Biashara Sheria.5. Biashara ya Ubia

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Katika makala iliyopita tumeona mfumo wa uendeshaji biashara na mamlaka inayohusika na usajili wa biashara hizo. Tumeona juu ya makundi makuu 3 ya uendeshaji wa biashara kisheria na usajili wake. Leo tunakwenda kuchambua mojawapo ya aina ya biashara ya Ubia au ‘Partnership’. Karibu tujifunze.

Mfumo wa Biashara ya Ubia

Huu ni mfumo wa biashara ya ambao unafanywa baina ya watu wawili au zaidi kwa pamoja kwa kuchangia mtaji, weledi na rasilimali nyingine kwa lengo la kupata faida ya pamoja.

Mfumo wa biashara ya ubia umekuwepo kwa muda mrefu sana katika historia ya biashara duniani. Watu wengi wamefanya kazi kwa pamoja kibiashara kwa kupanua wigo wa biashara zao, kwa kuchangia ujuzi walionao ili kuongeza tija katika kile wanachokifanya.

Watu wanaofanya biashara kwenye mfumo wa ubia wanaweza kuwa na wazo moja la kibiashara ambalo wanatumia rasilimali walizonazo kufanikisha malengo yao. Kwa kawaida mfumo huu wa biashara wabia wanagawana faida na hasara zinazotokana na ubia wao. Ili kusajili mfumo wa ubia kibiashara kuna utaratibu wa kusajili BRELA na wabia wanapaswa kuwa na mkataba wa ubia.

Wafanyabiashara wengi wanafanya biashara kwa ubia pasipokuwa na makubaliano ya msingi kwa maandishi bali wanafanya kwa kuaminiana kwa maneno. Hii inaleta hatari kubwa ya kupoteza na kukosa hali ya uwajibikaji wa wabia katika biashara.

Tofauti kubwa kati ya biashara ya ubia na biashara ya mfumo wa kampuni ni kwamba endapo hasara itajitokeza basi wabia watawajibika wao binafsi kufidia hasara kama ilivyo kwa biashara ya mtu binafsi. Wabia wanaweza kusajili jina la biashara la ubia wao tofauti na majina yao binafsi.

Faida za Biashara ya Ubia

Zipo faida nyingi za kuendesha biashara ubia ambazo wabia wa biashara wanaweza kuzipata;

  • Mtaji; ni rahisi zaidi kwa wabia kuchangia mtaji mkubwa wakati wa kuanza biashara tofauti na biashara binafsi. Hii itasaidia ubia wao kuanza kwa kasi nzuri na kusadia kuleta faida mapema kutokana na fedha ya mtaji kuwa kubwa. Kwa kadri biashara inavyokuwa na wabia wengi basi mtaji wake huongezeka.

 

  • Urahisi wa uendeshaji; ubia ni aina ya mfumo wa biashara ambao ni rahisi kuanzisha na kuendesha. Kinachohitajika katika ubia ni makubaliano tu ya wabia na wao kufanya kazi kama walivyokubaliana. Biashara ya ubia haina kuingiliwa kama ilivyo kampuni na wenye hisa wake. Pia wabia wanaweza kufikia maamuzi mapema ya namna bora ya kuboresha biashara yao au kuibadilisha pasipo kuwa na mchakato mrefu.

 

 

  • Uwajibikaji wa pamoja; katika kuendesha mfumo wa biashara ya ubia, wabia wote wanahusika katika kuwajibika kwa majukumu yao. Mfumo huu unamtaka kila mmoja kutimiza wajibu wake, kwani kutimiza huko kutaamua suala la faida na hasara ambazo ubia unaweza kupata. Ndio maana ni muhimu sana wabia kuwa na mkataba wa kimaandishi kuhusiana na ubia wao utakaoainisha majukumu yao ya kila siku.

 

  • Mfumo wa maamuzi; katika biashara yoyote maamuzi ni jambo la msingi sana. Katika mfumo wa ubia maamuzi hufanywa na wabia kwa pamoja. Inapojitokeza changamoto iwapo biashara ni ya mtu binafsi inawezekana akafanya maamuzi yasiyo sahihi lakini wanapokuwa watu wawili au zaidi basi uamuzi unakuwa umechujwa vizuri na kwa ajili ya tija ya ubia.

