Biashara Sheria.6. Biashara kwa Mfumo wa Kampuni

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Katika makala iliyopita tumeona mfumo wa uendeshaji biashara na mamlaka inayohusika na usajili wa biashara hizo. Tumeona juu ya makundi makuu 3 ya uendeshaji wa biashara kisheria na usajili wake. Pia tumeangalia juu ya uchambuzi wa mifumo ya biashara binafsi na ile ya ubia. Leo tunakwenda kuchambua mojawapo ya aina ya biashara katika mfumo wa Kambuni  ‘Company’. Karibu tujifunze.

Mfumo wa Biashara ya Kampuni

Biashara katika mfumo wa kampuni ina ngazi ya juu ya ufanyaji wa biashara ambapo watu wanaunda taasisi ya kisheria inayoitwa kampuni kwa malengo ya kibiashara. Kama ilivyo mifumo mingine ya kibiashara kampuni nayo huanzishwa kwa mujibu wa sheria. Zipo aina nyingi za kampuni ikiwa ni za biashara au za hisani yaani zile zinazofanya shughuli pasipo kuingiza faida.

Tofauti kubwa kati ya kampuni na mifumo mingine ya kibiashara ni kwamba kampuni inapoundwa inapata hadhi ya kisheria ambayo inaitofautisha na wale walioinazisha kwa lugha ya kisheria au kiingereza ‘legal personality’ yaani kampuni ni mtu wa kisheria. Hivyo wamiliki wa kampuni wao wanamiliki hisa tu na endapo kampuni itafilisika basi madeni yataishia kwenye kampuni husika wala si kwa wamiliki wake.

Faida za Biashara katika Mfumo wa Kampuni

Zipo faida nyingi za kuendesha biashara katika mfumo wa kampuni ambazo wamiliki wa biashara wanaweza kuzipata;

  • Kampuni inatofautishwa na wamiliki wake au wana hisa wake. Wale wanaohusika na kuanzisha kampuni kisheria na kampuni huwa watu tofauti yaani kampuni inapata utu wake’‘legal personality’. Hivyo kuifanya kampuni kuwa na maamuzi yake na kuendesha shughuli zake pasipo kuingiliwa na wamiliki wake.

 

  • Kutokuwa na ukomo wa maisha; wamiliki wa kampuni wanaweza kufa au kujiondoa kwenye kampuni, lakini kampuni inaweza kudumu muda mrefu zaidi endapo itaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria. Huu ni mfumo mzuri wa biashara ambapo familia mnaweza kurithishana vizazi na vizazi endapo utasimamiwa vizuri.

 

  • Madeni; katika suala la madeni kampuni pekee ndiyo inahusika na madeni yake wamiliki wa kampuni hawausiki na madeni ya kampuni. Endapo kampuni ikafilisika basi kitakachofilisiwa ni kampuni peke yake

 

  • Urahisi wa kodi; katika mfumo wa kampuni kutegemeana na aina ya shughuli zake kodi zinaweza kuwa za wastani na zinahusiana na kampuni pekee. Mfumo wa kampuni unafanya masuala ya mahesabu kuzingatiwa zaidi na kufanywa kitaalam hii itasaidia katika suala la kulipa kodi zitalipwa kwa mujibu wa taarifa sahihi za kampuni.

 

  • Mtaji; ni rahisi zaidi kwa kampuni kupata mtaji wa kuiendesha kuliko mifumo mingine ya biashara. Kitendo cha uwepo wa wazo zuri la biashara na kuendeshwa kwa mfumo wa kampuni kunaweza kuchangia ukuaji wa mtaji kwa kuuza hisa zake katika soko la hisa na wanahisa kupata gawio la faida.

 

 

  • Uendeshaji; kampuni huendeshwa kisasa zaidi kuliko mifumo mingine ya kibiashara. Ni rahisi kwa kampuni kupata usaidizi wa wataalam wa fani mbalimbali kuliko mifumo mingine ya biashara. Hali hii huchangia ukuaji mkubwa na kasi wa kampuni.

 

  • Kurithisha; mmiliki wa hisha za kampuni anaweza kutoa hisa zake kama urithi wa warithi wake. Hii inasaidia kwa wanafamilia kutunza mali za familia na maslahi yao yaliyopo kwenye kampuni.

 

Changamoto za Biashara katika mfumo wa Kampuni

Pamoja kuwa na faida nyingi za mfumo wa kampuni zipo baadhi ya changamoto ambazo zinaikumba aina ya mfumo huu wa biashara ambazo zinajitokeza;

  • Gharama; mfumo wa kampuni una gharama za juu kidogo katika kuanzisha tofauti na mifumo mingine. Hata hivyo kama wafanyabiashara wanaweza kuunda ubia kwa kuchangia mtaji ni wazi kuwa wanaweza kuanzisha kampuni ya pamoja. Kwa kupata ushauri wa wanasheria unaweza kufungua kampuni kwa gharama ndogo ambazo unazimudu kulingana na aina ya kampuni unayotaka kufanya.

 

  • Uendeshaji; ni dhahiri kwamba unapokuwa na kampuni kuna mambo mengi yanajitokeza ya kiuendeshaji yanayohitaji usaidizi. Hii hutokea hasa kwenye kampuni kubwa sana, lakini kwa kampuni za kawaida hazihitaji uzoefu au utaalam wa ziada katika kuendesha kwani unafanya kama biashara nyingine tu. Ni mambo machache na kwa vipindi vichache utahitaji usaidizi wa wataalam.

 

  • Kuuza hisa; wakati mwengine kampuni inaweza kuwa na wazo zuri la biashara lakini ikashindikana kuliuza kwa wadau ili kuongeza mtaji.

 

  • Wanahisa wenye hisa chache; mfumo wa kampuni unampa yule mwenye hisa nyingi sauti kubwa kuliko wenye hisa chache hivyo kuminya sauti za wengine hata kama wana michango mizuri inaweza isikubaliwe.

Haya ni baadhi tu ya maeneo ya msingi ya kufahamu juu ya faida na changamoto zinazoikumba aina ya biashara ubia.

Hitimisho

Wengi wanapoisikia dhana ya kampuni hasa wafanyabiashara wanaona ni jambo kubwa na gumu kuanzisha au kulifanya hatahivyo hali haipo kama wanavyofikiri. Kama mfanyabiashara ukipata ushauri mzuri kwa wanasheria kuanzisha kampuni ni rahisi na ndio mfumo mzuri zaidi wa kufanya biashara kwa ngazi zote yaani kitaifa na hata kimataifa.

Mfumo wa kampuni ni mfumo bora zaidi wa kibiashara ambao wafanyabiashara wote wanapaswa kuchangamkia na kuzibadili biashara zao kwenda katika mfumo huo. Kutokana na mwingiliano wa kibiashara kwa mataifa mbalimbali, ni wachache sana wanafanya biashara kwa majina yao binafsi au ubia, biashara za kimataifa zinahitaji mifumo ya kampuni.

Hivyo nitoe rai kwa watu wote na wasomaji wetu endapo unafikiria kuanza biashara au tayari upo kwenye biashara mfumo bora unaoweza kuleta tija na ufanisi na manufaa kwa muda mrefu ni kufikiria kwenda katika kampuni.

Usikose tena kufuatilia katika makala ya Biashara Sheria wakati ujao tunapoendelea kuchambua mifumo hii ya kibiashara na namna zinavyoweza kusajiliwa katika mamlaka husika. Karibu.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili