Biashara Sheria.3. Mfumo wa Uendeshaji Biashara Kisheria

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Katika makala zilizopita tuliona juu ya utangulizi kuhusu malengo ya ukurasa huu na hasa wahitaji wa maarifa haya ya uendeshaji wa biashara au shughuli za uzalishaji mali kwa mujibu wa sheria. Tumeona juu ya watu wengi wanaendesha biashara au shughuli zao pasipo kuwa na usajili au kutambulika kisheria. Leo tunaenda kuangalia kwa kifupi juu ya mifumo ya uendeshaji biashara kisheria. Karibu tujifunze.

Mfumo wa Biashara Kisheria

Katika uendeshaji biashara, sheria inatambua makundi kadhaa ya uendeshaji biashara ambayo yanaweza kuendeshwa au kusajiliwa na Mamlaka ya Usajili wa Biashara yaani BRELA.

Sheria imeunda chombo cha kufanya usajili wa biashara  kinachojulikana kama ‘Business Registrations and Licensing Agency’ BRELA. Chombo hiki ndicho chenye mamlaka ya usajili wa biashara zote zinazofanya kazi nchini Tanzania.

Biashara au shughuli za uzalishaji mali zinazosajiliwa na mamlaka ya BRELA ni kama ifuatavyo;

  1. Biashara ya mtu Binafsi

Mamlaka ya usajili wa biashara inasajili biashara ambayo inaendeshwa na mtu binafsi. Biashara hii au usajili huu unaitwa kwa lugha ya kiingereza ‘Sole Proprietorship’. Hii ni ngazi ya chini kabisa katika uendeshaji wa biashara. Katika mfumo wa biashara hii inahusisha mtu mmoja ambaye anasimamia biashara yake mwenyewe katika kuiendesha siku kwa siku.

  1. Biashara ya Ubia

Mamlaka ya usajili wa biashara pia inasajili biashara au uendeshaji wa huduma unaofanyika kupitia ubia yaani ‘Partnership’. Huu ni mfumo wa biashara au uendeshaji wa shughuli unaofanywa na watu wawili au zaidi kwa malengo ya kibiashara au utoaji wa huduma fulani. Hivyo watu wawili au zaidi wanaweza kuwa na malengo yao ya kibiashara na wakataka kufanya kazi pamoja wanaweza kuendesha shughuli yao kwa ubia.

 

 

  1. Kampuni

Huu ni mfumo mwengine wa uendeshaji wa biashara au huduma ya uzalishaji katika jamii unaoweza kusajiliwa na Mamlaka ya Usajili yaani BRELA. Kampuni ndio mfumo wa biashara wa juu ambao wadau wa kampuni wanaweza kutumia kuanzisha shirika/kampuni na kufanya kazi kwa niaba yao kama chombo kinachojitegemea katika kufanikisha malengo ya kibiashara. Ili kuanzisha kampuni inaanzia idadi ya wadau wawili na kuendelea.

Wafanyabiashara wengi katika jamii yetu wanaangukia katika mfumo wa kwanza yaani biashara binafsi ‘Sole Proprietorship’ ambazo ndizo wanaendesha maisha yao ya siku kwa siku. Pamoja na kwamba wengi wako katika utendaji kwenye mfumo wa biashara binafsi si wote wamesajili shuguli zao na kutambuliwa na mamlaka ya usajili BRELA katika uendeshaji wa shughuli zao. Tutaendelea kuchambua faida na hasara za kila mfumo wa kibiashara ambao mtu anatumia au anakusudia kuutumia kuzalisha mali au kuendesha shughuli zake katika makala zinazokuja.

Hitimisho

Leo tumeona aina kuu 3 za mfumo wa uendeshaji wa biashara yaani biashara binafsi, biashara kwa njia ya ubia na biashara kupitia kampuni. Mfumo huu wa biashara au shughuli za uzalishaji ndio unatumika mahali pote. Katika makala zinazofuata tutaendelea kuzichambua kila moja na vigezo ambavyo mtu anapaswa kuwa navyo ili kuweza kusajili biashara mojawapo kati ya hizo.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Tumain J.Anthony
    Tumain J.Anthony says:

    Asante sana Isack, Nimejifunza kitu hapa.Nilikuwa sijui mifumo ya biashara kisheria leo nimeifahamu vyema. Mungu akubariki sana.

Comments are closed.