35. Hatua za Usuluhishi

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya mchakato wa utatuzi wa mgogoro kwa njia ya usuluhishi. Tuliona juu namna mgogoro unavyowasilishwa na mambo muhimu ya kuzingatia. Leo tunaangalia juu ya taratibu za Usuluhishi. Karibu tujifunze.

Hatua za Usuluhishi

Kama tulivyoeleza juu ya maana ya usuluhishi katika makala zilizopita ambapo mchakato huu unahusisha uwepo wa mtu ambaye hana upande wowote kusaidia mwajiri na mfanyakazi kufikia makubaliano katika mgogoro wa kiajira ulio mbele yake.

Kwa mujibu wa sheria za Ajira, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ndio ina jukumu la kufanya usuluhishi. Wapo wasuluhishi ambao ni waajiriwa wa Tume wenye mamlaka ya kufanya usuluhishi.

Mchakato wa usuluhishi unaanza pale wadaawa wameitwa kwa siku na muda unaooneshwa kwenye hati ya wito ‘summons’ kuja mbele ya Msuluhishi.

  1. Utambulisho/ Dhana ya Usuluhishi

Sheria ya Ajira inamwelekeza Msuluhishi kufanya utambulisho wa wadaawa na kuwakaribisha katika usuluhishi. Mara nyingi wadaawa wanapokuja katika shauri tayari wana misimamo yao na hali ya uadui ilishajengeka katika fikra zao. Ni kazi ya msuluhishi kueleza vizuri juu ya dhana ya usuluhishi pande zote zikaelewa faida na hasara zake kama zipo. Mfano usuluhishi ni njia pekee katika utatuzi inayoacha walau hali njema ya mahusiano kati ya mwajiri na mfanyakazi, pia inaokoa muda wa Tume na wadaawa pia. Changamoto ya usuluhishi ni kwamba kila mmoja akubali kupata na kupoteza. Huwezi kwenda meza ya usuluhishi kutegemea madai yako yote yatatimizwa kama ulivyoomba kwenye CMA Form 1.

Katika ngazi hii msuluhishi anawaeleza pande zote kuwa watazungumza kirafiki na kuona namna bora ya kutatua tatizo lililopo bila kulaumiana au kuonyeshana kidole.

  1. Kikao cha pamoja

Baada ya utambulisho na maelezo ya kina juu ya dhana ya usuluhishi. Msuluhishi ataanza kuwasikiliza wadaawa juu ya mapendekezo yao namna bora ya kumaliza mgogoro kwa amani. Mfano mfanyakazi anadai mishahara ya miezi 12 kama fidia ya kuachishwa kazi pasipo utaratibu kwenye usuluhishi mfanyakazi anaweza kupendekeza alipwe walau mishahara ya miezi 10 na mwajiri anaweza kupendekeza kulipa miezi 6 ili wamalize kwa usuluhishi. Kama nilivyoeleza katika hatua ya usuluhishi hayazungumzwi masuala ya kisheria bali namna gani mmnalize bila kupitia masuala ya ushahidi na kisheria.

 

  1. Kikao cha mmoja mmoja

Inapoonekana kuwa pande zote zinashindwa kufikia mwafaka wa namna ya kumaliza tatizo, msuluhishi anaweza kufanya kikao na upande mmoja na kisha na upande mwengine ili kuzielewa hoja zao na kutoa ushauri pia pasipo kueleza kwa upande mwengine yale aliyozungumza wakati mwengine hayupo. Hili ni muhimu kulifahamu na kulielewa kama msuluhishi na wadaawa maana wengine wanadhani huo ni muda ambao msuluhishi anataka kupendelea upande mmoja au mwengine. Ndio maana ni msingi kwa msuluhishi kueleza hatua zote atakazofanya wakati wa usuluhishi mwazoni

  1. Majumuisho

Endapo pande zote zitaafikiana basi msuluhishi atayaandaa makubaliano kama walivyokubaliana katika fomu maalum CMA Form No.5. Fomu hii itajazwa na msuluhishi na kusainiwa na wadaawa na wawakilishi wao endapo watakuwepo wakati wa usuluhishi.

Ikiwa pande hizi hazitaafikiana katika hatua ya usuluhishi basi, msuluhishi anaweza kuwapa muda wa kutafakari na kuhairisha shauri lao. Ikishindikana pia kwenye kikao kingine basi msuluhishi anaweza kujaza fomu husika kwamba mgogoro umeshindikana kusuluhishwa.

Ikumbukuwe kuwa mgogoro unapaswa kusuluhishwa ndani ya siku 30 tangu kuanza hatua za usuluhishi.

 

Hitimisho

Usuluhishi ni hatua njema sana kwa ajili kumaliza mgogoro wa kikazi baina ya mwajiri na mfanyakazi kama njia hii ikitumiwa vizuri italeta faida na tija kwa pande zote. Changamoto kubwa ambayo ipo katika ngazi ya usuluhishi ni uwepo wa wakilishi wa pande mbili ambao wamekuwa wakilaumiwa kufanya usuluhishi kuwa mgumu kwani kila mmoja anavutia maslahi yake kwa kumshawishi mteja wake vinginevyo.

Usikose kufuatilia makala nyingine ya ufafanuzi juu ya usuluhishi kama njia ya kutatua mgogoro wa kazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.