11.A. Uhuru wa Kuunda Vyama kwa Waajiri na Wafanyakazi
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Ijue sheria ya Kazi nashukuru tumeendelea kuwa pamoja na kupata maarifa haya ambayo yanaletwa kwako kupitia www.ulizasheria.co.tz katika makala iliyopita tuliangalia juu ya viwango vya ajira katika makala zaidi ya 5 mfululizo. Leo tunakwenda kuona juu ya Uhuru wa Kujumuika katika Vyama vya Wafanyakazi, Jumuiya za Waajirina Mashirikisho karibu sana tuendelee na mfululizo wa makala za ijue Sheria ya Kazi.
Uhuru wa kujumuika ni moja ya haki inayolindwa na Sheria ya Kazi ambapo kila mfanyakazi aliyeajiriwa anayo haki ya kuunda na kujiunga na Chama cha Wafanyakazi pamoja na kushiriki shughuli halali za chama chake. Pia haki hii inaenda sambamba kwa waajiri pia ambapo kila mwajiri ana haki ya kuunganika katika Jumuiya za waajiri.
Hata hivyo uhuru huu umeweka mipaka kwa baadhi ya wafanyakazi wafuatao;
- Hakimu anaweza kuunda au kujiunga na Chama cha Maafisa wa Mahakama pekee
- Mwendesha Mashtaka anawea kuunda au kujiunga na chama cha Waendesha mashitaka au watendaji wengine wa mahakama pekee
- Mfanyakazi meneja mwandamizi, ambaye kwa nafasi yake kazini anatengeneza sera kwa niaba ya mwajiri na ana mamlaka ya kuingia katika makubaliano ya pamoja na chama cha wafanyakazi kwa niaba ya mwajiri, anaweza asijiunge na chama cha wafanyakazi ambacho wafanyakazi si mameneja waandamizi
Haki ya uhuru wa kujumuika inatoa kinga ya kutokubaguliwa kwa mfanyakazi anayetekeleza haki hii na kwa mtendaji au kiongozi wa Chama au Shirikisho anapotekeleza majukumu yake halali.
Hali kadhalika chama chini ya haki ya uhuru wa kujumuika kinakuwa na haki ya;
- Kutengeneza katiba yake
- Kupanga na kuendesha mambo yake ya ndani na shughuli halali bila kuingiliwa
- Kujiunga au kuunda Shirikisho
- Kushiriki katika shughuli halali za Shirikisho
- Kujishirikisha na vyama au mashirikisho ya kiulimwengu, kuchangia na kupokea misaadaya kifedha kutokakwa vyama au mashirika hayo.
Utaratibu wa Kuunda chama cha Wafanyakazi
Chama cha wafanyakazi kinaanzishwa na wafanyakazi wasiopungua 20 ambao wanapaswa kuitisha kikao chao cha kuanzisha chama kisha watajiorodhesha na kutia saini zao katika regista ya mahudhurio. Watamteua Katibu wa kikao ambaye atatayarisha muhtasari wa kikao wenye azimio la kuanzisha chama.
Katika kuanzisha chama cha wafanyakazi mambo yafuatayo ni lazima kuzingatiwa:-
- Chama kiwe chama halisi cha wafanyakazi
- Kiwe chama huru kwa maana kianzishwe na mwajiri au Jumuiya ya waajiri
- Kianzishwe na wafanyakazi wasiopungua 20
- Kiwe na Katiba na Kanuni zinazozingatia kifungu cha 47 cha Sheria ya Ajira
- Kiwe na jina lisilofanana na jina la chama kingine kuzuia mkanganyiko au kuwapotosha watu
- Kiwe na makao yake makuu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Utaratibu wa kusajili chama
- Chama cha wafanyakazi kinapaswa kusajiliwa ndani miezi 6 kuanzia tarehe ya kuanzishwa kwake
- Maombi ya usajili yatafanywa kwa kujaza fomu maalum ambayo itajazwa kikamilifu na kusainiwa na Katibu wa kikao kilichoazimia kuanzisha chama.
- Fomu itaambatana na nakala zilizodhibitishwa za regista ya maudhurio, na muhtasari wa kikao kilichoanzisha chama, nakala zilizodhibitishwa za katiba na Kanuni
- Msajili atakisajili chama baada ya kudhibitisha kuwa kimetimiza masharti yote muhimu ya kisheria. Pia msajili anaweza kukataa kusajili chama na kutoa notisi kwa waleta maombi akieleza sababu za kutokusajili
- Wasioridhika na maamuzi ya msajili wa vyama vya wafanyakazi na jumuiya za waajiri ana haki ya kukata rufaa Mahakama ya Kazi.
Wajibu wa chama kilichosajiliwa
Chama kilichosajiliwa kina wajibu wa kuwasilisha kwa Msajili kila ifikapo tarehe 31 Machi ya kila mwaka taarifa zifuatazo:
- Taarifa ya fedha zilizokaguliwa kwa kipindi cha fedha kinachoishia tarehe 31 Disemba ya mwaka uliopita
- Orodha ya wanachama inayoonyesha jumla ya wanachama kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Disemba ya mwaka uliopita
- Majina ya viongozi walioteuliwa au kuchaguliwa na anuani zao ndani ya siku 30 tangu uteuzi au uchaguzi kufanyika
- Mabadiliko ya kanuni ndani ya siku 30 kuanzia siku ya mabadiliko hayo
Pia chama kina wajibu wa kutunza kwa miaka walau 5 kumbukumbu zifuatazo;
- Orodha ya wanachama katika fomu maalum
- Mihutasari ya vikao
- Karatasi za kura
Wajibu wa kuzingatia katiba ya chama
Chama cha wafanyakazi kinapaswa wakati wote kutekeleza shughuli zake kwa mujibu wa Katiba, kanuni na mazoea. Endapo itatokea chama kimeshindwa kuzingatia Katiba yake, Msajili au wanachama wanaweza kupeleka maombi Mahakama ya Kazi kutengua suala hilo lililofanyika kinyume cha Katiba.
Kabla ya maombi kupelekwa Mahakamani, taratibu za ndani za chama lazima zifuatwe kwanza isipokuwa kama kwa maslahi ya chama ni vizuri maombi hayo kusikiliwa bila utaratibu ndani ya chama.
Hitimisho
Sheria inaruhusu wafanyakazi na waajiri kuunda vyama vyao kwa kuangalia maslahi yao. Ni muhimu sana kuizingatia haki hii kwani umoja ni nguvu na utengano huleta udhaifu. Hata hivyo waajiri wengi wamekuwa wanawarudisha nyuma wafanyakazi kuunda vyama au kujiunga kwenye vyama, hii ni kinyume cha Sheria ya Ajira. Mwajiri haruhusiwi kumfukuza kazi au kumchukulia hatua zozote za kinidhamu mfanyakazi ambaye anatekeleleza haki yake ya kuunda au kujiunga na chama. Wafanyakazi watambue chama cha wafanyakazi si kuleta vurugu au madai ambayo hayatekelezeki kwa mwajiri bali ni kutafuta namna bora yakuboresha utendaji wao na ufanisi zaidi mahali pa kazi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Wako
Isaack Zake, Wakili