au kaumia, hii ni kinyume cha taratibu za sheria za ajira.

Tuendelee kufuatilia mfululizo wa makala hizi kujifunza juu ya taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kusitisha ajira kutokana na kuumia au ugonjwa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.