Sheria Leo. Kwa Nini watu hawachukui hatua dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Tumejifunza kwa muda mrefu juu ya makosa mbali mbali na namna ya kisheria kosa linavyotokea kwa kitendo na dhamira. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya Ulinzi wa Kisheria dhidi ya Ukatili kwenye Mahusiano. Leo tutajifunza ‘Kwa nini watu husita kuchukua hatua dhidi ya ukatili kwenye mahusiano’.

Karibu tujifunze.

Kusita Kuchukua Hatua

Kumekuwa na dhana ya muda mrefu ndani ya jamii kutokuwa wazi kuhusuana na ukatili unaoendelea katika mahusiano. Wengi wao wanaona si jambo la kiungwana kueleza juu ya hali wanazopitia ndani ya mahusiano hasa masuala ya manyanyaso na vipigo vya mara kwa mara. Wengine wameenda mbali kuona ni suala la kitamaduni na linalohitaji uvumilivu. Zimekuwepo sababu nyingi za kuwafanya waathiriwa kutochukua hatua kukomesha au kuondoa tatizo hili. Sababu hizo ni pamoja na;

  1. Aibu au fedheha kwa jamii

Wanamahusiano wengi wanaogopa kuchukua hatua dhidi ya ukatili au vipigo ndani ya mahusiano kwa hofu ya fedheha kwa jamii. Wanajiuliza kuwa wataonekana vipi mbele ya jamii. Je, jamii itawachukulia vipi juu ya uhusiano wao. Hii si sababu ya msingi kwani ulinzi wa maisha yako ni jukumu lako la kwanza. Aibu hii na hofu hii imewaponza wengi na kusababishiwa ulemavu na hata kupelekea kifo. Kama wangepata ujasiri wa kusema basi madhara zaidi yangeepukwa.

  1. Kutoonekana mvumilivu wa maisha ya mahusiano au ndoa

Kuna msemo usemao kuwa ndoa ni uvumilivu au mahusiano ni uvumilivu. Ni kweli yapo mazingira katika mahusiano yanahitaji kuvumilia. Ni lazima tujue kilichowaunganisha watu wawili mwanzo ni upendo. Upendo ukiondoka na uvumilivu hupungua au kutoweka kabisa. Ielewe yapo yanayovumilika ila si vipigo na kuharibu maisha ya wengine kwa kigezo cha kuvumiliwa.

  1. Sababu za kiuchumi

Hii pia imekuwa sababu ya watu kutochukua hatua au kusita kuchukua hatua dhidi ya unyanyasaji au ukatili katika mahusiano. Inawezekana mmoja katika mahusiano ana uwezo wa kiuchumi na ndiye anahusika na mahitaji yote na kwa kigezo hiki anakitumia dhidi ya mwengine. Lazima turudie kuwa uhai au afya ya mtu ni muhimu na inapaswa kupewa kipaombele kabla ya vingine. Hili ni suala la kifikra tu na kujiuliza je mahitaji ya kiuchumi yana nafasi kubwa kuliko afya na uhai wako au la?

  1. Sababu za watoto

Watoto wamekuwa wakitumiwa kama sababu ya kuficha unyanyasaji na ukatili kwenye mahusiano. Wengi wanahofu kuchukua hatua ya kuzuia au kuondoa hali hii kwa sababu ya watoto. Anajiuliza itakuwaje juu ya malezi ya watoto endapo uhusiano huu utaisha? Ni muhimu kufahamu kuwa afya, uzima wako ni muhimu sana kwa watoto hao ili uweze kuwahudumia vizuri. Usiache kuchukua hatua kwa kigezo cha kutokujua hatma ya watoto. Vipo vyombo vya kisheria vinavyoweza kusaidia kupata haki ya malezi na matunzo kwa watoto endapo uhusiano baina ya wazazi utakuwa umeharibika.

  1. Hofu ya kuogopa hali kuwa mbaya zaidi

Katika kuendeleza unyanyasaji wa maneno na vitendo, baadhi ya watu wamekuwa watisha wenzi wao kuwa endapo ataeleza kwa watu au vyombo vingine basi ataendeleza mateso au manyanyaso zaidi. Ieleweke kuwa mtu anayetoa vitisho hivyo tayari yeye ni mwoga, ana hofu ya kuchukuliwa hatua na vyombo husika. Usikubali kuendelea kunyanyasika kila leo kwa hofu ya mateso kuendelea. Ni heri kutoa taarifa ili kupata msaada wa mapema kabla mambo hayajaharibika zaidi.

  1. Mfungamano wa Kifamilia

Kama tunavyofahamu kuwa mahusiano ya kindoa au uzazi yanahusisha familia pana zaidi yaani ndugu wa pande zote. Ndugu pia wamekuwa chanzo cha kuendeleza manyanyaso na vipigo dhidi ya wanandoa kwa kuingilia au kupendelea pande za ndugu zao. Wengi wanahofu ya kuchukua hatua kutokana na mitazamo ya ndugu watasemaje. Pia upo wakati wa ndugu kulaumu endapo ndugu yao atachukuliwa hatua dhidi ya unyanyasaji.

Kwa kuangalia sababu zote hizi haziwezi kuwa mbadala wa uhai wa mwathiriwa au ustawi wa afya yake kwa ujumla. Hakuna sababu ya msingi inayoweza kumzui mtu kuchukua hatua. Kama upo kwenye kundi la watu ambao wananyanyasika kwenye uhusiano na una mojawapo ya sababu hizi ni vyema kufahamu kuwa hiyo si sababu ya msingi. Uhai wako na ustawi wa afya yako kama mwanadamu ndio sababu ya msingi na kitu cha kwanza kulindwa na wewe.

Ni vyema kama jamii tukachukua mtazamo mmoja wa kutoruhusu jamii yetu iishi katika hali hii ya vipigo na manyanyaso. Kama kuna tatizo baina ya watu walio kwenye mahusiano basi jamii tuwasidie kufikia mwafaka pasipo kupigana. Tusikubali kuchukua upande wa wanyanyasaji hata kama ni ndugu zetu, tuwasaidie kumaliza tofauti zao kwa amani na ikishindikana hivyo basi wafuate utaratibu wa kisheria inavyopaswa pasipo madhara ya kupigana.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail ulizasheria@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili