Sheria Leo. Kufuata Mkumbo ni sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Kufuata Mkumbo. Karibi tujifunze.

 

Kufuata Mkumbo kama sababu ya watu kuchukua sheria mkononi

Katika makala iliyopita tumeweza kuzianisha na kueleza kwa kifupi sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia watu kujichukulia sheria mkononi. Mojawapo ya sababu hiyo ni kufuata Mkumbo.

Kufuata mkumbo ni ile hali ya kutekeleza maamuzi ya aina fulani ambayo yamefanywa na mtu au watu wengine pasipo kuwa na muda wako binafsi kufikiri kwa kina athari hasi au chanya za maamuzi hayo.

Katika mfumo wa jamii yetu baadhi ya watu hawapendi kujipa muda wa kufikiri kabla ya kutenda. Wao wapo tayari wakati wote kuambiwa ni kitu gani cha kufanya katika maisha. Tabia hii imeshamiri sana katika jamii, huu ni ‘uvivu wa kufikiri’.

Mathalani utakuta watu wazima wanashawishiwa na mtu kuwa mtu wa aina fulani hawatakii mema kwa kuwa anamiliki eneo kubwa kuliko wao basi waungane wakavamie eneo husika. Watu hao wanachukua hatua hiyo pasipo hata kufikiri huyo mtu ana uhalali kiasi gani wa kumiliki eneo husika. Ipo mifano mingi ya watu kufuata tu mkumbo kwa kigezo kuwa wanaonewa au wananyanyaswa pasipo kufikiri athari ya utekelezaji wa maamuzi hayo.

Kumekuwa na tabia ndani ya jamii ya kufuata mkumbo kwa watu kukosa maamuzi binafsi na kufanya kila jambo kwa mazoea. Watu wakisikia kuwa jambo fulani limefanyika mahali nao wanahamasika kufanya pasipo kuchukua taadhari na kufanya tathmini juu ya madhara ya maamuzi hayo.

Maamuzi ya kufuata mkumbo kwa tafsiri nyingine kwa lugha ya kiingereza ‘mob psychology’ yaani maamuzi yanayotokana na ushawishi ndani ya kikundi au kundi la watu kwenye jamii.

Labda nikupe kisa kimoja ambacho nilikishuhudia maeneo ya mjini karibu na hospital ya Hindumandal ambapo zilitokea kelele za mwizi na kijana akawa anakimbia huku kundi kubwa la watu wakimkimbiza. Baada ya kukamatwa kijana akaleza kuwa yeye si mwizi isipokuwa ana tofauti na binti mmoja na ndiye aliyemuitia kelele za mwizi. Pakajitokeza watu wenye busara kati ya kundi lile wakaamua kumuuliza alipo binti huyo na kisha wakamrudisha mpaka mahali hapo. Baada ya kufika na kukutana na binti  watu wakaanza kumuuliza huyo binti kitu gani ameibiwa akakosa jibu. Kumbe wanafahamiana na walihitilafiana kauli na kupelekea yule kijana kumpiga kibao na baadae binti kuanza kuitia kelele za mwizi.

Kisa hiki kimenitafakarisha mambo mengi sana juu ya aina ya jamii yetu kuchukua maamuzi ya mkumbo pasipo kufikiri.

  • Je, kama wasingejitokeza watu wenye busara kutaka kujua kitu gani kimetokea kwa yule kijana hali ingekuwaje?
  • Je, kama yule binti asingepatikana kueleza kuwa si suala wizi bali kutokuelewana kwao?
  • Je, kama wasingekuwepo watu walioshuhudia kile kilichotokea kati ya kijana na yule binti hali ingekuwaje?

Ndugu msomaji ni dhahiri kwamba busara ilisaidia kuepusha maafa ya yule kijana kutokana na dhana aliyodhaniwa nayo kuwa ni mwizi kumbe ni tofauti ya kauli kati yake na binti. Wapo watu ambao tayari walishampiga pasipo kuuliza na walikuwa tayari kutekeleza mauaji pasipo kujua hata chanzo cha suala husika.

Hatua za kuchukua

  • Kabla ya kutekeleza uamuzi wa jumuiya jiulize au uliza chanzo cha uamuzi huu ni nini.
  • Kabla hujatekeleza maamuzi ya jumuia tafakari kwanza juu ya athari chanya na hasi za uamuzi huo
  • Zaidi ya yote tujifunze kuwa na subira kabla ya kutekeleza maamuzi yoyote ikiwa ni binafsi au ya jumuiya.

Ni wazi kuwa busara katika kuteleleza maamuzi ndani ya jamii hasa maamuzi ya kijumuiya inahitajika ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa mtu au kitu au jamii nzima. Tumekuwa na shuhuda mbalimbali za matukio yanayofanywa ndani ya jamii kutokana tu na hali ya maamuzi ya kufuata mkumbo. Hii haitusaidii kuleta suluhu katika jamii bali inaweza kuleta jamii ambayo siku zote inategemea kuishi kwa ghasia kusuluhisha matatizo yake, kitu ambacho hakileti suluhu bali maangamizi ya kila kukicha.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema na mwanzo mwema wa 2018.

Wako

Isaack Zake, Wakili