Dhamira ya Kijinai ‘Mens rea’

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala iliyopita kwenye tuliangalia kwa kiashiria kimojawapo cha kosa la kijinai yaani kitendo cha kijinai ‘actus reus’ tumeona kuwa kitendo cha kijinai kinaweza kuwa suala la kutenda tendo lililokatazwa na sheria au kutokutenda kile ambacho sheria inakutaka utende. Leo tunakwenda kuangalia kiashiria kingine cha kosa la jinai yaani dhamira ya kijinai ‘Mens rea’.

Dhana Kuu za Viashiria vya Kosa la Jinai

Kama tulivyojifunza katika makala zilizotangulia kuwa msingi wa kudhibitisha kosa la kijinai linahusisha kukamilishwa kwa viashiria vikuu vya kosa husika yaani kitendo na dhamira ya kutenda kosa.

Dhana hii kama inavyoelezwa katika lugha ya Kiingereza kwa maneno haya

‘the act itself does not constitute guilt unless done with a guilty intent’

Tumeona dhana hii ikidhibitishwa na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Kifungu cha 10 kinachoeleza kwamba

‘Kulingana na masharti yaliyotajwa katika Kanuni hii kuhusiana na vitendo vya uzembe na kuacha kufanya, mtu hatawajibika kwa kosa la kijinai kwa kutenda au kuacha kutenda jambo ambalo limetokea bila ya idhini yake, au kwa tukio lililotokea kwa bahati mbaya’.

Maana ya Dhamira ya Kijinai

Dhamira ya kutenda kosa la kijinai ni pale mtu anakuwa amekusudia ndani ya fikra zake kutenda kitendo kinyume cha sheria. Hii ina maana kwamba mtenda kosa tayari amewaza/kutafakari na kufanya uamuzi kwenye fikra zake kutenda au kuacha kutenda kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Katika kudhibitisha juu ya uwepo wa dhamira ya kijinai kwa mtuhumiwa wa kosa la kijinai ni muhimu kuzingatia mambo matatu

  • Kwamba mtuhumiwa alifanya kitendo husika bila ya kulazimishwa

Dhamira ya kijinai kudhibitisha inabidi ionekane kuwa hapakuwa na kulazimishwa kwa mtuhumiwa kutenda jambo ambalo ni kosa. Na kwamba amelitenda kwa ridhaa yake mwenyewe pasipo kulazimishwa na mtu au mazingira yanayomzunguka kutenda jambo hilo. Kwa lugha ya kiingereza inaitwa ‘voluntariness’. Kitendo chochote kinachotendwa kinyume na utashi wa mtu au nje ya uwezo wake hakiwezi kudhibitisha dhamira ya kijinai.

 

  • Kwamba mtuhumiwa alikuwa anajua kile anachokitenda.

Mtuhumiwa anapaswa kujua kile anachokitenda. Kujua huku hakumaanishi kwamba lazima ajue kuwa anachokitenda ni kosa au la bali kujua kuwa anatenda tendo fulani. Wengi wanajitetea kuwa nimefanya jambo hili lakini sikujua kuwa ni kosa. Haina maana ya kujua kile unachofanya ni kosa bali kujua huku kuna maana ya kufahamu ni kitendo gani unachokitenda.

 

  • Kwamba mtuhumiwa alikuwa anatarajiwa kufahamu madhara ya kitendo alichokifanya.

Hapa mtuhumiwa anatarajiwa kufahamu au kuaminika kuwa anafahamu madhara yatokanayo na kitendo anachokitenda. Mfano mtu anampiga mwenzake ina maana ndani yake tayari anafahamu kuwa madhara yatokanayo na kitendo chake cha kumpiga mtu ni kuumia kwa mwenzake.

Katika shauri kati ya Antony Mhikwa vs Jamhuri (1968) HCD,460 mtuhumiwa alitiwa hatiani na mahakama ya chini kwa kosa la kuidharau mahakama kwa kucheka na kutoa sauti za kukera akiwa mahakamani kinyume cha Kifungu 114(1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Mtuhumiwa alikata rufaa na kutoa hoja kwamba nzi aliingia katika pua yake na kusababisha kutoa sauti ya ajabu na kupiga chafya mfululizo mahakamani. Mahakama Kuu ya Tanzania ilibatilisha uamuzi wa mahakama ya chini na kueleza kuwa vitendo vya mtuhumiwa vilikosa dhamira ya kijinai kwani havikutona na utashi wake mwenyewe

Hitimisho

Leo tumejifunza juu ya dhamira ya kijinai na namna ambavyo inaweza kuonekana kwa kupimwa na mahakama kutokana na ushahidi utakaowasilishwa. Kwa kuwa suala la dhamira ni suala la ndani ya mtu si rahisi kuliona lakini linapimwa kutokana na vitendo vya mtuhumiwa na kwa namna vilivyotekelezwa.

Endelea kufuatilia makala ijayo ili kujifunza zaidi juu ya kiashiria kingine cha kosa la kijinai.

‘Anzisha na fuata mchakato wa kisheria katika kushughulikia masuala ya uhalifu katika jamii’

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

 

2 replies

Comments are closed.