20. Kigezo cha Kuzingatia Sheria ya Ajira katika kusitisha Ajira
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi, tumeendelea kuwa pamoja kwa kipindi chote hiki. Makala iliyopita tuliangalia kigezo cha Vipengele vya Mkataba katika usitishaji wa ajira. Katika makala ya leo tunaangalia kigezo kingine cha Kuzingatia Sheria ya Ajira. Karibu tujifunze.
Maana ya Kigezo cha Sheria ya Ajira
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini imeweka masharti ambayo lazima mwajiri ayazingatie wakati anakusudia kusitisha ajira. Kama tulivyoeleza kuwa usitishaji wa ajira ni suala la mchakato ambao uhahusisha hatua mbalimbali. Inapofika mwisho wa mchakato huo yapo masharti ambayo mwajiri anapaswa kuyazingatia ili usitishaji huo uwe halali.
Sheria ya Ajira imeanisha baadhi ya mambo hayo ambayo mwajiri anapaswa kuzingatia ni kama ifuatavyo
- Notisi/Taarifa ya Usitishwaji wa Ajira
Hii ni taarifa ya kimaandishi mwajiri anapaswa kumpatia mfanyakazi juu ya kusudio lake la kusitisha ajira. Notisi hii itaainisha sababu za usitishaji wa ajira na tarehe husika ya notisi ambayo inatolewa. Ikiwa ni mfanyakazi wa siku au wiki basi notisi inatakiwa kutolewa siku 4 kabla ya usitishaji. Ikiwa mfanyakazi ni wa mwezi basi notisi itatolewa siku 28 kabla ya muda wake. Ingawa kwa njia ya mkataba notisi inaweza kuongezwa muda wake. Mwajiri anaweza kutoa malipo badala ya notisi. Hata hivyo mwajiri haruhusiwi kutoa notisi ya kusitisha ajira kwa mfanyakazi aliye likizo au iambatane na likizo.
- Malipo ya Kiinua Mgongo
Haya ni malipo ambayo anapaswa kulipwa mfanyakazi pindi ajira itakapositishwa. Kiinua mgongo ni jumla ya mshahara wa siku 7 kwa kila mwaka aliofanya mfanyakazi katika kipindi kisichozidi miaka 10.
Mfano
Maria ana mshahara wa Tsh.100,000/- kwa mwezi amefanya kazi kwa kipindi cha miaka 10. Je, atapata kiasi gani cha malipo ya kiinua mgongo?
Tafuta mshahara wa siku
Mshahara wa mwezi / siku za kazi katika mwezi
100,000 = 3,846
26
Kiinua mgongo
Mshahara wa siku x siku 7 kwa kila mwaka
3,846 x 7 x 10 = 269,220
Maria atalipwa kiasi cha Tsh.269,220 kama kiinua mgongo katika kipindi cha miaka 10 aliyofanya kazi.
Note; Siku za kufanya kazi ni 26 kwa mwezi kwa kuondoa siku ya Jumapili katika mzunguko wa wiki nne kwa mwezi.
Hata hivyo mwajiri hatalazimika kulipa kiinua mgongo ikiwa usitishaji huo umetokana na utovu wa kinidhamu.
- Usafirishaji mpaka eneo la kuajiriwa
Endapo mfanyakazi atasitishwa ajira mbali na eneo lile aliloajiriwa basi mwajiri anawajibika kisheria kumrudisha mfanyakazi, familia na vifaa vyake mpaka eneo lile alilomwajiri. Pia mwajiri anaweza kumlipa mfanyakazi kiasi cha kuweza kusafiri na familia yake.
- Malipo mengine
Wakati wa kusitisha ajira ya mfanyakazi, mwajiri anapaswa kuzingatia malipo yafuatayo ili yalipwe;
- Mshahara wowote ambao mfanyakazi anadai ambao aliufanyia kazi
- Likizo yoyote ile ambayo mfanyakazi hakwenda
- Malipo ya notisi ikiwa ni mbadala wa notisi
- Kiinua mgongo
- Posho ya usafiri
- Cheti cha utumishi
Mwajiri anawajibika kumpatia mfanyakazi cheti cha utumishi wakati wa kusitisha ajira. Sheria inaelekeza kuwa mwajiri ampatie mfanyakazi cheti cha utumishi. Cheti hiki mfanyakazi anaweza kukitumia katika kupata kazi sehemu nyingine ikiwa anataka kuajiriwa.
Hitimisho
Vigezo vya kisheria katika usitishaji wa ajira ni sehemu muhimu sana ya kuzingatia kwani ukiukwaji wake unaweza kuibua mgogoro. Hata hivyo ni muhimu kufahamu malipo haya ya kisheria haimaanishi ndio malipo yote anayostahili mfanyakazi wala si mbadala wa madai yake mengine ya kiajira, haya ni baadhi tu. Kwenye mikataba mengine kuna kuwa na malipo ya mkono wa heri ‘golden hand shake’ na malipo mengine. Pia mwajiri anapaswa kuhakikisha mfanyakazi wake ni mwanachama wa mifuko ya hifadhi ya kijamii ili sehemu ya mshahara wake umfae wakati wa kustaafu.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu
Wako
Isaack Zake, Wakili.
Thanks for that!!
Ahsante kwa ufafanuzi mzuri wa kisheria.. Je hiyo miaka kumi ni jumla kwa miez yake au? Kwa mfano mshahara wa siku saba ni 200000 na amefanya kwa miaka miwili itakuwa ni 200,000*2 au 200,000*24.. Msaada pliz.
Na je mwajiri anaweza akapunguza wafanyakazi kwa kigezo cha uendeshaji mbovu na kupata hasara halafu akaendelea kuajiri wapya sambamba na upunguzaji huo.
Karibu sana Fatuma Ramadhani
Nashukuru kwa swali zuri ambalo tumefafanua formula hiyo ya kiinua mgongo katika makala ya Uchambuzi wa Sheria ya Kazi;47A Madai Mengine Munimu katika Usitishaji wa Ajira. Tafadhali pitia makala hii utajifunza na mengine.
Vigezo vinavyoweza kumfanya mwajiri kupunguza wafanyakazi ni endapo anabadili mfumo kutokana na teknolojia, au hali mbaya ya kiuchumi ya kampuni, au muundo wa kampuni kubadilishwa mfano kununuliwa na kampuni nyingine. Sasa itategemea ni sababu ipi kati ya hizo ameamua kupunguza wafanyakazi, zipo ambazo zinaweza kumruhusu kuajiri ili kukidhi hali mpya ya kuendesha kampuni. Pitia makala zinazoongelea Usitishaji wa Ajira kwa Kupunguza wafanyakazi makala Namba 29A na 29 B
Karibu sana ndugu yetu
Asante kwa ufafanuzi mzuri wa hii makala ila swali langu ni je ninaweza kulipwa kiinua mgongo na mwajiri kma nimeomba kuacha kaz?