36. Utatuzi wa Migogoro ya Kazi kwa njia ya Uamuzi

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia hatua za usuluhishi. Leo tunaendelea kuchambua kila njia ya utatuzi wa mgogoro kwa Uamuzi ‘Arbitration’. Karibu tujifunze.

Uamuzi

Hii ni njia ya pili inayotumika katika utatuzi wa migogoro ya kazi. Kwa kawaida migogoro ya kazi huanza na hatua ya Usuluhishi na pale ambapo usuluhishi unashindikana basi njia hii ya Uamuzi hutumika. Taasisi yenye mamlaka ya kufanya uamuzi kwa mujibu wa sheria za kazi ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ‘The Commission for Mediation and Arbitration’ CMA.

Maana ya Uamuzi kama ilivyo kwa usuluhishi pia ni mchakato ambapo anateuliwa mtu huru ambaye hafungamani na upande wowote wa wadaawa ambaye atakuwa na kazi ya kusikiliza hoja ya pande zote na kutoa uamuzi wake kulingana na sheria za Ajira.

Katika hatua ya Uamuzi tofauti na usuluhishi, mwamuzi anayo mamlaka ya juu kwani hatoi ushauri bali atasikiliza ushahidi wa pande zote na kutoa maamuzi yake kwa mujibu wa sheria za Ajira. Uamuzi unahusisha utoaji wa ushahidi ikiwa ni wa mdomo na vielelezo, uamuzi au TUZO anayotoa mwamuzi pamoja na sababu za uamuzi huo kwa mujibu wa sheria.

Hatua za kufikia ngazi ya Uamuzi

Zipo hatua ambazo anapaswa kuzingatia mwajiri au mfanyakazi zinazoongozwa na sheria za Ajira ili kumwezesha mgogoro wake kuwasilishwa Tume kwa ajili ya uamuzi.

Sheria ya Ajira kwa kupitia kanuni zake za Tangazo la Serikali Na.47/2017 imeandaa fomu maalum kuhusiana na uwasilishwaji wa migogoro mbele ya Tume chini ya Kanuni ya 34(1).

  1. Cheti cha Kutosuluhishwa

Sheria ya Ajira imeandaa fomu maalum ambayo hujazwa na Msuluhishi pale mgogoro unaposhindikana kusuluhishwa, hii ni   CMA Form No.6. mara baada ya fomu hii ya kuonesha mgogoro haujasuluhishwa, basi yeyote yule kati ya mwajiri au mfanyakazi anaweza kuchua hatua za ziada kwa ngazi ya uamuzi.

  1. Notisi ya kuwasilisha Mgogoro ngazi ya Uamuzi

Mara baada ya mgogoro kushindikana kusuluhishwa, upande ule unaoathirika kutokana na kutosuluhishwa mgogoro unaweza kutoa notisi kwa Tume na upande mwengine juu ya kuwasilisha mgogoro kwenye ngazi ya Uamuzi. Uwasilishwaji huu unafanywa kupitia CMA. Form. No.8 ambayo inatakiwa kuwasilishwa mbele ya Tume ndani ya siku 30 baada ya kushindikana usuluhishi.

  1. Tume kuteua Mwamuzi wa mgogoro wa Kazi

Mara baada ya notisi ya uamuzi kuwasilishwa mbele ya Tume, Tume itafanya mchakato wa kumteua mwamuzi ambaye ni tofauti na yule aliyesuluhisha mgogoro wa kazi hapo awali.

  1. Kupata wito wa kuitwa mbele ya Tume kwa ajili ya Uamuzi

Mwamuzi aliyeteuliwa na Tume kusikiliza mgogoro wa kazi ataandika wito ‘summons’ wa kuita pande zote mbele ya Tume kwa ajili ya kuanza mchakato wa uamuzi kwa mujibu wa sheria za Ajira.

 

Hitimisho

Leo tumejifunza mchakato wa hatua ya uamuzi katika utatuzi wa migogoro ya kazi. Kumekuwa na makosa ya wengi mara baada ya usuluhishi kushindwa nao hawachukui hatua zaidi. Inapaswa kujaza fomu maalum ili shauri lako liende katika ngazi ya uamuzi ambapo pande zote mbili watapewa nafasi ya kuwasilisha maelezo, vielelezo na hoja zao za msingi ili Tume kupata fursa ya kuamua kwa mujibu wa sheria za Ajira.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.

 

 

 

 

 

4 replies
  1. Baraka issa
    Baraka issa says:

    Habari mhe. Mimi ni mwakilishi mchanga wa chama cha wafanyakazi kiukweli nitoe shukrani zangu za dhati kwako kwaninumekuwa msaada mkubwa sana kwangu, matarajio yangu ni kuwa mwanasheria mbobevu so naamn chini ya darasa laki hili lengo langu litatimia.nikwa namna gani tunaweza kuwa na machapisho yako? Mfano majarida? Ubarikiwe sana.

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Karibu sana ndugu Baraka Issa
      Mwaka huu tumejipanga kuanza kutoa machapisho/vitabu ambavyo wadau wanaweza kutumia kama rejea katika masuala yao ya kazi ikiwa ni wafanyakazi, waajiri au wawakilishi.
      Karibu sana

Comments are closed.