27.C. Utaratibu wa kusitisha ajira kwa sababu ya Ugonjwa au Kuumia kwa Mfanyakazi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Leo tunaendelea kuangalia juu ya usitishaji wa Ajira kwa sababu ya uwezo mdogo wa kazi kutokana na Ugonjwa au Kuumia.

Utaratibu wa Haki wa Kusitisha Ajira

Katika makala zilizopita tumeweza kuona namna ya uchunguzi wa sababu ya ugonjwa au kuumia kazini. Pia tumeona juu ya vigezo ambavyo vinapaswa kutumika wakati wa uchunguzi na matokeo ya uchunguzi husika.

Hatahivyo, yapo mazingira ambayo yanajitokeza wakati wa uchunguzi na kushughulikia tatizo la mfanyakazi alieyeumia au aliyepata ugonjwa na kuathirika kwa utendaji wake. Endapo itabainika kuwa suluhu zote mbadala ya kuweza kutunza ajira yake haziwezekani basi mchakato wa kusitisha ajira ya mfanyakazi unaweza kufanyika.

Ni muhimu sana kwa mwajiri kuzingatia mchakato huu kwani ni lazima ufanywe kwa mujibu wa sheria na taratibu, vinginevyo zoezi zima la usitishaji wa ajira linaweza kuwa batili.

Ufuatao ni utaratibu unaopaswa kuzingatiwa endapo mwajiri anataka kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa sababu ya ugonjwa au kuumia;

  1. Mwajiri lazima afanye uchunguzi ili kujiridhisha endapo hali ya kupungua kwa ufanisi wa mfanyakazi ni matokeo ya ugonjwa au kuumia.

 

  1. Mfanyakazi ni lazima ashirikishwe katika kipindi chote cha uchunguzi na kupewa njia mbadala za kutatua changamoto husika.

 

 

  1. Mwajiri pia anapaswa kuzingatia njia mbadala atakazopendekeza mfanyakazi. Endapo mwajiri atazikataa ni lazima atoe sababu.

 

  1. Mfanyakazi anayo haki ya kuwakilishwa na mwakilishi wa chama au mfanyakazi mwenzake wakati wa majadiliano.
  2. Kabla ya kuchukua maamuzi ya kusitisha ajira kutokana na ugonjwa au kuumia, mwajiri ni lazima aitishe kikao na mfanyakazi husika na mfanyakazi anayo haki ya kuwakilishwa kwenye kikao na mfanyakazi mwenzake au mwakilishi wa chama cha wafanyakazi.

 

  1. Mwajiri anapaswa kutoa sababu za hatua anazochukua na mfanyakazi anaweza kujibu hoja hizo au mwakilishi wake kabla ya kufikia maamuzi ya mwisho.

 

 

  1. Mwajiri anapaswa kuzingatia hoja za mfanyakazi au mwakilishi wake endapo zinakubalika au la na kutoa sababu kwa nini hazikubaliki.

 

  1. Matokeo ya kikao yanapaswa kuwasilishwa kwa mfanyakazi kwa maandishi na kueleza sababu za maamuzi hayo kwa kifupi.

Hizi ndizo hatua ambazo mwajiri anapaswa kuzichukua endapo anakusudia kusitisha ajira ya mfanyakazi kutokana na ugonjwa au kuumia.

Ni muhimu kufahamu kuwa mwajiri hapaswi kusitisha ajira ya mfanyakazi kwa sababu tu ya ugonjwa wa VVU yaani kuwa na maradhi yatokanayo na maambukizi ya ukimwi. Sheria inampiga marifuku mwajiri kumwachisha mfanyakazi kwa sababu hiyo. Ni mpaka pale ambapo itabainika kuwa mfanyakazi hawezi tena kufanya majukumu yake kutokana na maradhi husika.

Hitimisho

Katika mfululizo wa makala hizi za utendaji usioridhisha tumeweza kujifunza sababu mbalimbali ambazo zinachangia utendaji usioridhisha ikiwepo uzembe, ugonjwa na kuumia. Muhimu kwa mwajiri kuchunguza hasa sababu inayochangia utendaji usioridhisha na kuchukua hatua zinazostahili kulingana na sababu. Waajiri wengi wanapuuza kufuata utaratibu na matokeo yake ni migogoro ya mara kwa mara na wafanyakazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.