30. Usitishaji wa Ajira kwa Notisi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala za hivi karibuni tumekuwa tukichambua sababu na taratibu mbalimbali zinazoweza kusababisha au kufuatwa ili kusitisha ajira ya mfanyakazi kihalali. Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukichambua usitishaji wa ajira unaofanywa na mwajiri. Leo tunakwenda kuangalia usitishaji wa ajira kwa Notisi. Karibu tujifunze.

Maana ya Usitishaji wa Ajira kwa Notisi

Hii ni aina mojawapo ya usitishaji wa ajira kwa kutoa taarifa kwa upande mwengine. Usitishaji huu unaweza kufanywa na mwajiri au mfanyakazi. Kama tunavyofahamu suala la ajira ni la mkataba na hakuna upande unaolazimishwa kuendelea na mkataba endapo kutakuwa na sababu zozote za msingi kutaka kusitisha mkataba huo. Hivyo basi sheria inatoa mwanya kwa upande wowote baina ya mwajiri na mfanyakazi kutoa notisi ya muda fulani kwa nia ya kutaka kusitisha mkataba wa ajira.

Utoaji wa notisi au taarifa ni kwa malengo ya kuandaa upande mwengine ili kuanza kuchukua hatua stahiki kwa nia ya kujipanga kutokana na mabadiliko ya kimahusiano yatakayokuwa mbele. Kwa mwajiri kutoa notisi kwa mfanyakazi ni kumwandaa kuanza kutafuta au kujua kuwa ajira yake inakaribia ukomo na hali kadhalika kwa mfanyakazi kutoa notisi kwa mwajiri ni kumwandaa mwajiri kutafuta mtu mwengine ambaye atachukua wajibu wa mfanyakazi anayekusudia kuacha kazi.

Kwa kawaida notisi au taarifa ya kusidio la kusitisha ajira hutolewa kwa maandishi na kueleza sababu za kukusudia kusitisha ajira na tarehe ya notisi hiyo na siku ambayo ajira hiyo itakoma.

Muda wa Notisi

Sheria ya Ajira imeweka viwango vya muda maalum ambavyo mfanyakazi na mwajiri wanapaswa kuzingatia wakati wa kutoa notisi ya kusitisha ajira. Viwango vya muda huo ni kama ifuatavyo;

  1. Notisi ya siku 7

Endapo mfanyakazi au mwajiri anakusudia kusitisha ajira ndani ya mwezi wa kwanza wa kufanya kazi basi upande wowote unaokusudia kusitisha ajira utapaswa kutoa notisi ya maandishi kwa muda usiopungua siku 7 kabla ya tarehe ya mwisho ya kufanya kazi.

 

  1. Notisi ya siku 4

Kwa mfanyakazi aliyefanya kazi zaidi ya mwezi mmoja kwa mwajiri wake na endapo malipo yake ni kwa siku au kwa wiki basi taarifa ya kusudio la kusitisha ajira inapaswa kutokupungua siku 4 kabla ya siku ya mwisho ya kufanya kazi.

  1. Notisi ya siku 28

Kwa mahusiano ya kiajira ambayo yamezidi mwezi mmoja na malipo yanayotolewa kwa mwezi basi notisi inapaswa kutokupungua siku 28 kabla ya siku ya mwisho ya kufanya kazi.

Hata hivyo sheria ya ajira inaruhusu namna nyingine ya utoaji wa taarifa endapo pande zote zitakubaliana. Ipo mikataba ya ajira ambayo inasema juu ya notisi kutolewa katika kipindi kisichopungua miezi mitatu. Hivyo matakwa ya kwenye mkataba wa ajira yataheshimiwa na pande zote.

Sheria ya Ajira inatoa katazo la kusitisha ajira wakati wa likizo au kutoa notisi ya kusitisha ajira ikiwa sambamba na likizo.

Hatahivyo, mwajiri anaweza kusitisha ajira ya mfanyakazi na kumlipa msharara badala ya notisi au taarifa. Hii ina maana kama mwajiri anakusudia kusitisha ajira ya mfanyakazi mwezi Machi 2018 basi atawajibika kumlipa mfanyakazi mshahara wa mwezi huu Februari 2018 ambao mfanyakazi ataufanyia kazi na pia kumpa nyongeza ya mshahara wa mwezi Machi 2018 ambao mfanyakazi hatoufanyia kazi.

Hitimisho

Usitishaji wa ajira kwa njia ya notisi ni mojawapo ya njia za usitishaji wa ajira ambao pande zote zina haki ya kuutumia. Mfanyakazi asiyeridhika na usitishaji wa ajira kwa njia hii anayo haki ya kuwasilisha mgogoro wake katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kwa ajili ya utatuzi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.