 

 

Changamoto za Biashara ya Ubia

Pamoja kuwa na mfumo rahisi wa uanzishwaji na faida nyingine ndani ya biashara ya ubia, zipo changamoto ambazo zinaikumba aina ya mfumo huu wa biashara ambazo zinajitokeza;

  • Kutokukubaliana kwa wabia; mojawapo ya changamoto kubwa ya kuendesha biashara kwa mfumo wa ubia ni hatari ya kutokukubaliana kwenye baadhi ya maamuzi ya msingi. Hali ya kutokukubaliana mara nyingi inavunja ubia. Pamoja na kuwa na mawazo mbadala kunaweza kuleta tija katika biashara lakini pia kunaweza kuvunja biashara. Hivyo kupunguza hali hii inashauriwa biashara ya ubia isiwe na watu wengi sana kwani itaathiri maamuzi.

 

  • Mkataba; msingi wa uendeshaji wa biashara ya ubia ni mkataba. Mkataba huu unaweza kuwa wa maandishi au wa mdomo. Ikiwa ni kwa mdomo ipo hatari ya wabia kutotimiza wajibu wao na kukwepa lawama. Kwa sheria za Tanzania ili kusajili ubia kwenye mamlaka ya BRELA uwepo wa mkataba wa maandishi ni muhimu kwa wabia kueleza namna wanavyokusudia kuendesha shughuli zao.

 

 

  • Hasara/madeni; katika mfumo wa biashara ya ubia hasara inaenda kwa wabia binafsi. Endapo patajitokeza madeni au kufilisika basi mali binafsi za wabia zitahusika kulipa madai au fidia kwa wanaodai ubia huo. Hasara zinaweza kusababishwa na uzembe au mmoja wa wabia kutokutimiza majukumu yake huku wote wakihusika kubeba hasara hiyo.

 

  • Kodi; mojawapo cha changamoto kubwa dhidi ya mfumo wa biashara ya ubia ni kodi kwani kila mmbia anapaswa kulipa kodi peke yake wala kodi hailipwi kutokana na ubia. Hii inasababisha pamoja na kuwa biashara ni moja na huduma wanayotoa ni moja kila mmoja ndani ya ubia analipa kodi.

 

 

  • Mgao wa faida; mara nyingi mgao wa faida kwa wabia huwa sawa. Hatahivyo msingi huu wa mgao unaleta changamoto kwa wabia endapo wapo baadhi ambao hawawekezi nguvu zao za kutosha katika kufanikisha malengo ya kibiashara.

 

  • Uaminifu; shughuli nyingi za ubia zimegubikwa na hali ya wabia kutokuaminiana. Wengine wanatumia rasilimali za ubia kufanikisha malengo binafsi pasipo wenzao kufahamu. Hii imekuwa sababu kubwa ya kuvunja ubia mara kwa mara yaani wabia wanakosa uwazi na kuweka maslahi ya ubia wao mbele kuliko maslahi binafsi.

Haya ni baadhi tu ya maeneo ya msingi ya kufahamu juu ya faida na changamoto zinazoikumba aina ya biashara ubia.

Hitimisho

Mfumo wa biashara ya ubia ni mfumo mzuri sana kwa watu ambao wanataka kufanya biashara ya kati. Pia mfumo huu unafaa sana kutumika na watu wanaotoa huduma kutokana na taaluma zao kama wahasibu, wanasheria, madaktari au wahandisi. Zipo biashara nyingi zinaendeshwa kwa mfumo wa ubia ingawa hazijasajiliwa na mamlaka ya usajili au zimesajiliwa kama biashara binafsi. Ni muhimu sana kwako mfanyabiashara au ndugu unayetaka kuanza biashara kufahamu mifumo hii na kupata kujua faida na changamoto zake na njia bora za kukabiliana nazo. Unapoamua kufanya biashara ya ubia ni muhimu sana umfahamu huyo unayeingia ubia naye juu ya tabia na haiba na wajihi wa muhusika ili kuepuka hasara na migogoro ya baadae.

Usikose tena kufuatilia katika makala ya Biashara Sheria wakati ujao tunapoendelea kuchambua mifumo hii ya kibiashara. Karibu.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili