33. Utatuzi wa Migogoro ya Kazi
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tumeweza kuzungumza juu ya maana ya migogoro ya kazi na kuzifahamu aina kuu za migogoro yaani migogoro ya maslahi ‘dispute of interest’ na lalamiko ‘dispute of right’. Leo tunaanza kuangalia taratibu za kisheria za utatuzi wa migogoro ya kazi. Karibu tujifunze.
Mgogoro wa Kikazi
Dawa ya mgogoro wowote siku zote ni utatuzi hakuna mbadala. Sheria ya Ajira kwa kujua kuwa mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri kuwa yana chamgamoto zake ambazo zinaweza kuibua migogoro imeweka njia nzuri na mfumo madhubuti wa kusaidia utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa mapema zaidi.
Sheria ya kazi imeweka utaratibu wa utatuzi wa migogoro katika ngazi mbalimbali ikiwepo Usuluhishi, Uamuzi na Mahakama. Hatahivyo, kama mahusiano mengine ya kimkataba pande mbili zinaweza kuwa zimekubaliana namna bora ya utatuzi wa mgogoro endapo utajitokeza.
Katika makala hii ya leo tutaeleza hatua hizi 3 au mfumo huu wa utatuzi wa migogoro ya kiajira kwa utangulizi ili kufahamu juu ya mchakato mzima na maana ya maneno ya usuluhishi, uamuzi na mahakama.
- Utatuzi kwa njia ya Usuluhishi
Hii ni njia mojawapo ya utatuzi wa migogoro ya kikazi pale unapojitokeza baina ya mwajiri na mfanyakazi. Hatua ya usuluhishi ndio hatua ya awali kabisa katika kujaribu kufikia makubaliano pande mbili. Usuluhishi ni mchakato wa utatuzi wa mgogoro ambapo mtu huru anawasaidia wadaawa yaani mwajiri na mfanyakazi kuzungumza na kufikia suluhu ya tatizo au mgogoro wao. Katika usuluhishi mtu huru hana mamlaka ya kulazimisha pande mbili zipatane bali atatumia uzoefu wake katika migogoro kuwashauri namna bora ya kumaliza mgogoro wao. Sheria za Ajira zimetoa fursa ya matumizi ya usuluhishi kama njia ya awali ya kutatua mgogoro kwa haraka kuliko njia nyingine.
Katika zoezi la usuluhishi lengo halipo kwenye sheria au msingi wa mgogoro baina ya wadaawa bali namna bora ya kumaliza mgogoro kwa pande zote kuondoka kwa amani. Hivyo wadaawa hawapaswi kung’ang’ania hoja za kisheria wala kuhusisha nyaraka bali mazungumzo ya pande mbili ya kuthamnini uhusiano uliopo kati ya mwajiri na mfanyakazi. Katika kufanikisha zoezi la usuluhishi, msuluhishi anaweza kufanya vikao vya pamoja na wadaawa au akafanya vikao na kila mdaawa ili kuona namna bora ya kumaliza mgogoro. Hii ndio njia bora zaidi ya kumaliza mgogoro kwa haraka na amani kwani hakuna upande unaoondoka na ushindi katika usuluhishi wote mnapata kidogo na kupoteza kidogo yaani ‘win-win situation’. Usuluhishi kwa lugha ya kiingereza unafahamika kama ‘mediation’.
- Utatuzi wa Mgogoro kwa njia ya Uamuzi
Uamuzi hii ni ngazi nyingine ya utatuzi wa migogoro ya kazi kwa mujibu wa sheria ya Ajira. Uamuzi kama ilivyo kwa usuluhishi pia ni mchakato ambapo anateuliwa mtu huru ambaye hafungamani na upande wowote wa wadaawa ambaye atakuwa na kazi ya kusikiliza hoja ya pande zote na kutoa uamuzi wake. Hapa tofauti na usuluhishi, mwamuzi anayo mamlaka ya juu kwani hatoi ushauri bali atasikiliza ushahidi wa pande zote na kutoa maamuzi yake kwa mujibu wa sheria za Ajira. Uamuzi unahusisha utoaji wa ushahidi ikiwa ni wa mdomo na vielelezo, uamuzi au TUZO anayotoa mwamuzi pamoja na sababu za uamuzi huo kwa mujibu wa sheria.
Katika zoezi la uamuzi lengo lipo katika kuzingatia matakwa ya sheria ya Ajira ili kuona endapo pande mbili zimezingatia majukumu yao kisheria au la. Upande ule utakaoonekana umekiuka masharti ya sheria ya Ajira basi utawajibika ipasavyo kisheria. Uamuzi katika lugha ya kiingereza unafahamika kama ‘Arbitration process’.
- Utatuzi wa mgogoro kwa njia ya Mahakama
Kama tulivyowahi kueleza katika makala za mwanzo juu ya Taasisi za Kazi kuwa Mahakama ya Kazi yaani Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ni mojawapo ya chombo kinachohusika na utatuzi wa migogoro ya kazi. Hii ni sehemu ya kitengo cha Mahakama Kuu kama mahakama nyingine yenye kushughulikia tu migogoro ya kazi. Migogoro ya kazi ina mfumo wake ya utatuzi ambapo huanzia kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kisha Mahakama ya Kazi na endapo upande wowote haujaridhika basi unaweza kufika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambacho ndicho chombo cha juu kabisa kwenye utatuzi wa migogoro yote.
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi inayo mamlaka ya kutafsiri sheria za kazi, kusikiliza rufaa kutoka kwa msajili wa vyama vya wafanyakazi na jumuiya za waajiri, kusikiliza mgogoro wa kimaslahi au lalamiko na kufanya marejeo ya uamuzi wowote kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi. Utatuzi kwa njia ya Mahakama kwa lugha ya kiingereza unajulikana kama ‘Adjudication process’
Hitimisho
Ndugu msomaji, leo tumejifunza njia ambazo zimewekwa kisheria za kushughulikia migogoro ya kazi kwa mujibu wa sheria. Tumeona njia ya Usuluhishi, Uamuzi na mchakato wa Mahakama ya Kazi. Pamekuwa na upotofu kwa watu wengi hasa wafanyakazi kwa kutokujua wapi wanapaswa kuwasilisha malalamiko au migogoro ya kazi tunaona wakiwasilisha Polisi au kwa watendaji wa serikali ikiwa ni serikali za mtaa, kata, wilaya hata mkoa hii yote ni kutokujua wapi wanapaswa kusikilizwa. Ni vyema wadaawa wote wakajua ni wapi eneo maalum linahusika na tatizo la kiajira, kwani kuwasilisha mgogoro eneo lisilohusika ni kupoteza muda na hatari yake ni kuchelewa kuwasilisha mahali husika na hatimaye kupoteza haki zako za msingi.
Katika makala zinazokuja tutaendelea kuchambua njia hizi za utatuzi wa migogoro na namna zinavyofanya kazi. Usikose kufuatilia.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.