31. Kusimamishwa Kazi kwa Mfanyakazi

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Kwa kipindi kirefu tumejifunza njia mbalimbali za usitishaji wa ajira. Leo tunakwenda kuangalia juu ya kusimamishwa kazi kwa mfanyakazi. Karibu tujifunze.

Maana ya Kusimamishwa Kazi

Kusimamishwa kazi au kusimamisha kazi ni kitendo kinachofanywa na mwajiri dhidi ya mfanyakazi kwa kutokumruhusu kuendelea na majukumu yake ya kila siku kwa kipindi fulani. Mwajiri anayo haki ya kumsimamisha kazi mfanyakazi, hata hivyo ni lazima kusimamishwa huku kazi kuambatane na sababu za msingi.

Sababu za Kusimamishwa Kazi

Mwajiri ni lazima atoe sababu za kumsimamisha mfanyakazi majukumu yake ya kila siku. Sheria ya kazi inatambua sababu kuu mbili za usiamimamishaji wa kazi;

  1. Kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi

Endapo kutajitokeza mazingira ambayo yanahusiana na utendaji au uwezo wa mfanyakazi katika utendaji wake na kusababisha makosa kwa mwajiri ndipo mwajiri anaweza kumsimamisha mfanyakazi ili kupisha uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili.

  • Endapo kuwepo kwa mfanyakazi mahali pa kazi kunaweza kuathiri uchunguzi dhidi yake
  • Kuendelea kutekeleza majukumu mahali pa kazi kunaweza kuleta tatizo wakati uchunguzi unaendelea.

 

  1. Kusimamishwa kazi kama adhabu

Kusimamishwa kazi kama adhabu ni pale ambapo tayari makosa ya mfanyakazi yamedhibitika kuhusiana na tuhuma au suala fulani, ndipo mwajiri anaweza kumsimamisha kazi mfanyakazi kama adhabu kutokana na makosa hayo.

Ni muhimu kufahamu kuwa mfanyakazi anayesimamishwa kazi kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili anapaswa kulipwa mshahara wake wote na marupurupu yote kama vile ambavyo yupo kazini. Hata hivyo mfanyakazi anayesimamishwa kazi kwa sababu ya adhabu hastahili kulipwa mshahara katika kipindi alichosimamishwa kazi.

Hatua za kuzingatia wakati wa kusimamisha kazi

  • Mwajiri lazima ampatie mfanyakazi taarifa au barua ya kumsimamisha kazi inayoeleza sababu ya kumsimamisha kazi na masharti mengine ya kusimamishwa kazi.
  • Kwamba kipindi cha kusimamishwa kazi kiwe cha wastani kuwezesha suala la uchunguzi au adhabu kuweza kutekelezwa
  • Endapo mfanyakazi anashtakiwa kwa makosa ya kijinai yanayohusiana na kazi basi mwajiri anaweza kumsimamisha kazi lakini kwa kumlipa mshahara wake wote na marupurupu yake mpaka kesi itakapomalizika.

Hitimisho

Kusimamisha kazi kwa mfanyakazi ni sehemu ya haki ya mwajiri kutokana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika mahusiano ya kiajira. Ni wazi kuwa waajiri wengi wanatumia vibaya madaraka haya ya kusimamisha kazi wafanyakazi hata pasipokuzingatia sababu za kisheria ambazo zimeainishwa hapa. Tunashuhudia waajiri wakisimamisha wafanyakazi kutokana na sababu za kifamilia au nyingine zozote ambazo hazihusiani na kazi. Pia waajiri wanaposimamisha wafanyakazi kazi hakuna uchunguzi wowote unaoendelea wala hakuna malipo kwa wafanyakazi. Mfanyakazi unayesimamishwa kazi ni lazima ujue sababu na endapo hujapatiwa basi chukua hatua za kisheria dhidi ya mwajiri.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.