32. Migogoro ya Kazi

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Kwa kipindi kirefu tumejifunza njia mbalimbali za usitishaji wa ajira. Leo tunaanza kuangalia taratibu za kisheria za utatuzi wa migogoro ya kazi. Karibu tujifunze.

Maana ya Mgogoro wa Kikazi

Kabla hatujaanza kujifunza juu ya utatuzi wa mgogoro wa kiajira ni vyema tukapata tafsiri ya mgogoro wa kiajira maana yake ni nini.

Mgogoro wa kazi ni aina ya mgongano baina ya mwajiri na wafanyakazi au mfanyakazi kuhusiana na jambo lolote la kimaslahi au lalamiko. Sheria ya kazi inaeleza kuwa migogoro ya kazi ni migogoro inayohusisha mwajiri au jumuiya ya waajiri kwa upande mmoja  na mfanyakazi au chama cha wafanyakazi kwa upande mwengine.

Ni matarajio ya kila mmoja yaani mfanyakazi na mwajiri kutekeleza wajibu wa mkataba au mahusiano ya kiajira kwa amani na kwa kunufaisha pande zote. Hatahivyo, yapo mazingira ambayo yanaweza kusababisha kutokuelewana baina ya pande hizi mbili na kuibua mgogoro.

Aina za Migogoro ya Kikazi

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira mgogoro umegawanyika katika sehemu kuu mbili yaani migogoro ya maslahi na migogoro ya kudai haki au lalamiko.

  1. Mgogoro wa Maslahi

Hii ni aina ya mgogoro ambao unahusisha madai ya kutengeneza haki ya baadae. Yaani katika mahusiano baina ya mwajiri na mfanyakazi inajitokeza kuwa kuna maslahi ambayo upande mmoja unahitaji yatambuliwe na upande mwengine ili yawe haki katika mahusiano yao. Hii ni aina ya mgogoro ambayo si lalamiko.

Mfano wa mgogoro wa maslahi

  • Mgogoro kuhusu nyongeza ya mshahara; hapa tayari kuna mshahara ambao pande zote zinakubaliana lakini upande mmoja ungependa kutokana na mazingira yaliyopo mshahara uongezwe au upunguzwe. Katika hali hii endapo pande hizi hazitaafikiana basi mgogoro wa maslahi hujitokeza.

 

  • Mgogoro kuhusu kuongezwa au kupunguzwa saa za kazi; hapa zipo saa za kazi ambazo pande zote zimekubaliana hata hivyo endapo mwajiri anataka kuongeza saa za kazi au wafanyakazi wanataka saa zipunguzwe na pakatokea kutokuelewana ndipo mgogoro wa maslahi hujitokeza.

 

 

  • Mgogoro kuhusu kurejewa makubaliano ya pamoja; hapa tayari yapo makubaliano ya pande zote lakini panajitokeza hali ya kutaka kurejewa makubaliano hayo ili kuongeza maslahi ya upande wowote ndipo mgogoro wa maslahi hujitokeza.

 

  1. Lalamiko

Lalamiko ni aina ya mgogoro unaohusu haki ambayo tayari ipo baina ya mwajiri na wafanyakazi. Hapa tayari kila upande una haki yake na endapo upande mmoja hautekelezi wajibu wake kwa kutimiza haki ya upande mwengine basi upande ulioathirika unayo haki ya kuleta lalamiko ili vyombo husika vitoe tafsiri juu ya haki hiyo.

Lalamiko au mgogoro wa haki unahusiana na

  • Haki zilizoainishwa katika mkataba baina ya mwajiri na mfanyakazi
  • Makubaliano ya pamoja kati ya Mwajiri au Jumuiya ya waajiri na chama cha wafanyakazi
  • Sheria za kazi

Mfano wa mgogoro wa haki au lalamiko ni;

  • Kushindwa kulipa mshahara
  • Kukiuka makubaliano ya pamoja
  • Kushindwa au kukataa kutekeleza masharti kwenye mkataba wa ajira
  • Kukiuka sheria za kazi

 

Hitimisho

Katika kujifunza juu ya taratibu za kutatua migogoro ya kazi ni muhimu kwa pande zote kufahamu maana ya mgogoro na aina za migogoro ya kikazi. Ufahamu huo unaweza kusaidia aina ya hatua za kuchukua katika kutatua migogoro hiyo. Kutokujua aina hizi za migogoro kunasababisha wadau husika kushindwa kuchukua hatua stahiki kuitatua. Katika makala zinazokuja tutaendelea kuchambua namna bora ya kisheria ya utatuzi wa migogoro hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.