Sheria Leo. Kulipa Kisasi ni sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Kulipa Kisasi. Karibu tujifunze.

Kulipa Kisasi kama sababu ya watu kuchukua sheria mkononi

Katika makala iliyopita tumeweza kuzianisha na kueleza kwa kifupi sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia watu kujichukulia sheria mkononi. Mojawapo ya sababu hiyo ni Nafasi ya kulipa kisasi.

Dhana ya kulipa kisasi kwenye jamii ni dhana ya muda mrefu sana na inafahamika na watu wengi na imekuwa ikitumika kama sehemu ya kuridhisha nafsi kutokana na madhila mtu aliyopata.

Kulipa kisasi ni namna ya kurejesha adhabu au maumivu kwa mtu ambaye alikufanyia jambo au mambo yaliyokuumiza katika maisha yako.

Katika mafundisho ya kijamii na hata masuala ya kidini tunaaswa kuachana na dhana ya kulipa kisasi kwa watu waliotufanyia mambo ambayo yalituudhi au kutuumiza katika maisha.

Nafasi ya kulipa kisasi imekuwa ikichukuliwa na watu wengi katika msingi wa kujichukulia sheria mkononi. Mathalani linapojitokeza tukio la uhalifu mahali ambapo wapo watu ambao ni waathiriwa wa matukio hayo na hawakuweza kuwapata wahalifu waliowatendea madhila hayo basi nafasi hiyo ya kulipa kisasi inakuwa imejitokeza na wanaitumia kikamilifu.

Tumekuwa mashuhuda wa namna ya wananchi wenye hasira kali wanapojichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu wahalifu ambao wamewakamata wakisema hatakama si hawa waliotudhuru basi tunayo haki ya kulipiza kisasi kutokana na kile ambacho tumefanyiwa na wahalifu wengine.

Katika mfano mwengine tunaona dhana hii ikitumika pia na wasafirishaji kwa njia ya boda boda. Mara kadhaa tumeshuhudia ajali zinazohusisha magari na boda boda barabarani zikileta dhana hii ya ulipaji wa kisasi. Tumeshuhudia wasafirishaji hawa mara baada ya ajali kabla hata ya kuacha sheria ichukue mkondo kujua nini chanzo cha ajali na nani aliyesababisha basi wanachukua hatua la kumvamia dereva wa gari au hata kuharibu gari kwa kulichoma moto.

Tusishangae kutokana na hali hii ya kijamii ambayo imejitokeza katika jamii yetu, haiishii kwa wahalifu tu ambao wanaiba kwenye majumba yetu au maeneo yetu ya kazi bali wimbi hili la kujichukulia sheria mkononi linaenda hata kwenye mazingira haya ya usafiri.

Ndugu msomaji tutafakari maswali kadhaa ya kutusaidia kuhusu dhana hii ya ulipaji kisasi

  • Je, ni sahihi kwetu kujilipiza kisasi na kuacha mkondo wa sheria
  • Je, ni sahihi kutoa adhabu au kulipa kisasi kwa mtu au watu wasiohusika na madhara yaliyokupata?
  • Je, ni kiwango gani cha kupima adhabu na namna bora ya ulipaji wa kisasi kwa yule aliyekudhuru?
  • Je, madhara yaliyokupata yanafanana na kiwango cha kisasi unachotaka kulipa?

Tafakari hii isiishie tu kwa matukio ya wahalifu lakini tafakari pia mazingira yanayoweza kukukuta wewe ambaye unafuata sheria katika maisha yako lakini unajikuta kwenye ajali ambayo umesababisha madhara kwa mtembea kwa miguu au boda boda na unajikuta katika hali ya watu wa boda boda au wananchi wenye hasira kali wakikukabili. Unapata picha gani mpaka hapo?

Hatua za kuchukua

  • Kabla ya kuchukua uamuzi wa kujilipizia kisasi tafakari endapo ni kweli unayo sababu hiyo au kuna tukio ambalo limetokea na kukusababisha kufanya hivyo
  • Kabla ya kuchukua uamuzi wa kulipiza kisasi pima endapo kiwango cha kisasi unachotaka kulipa kinafanana kwa kiasi gani na kosa ulilotendewa
  • Kubali matokeo kuwa kama wewe unatenda kwa kulipa kisasi kwa wengine hata wasiohusika na kukuletea madhara basi uwe tayari na wewe siku moja kujikuta watu wanataka kulipa kisasi kwako hata kama hukuwadhuru kwa lolote.

Ni muhimu sana kufahamu kuwa kama umeamua kuishi kwa kulipa kisasi basi tegemea kuwa kuna siku watu watajilipiza kisasi katika maisha yako au kazi yako au familia yako hili ni jambo ambalo linatokea katika maisha yetu kila siku.

Maisha yetu ni mafupi sana tunahitaji upendo wa kutusaidia kuishi katika kipindi hiki na zaidi endapo kuna changamoto ambayo unajua inahusisha suala la haki ni vyema tu kufuata mchakato unaohusika.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili