Biashara Sheria. 2. Makundi ya Wahitaji wa Biashara Sheria
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji wa ukurasa mpya kabisa wa Biashara Sheria ambao unakuletea masuala kadhaa ya kisheria yanayohusiana na uanzishwaji, uendeshaji na usimamizi wa biashara au shughuli za uzalishaji mali na fedha kwa mujibu wa sheria. Katika ukurasa huu tutaendelea kutoa maarifa mbalimbali ya kusaidia wasomaji wetu kujua na kuzingatia taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa kwenye uendeshaji wa shughuli zao. Katika makala iliyopita tulieleza kwa kina juu ya malengo ya ukurasa huu, changamoto zinazoikumba sekta mbalimbali za uzalishaji kuendeshwa isivyo rasmi na kuangalia fursa au faida za kurasimisha biashara au shughuli fulani. Leo tunaenda kuangalia makundi ya watu mbalimbali tunayolenga kuwahudumia kupitia ukurasa huu wa Biashara Sheria. Karibu tujifunze kwa pamoja.
Makundi ya wahitaji wa masomo ya Biashara Sheria
Kwa uzoefu wa kutoa huduma za kisheria na kutazama mfumo wa uendeshaji wa biashara au shughuli za uzalishaji mali, yapo makundi kadhaa ambayo tumepanga kuyafikia kutokana na maarifa tutakayokuwa tunashirikishana kwenye ukurasa huu. Makundi hayo ni kama ifuatavyo;
- Watu wenye mawazo ya biashara au shughuli
Katika jamii yetu wapo watu ambao wanayo mawazo ya kibiashara au nia ya kuanzisha shughuli ya uzalishaji lakini wanakosa maarifa sahihi ya namna gani ya kisheria kuyaweka mawazo yao kimatendo. Wengi wakisikia mchakato wa kisheria unaohitajika ili biashara zao ziwe halali wanakata tamaa. Ikiwa wewe ni mmojawapo una wazo lakini hujui ni mfumo upi utakufaa kuendesha wazo lako kisheria basi ni muhimu sana kufuatilia ukurasa huu kwani tutaendelea kutoa maarifa yanayoweza kukusaidia namna bora ya kutekeleza wazo lako kwa mujibu wa sheria.
- Watu wenye biashara au shughuli ambayo haijarasimishwa
Eneo hili lina watu wengi sana wanaoendesha shughuli au biashara zao pasipo kuwa na usajili au kurasimishwa na mamlaka mbalimbali. Hapa tunazungumzia mifano mingi ya shughuli au huduma kama za wamachinga, wafanyabiashara wa masoko, mama lishe, wafanyabiashara maeneo ya standi za magari n.k. kwa kiasi kikubwa uchumi wa wanachi unazunguka kwa aina ya watu ambao wanaendesha shughuli zao katika mfumo usio rasmi. Ikiwa wewe ndugu msomaji unaendesha shughuli au biashara katika mfumo usio rasmi, basi darasa hili la Biashara Sheria linakuhusu sana kwani utajifunza faida na namna mbali mbali zinazoweza kukusaidia biashara au huduma yako kukua endapo utaifanya kuwa rasmi na kutambulika na mamlaka husika.
- Watu wenye mtaji wenye nia ya kuendesha biashara au shughuli
Wapo watu ambao wana vipato au mitaji mikubwa ya kuweza kuwekeza katika biashara au huduma za uzalishaji lakini hawana maarifa ya namna bora ya kuwekeza mitaji yao. Katika makala za ukurasa huu wa Biashara Sheria utajifunza namna nzuri za kisheria zinazoweza kukusaidia kuchukua hatua nzuri za uwekezaji wa mtaji wako kwenye huduma au biashara na kukupatia faida nzuri kwa matumizi ya baadae. Tutaeleza njia nzuri za kuanzisha biashara binafsi au za ushirika baina yako na watu wengine kwa lengo la kufikia faida nzuri ya pamoja.
- Waajiriwa wenye nia ya kuwa na biashara/shughuli nyingine ya kuingiza kipato
Lipo kundi kubwa la wafanyakazi yaani watu walioajiriwa ambao wana kiu na matamanio ya kuwa na biashara zao au huduma wanazotoa kwa jamii. Changamoto kubwa wanayoiona ni ukosefu wa muda na usimamizi bora wa huduma hizo au biashara wanazokusudia kufanya. Ikiwa ndugu yangu ni mmoja wa wafanyakazi mwenye nia hiyo basi usiache kufuatilia makala na mafundisho yanayotolewa katika ukurasa huu ambayo yatakusaidia kuanzisha na kuendesha biashara au huduma pasipo kuingilia majukumu yako ya kazi na kukupa chanzo kipya cha mapato kwa mujibu wa sheria.
Hitimisho
Katika mfululizo wa makala hizi za kwanza za Biashara Sheria tumeweza kueleza mambo ya msingi ambayo uliza sheria imejipanga kutoa maarifa ya kisheria kwa ajili ya makundi mbalimbali yanayoendesha biashara au huduma na wale ambao wanatarajia kuchukua hatua hizo. Lengo letu kubwa ni kuona biashara au huduma nyingi zinafanywa kwa mujibu wa sheria ili kusadia kwanza wale wenye biashara au huduma kukua na pia kuleta tija, ufanisi na maendeleo kwa taifa zima kwa ujumla.
Kumekuwa na dhana potofu kuwa mazingira ya ufanyaji biashara au huduma hasa ikiwa rasmi ni magumu sana kutokana na mifumo ya kodi kutofahamika vizuri kwa watu au masuala mengine mengi. Nieleze wazi kuwa kuna faida kubwa sana kwako msomaji au mfanyabiashara na mtoa huduma kuhakikisha unafanya biashara kwa mujibu wa sheria si kwa sababu ya kutotiwa hatiani kwa makosa ya kuendesha shughuli kinyume cha sheria tu bali hii inaleta dhana nzima ya uwajibikaji kwa taifa zima katika kuleta maendeleo yanayopaswa kuanzia ngazi binafsi mpaka ngazi ya taifa. Zipo fursa nzuri zaidi endapo huduma au biashara yako itakuwa rasmi na kukusaidia kukuza biashara yako siku kwa siku. Wengi kwa kutokujua hili au kwa hofu nyingine yoyote wamekuwa wakiendesha shughuli na biashara zao kwa kificho na ujanja ujanja ambao mwisho wake ni hasara kwao.
Hivyo nakukaribisha tena kuendelea kujifunza kupitia ukurasa huu katika makala zinazofuata wiki ijayo. Karibu sana.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema.
Wako
Isaack Zake, Wakili