Uhuru wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku. Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Leo tunaendelea na mfululizo makala juu ya Tume hii kama uilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu tujifunze.

Uhuru wa Tume

Tume katika kutekeleza majukumu yake itakuwa huru pasipo kuingiliwa na chombo chochote au mamlaka yoyote. Uhuru huo wa Tume umeanishwa katika Katiba, Ibara ya 130(2) inayosema;

‘Tume itakuwa ni idara inayojitegemea, na bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, Tume haitalazimika kufuata maagizo au amri ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote cha siasa au taasisi nyingine yoyote ya umma au ya sekta ya binafsi’

Ufafanuzi

Kipengele hiki cha Katiba inaipa Tume nguvu ya kutekeleza majukumu yake katika kusimamia na kuchunguza mwenendo wa haki za binadamu na utawala bora nchini pasipo kuingiliwa. Uhuru wa Tume ni jambo la muhimu sana kwani zipo taasisi au ofisi za umma zinazoweza kuchunguzwa juu ya mwenendo wake, hivyo Tume inapaswa kuwa huru kama Katiba inavyosisitiza.

Kama Katiba inavyoeleza suala la uhuru wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika kutekeleza majukumu yake. Uhuru wa Tume unaipa mamlaka ya kikatiba basipo kuingiliwa na chombo chochote katika

  • Kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu kutoka mahali ppopote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  • Kuanzisha na kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora;
  • Kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu au kurekebisha haki inayotokana na uvunjwaji huo wa haki za binadamu, au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora;
  • Kuchunguza mwenendo wa mtu yeyote anayehusika au taasisi yoyote inayohusika katika kuangalia utendaji wake kama unazingatia misingi ya haki na utawala bora.
  • Kutoa ushauri kwa Serikali na vyombo vingine vya umma na vya sekta binafsi kuhusu haki za binadamu na utawala bora.

 

Hitimisho

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inayo mamlaka makubwa na ni chombo kilichoundwa na katiba na kazi zake kulindwa na Katiba ili Mamlaka nyingine za nchi zisiweze kuingilia shughuli zake na utendaji wake kwa ujumla. Mwananchi ni lazima ujue kuwa unayo fursa ya kuwasilisha malalamiko yako katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora endapo utaona haki zako au jamii zimekiukwa na mtu au taasisi ya umma au binafsi na Tume itachukua hatua stahiki kuhakikisha haki zako zinalindwa kwa mujibu wa Katiba.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia zakejr@gmail.com

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu

Wako

Isaack Zake, Wakili