37. Hatua za Uamuzi
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya mchakato wa utatuzi wa mgogoro kwa njia ya uamuzi. Tuliona juu namna mgogoro unavyowasilishwa kwenye ngazi ya uamuzi. Leo tunaangalia juu ya taratibu za Uamuzi. Karibu tujifunze.
Hatua za Uamuzi
Kama tulivyoeleza juu ya maana ya uamuzi katika makala zilizopita ambapo mchakato huu unahusisha uwepo wa mtu ambaye hana upande wowote kwa ajili ya kuamua mgogoro wa kiajira baina ya mwajiri na mfanyakazi kwa mujibu wa sheria za kazi.
Kwa mujibu wa sheria za Ajira, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ndio ina jukumu la kufanya uamuzi wa mgogoro wa kikazi. Wapo waamuzi ambao ni waajiriwa wa Tume wenye mamlaka ya kufanya uamuzi.
Mchakato wa uamuzi unaanza pale wadaawa wameitwa kwa siku na muda unaooneshwa kwenye hati ya wito ‘summons’ kuja mbele ya Mwamuzi.
- Utangulizi
Sheria ya Ajira na kanuni zake inaleza kuwa mchakato wa uamuzi unaanza na hatua ya kwanza ya utangulizi. Katika hatua hii mwamuzi atachukua jukumu la kuwakaribisha wadaawa na wawakilishi wake na kutoa maelezo mafupi juu ya mchakato mzima wa uamuzi utakavyokuwa. Katika hatua hii pande zote zinakubaliana juu ya lugha itakayotumika katika mchakato wa uamuzi na endapo patahitajiwa mkalimani basi Tume itafanya utaratibu husika.
- Hoja za awali na Viini vya Mgogoro
Baada ya utambulisho na utangulizi ambao mwamuzi anaufanya siku ya kwanza ya kukutana na wadaawa. Mwamuzi atawataka wadaawa kuwasilisha hoja za awali zinazoelezea historia ya mgogoro kwa kila upande na hasa ni nini viini vya kisheria au hoja ambazo zinabishaniwa na kila upande. Hoja hizi huwasilishwa kwa maandishi ndani ya muda maalum ambao Mwamuzi atawataka pande husika kuwasilisha. Katika uwasilishaji wa hoja za awali, mdaawa ataeleza kwa ufupi juu ya historia ya mahusiano ya kiajira na namna tatizo au mgogoro ulivyoibuka na vitu ambavyo angependa Tume au Mwamuzi avizingatie kama viini vya mgogoro. Kisha upande utapendekeza juu ya nafuu ambazo ungependa Tume kutoa kutokana na mgogoro husika. Hapa kila upande unaweza kuwasilisha nakala ya vielelezo ambavyo unakusudia kuvitumia.
- Ushahidi
Hii ni hatua muhimu sana kwa kila upande ambapo utaleta mashahidi mbele ya Tume kudhibitisha au kukanusha kile ambacho upande mwengine unatuhumu. Ni muhimu sana wakati wa ushahidi pande zote kuzingatia mambo muhimu ambayo yatasaidia kushawishi hoja zake kukubalika mbele ya Tume. Hapa mashahidi watatoa ushahidi wao kwa njia yam domo na kama kuna nyaraka ambazo watahitaji kuzitumia kama ushahidi basi huu ndio wakati wa kuzitoa na kuzitolea maelezo. Wengi wanakosea katika hatua hii wanadhani kwa kuwa waliwasilisha vielelezo kwenye hoja za awali basi hawana haja ya kuvizungumzia. Katika ngazi ya ushahidi ndipo vielelezo vile vinafanya kazi kwa kutolewa na kukubaliwa na Tume kama sehemu ya ushahidi.
- Majumuisho/Hoja za Mwisho
Baada ya hatua za ushahidi wa pande zote ndipo, Tume au Mwamuzi kwa utaratibu anawapa tena wadaawa nafasi ya kuandaa majumuisho au hoja za mwisho. Hapa kila upande unafafanua msingi wa hoja zake na kwa nini Tume iamue kwa upande wake. Hapa mdaawa anaeleza hoja zake kulinganisha na ushahidi au vielelezo vilivyowasilishwa pamoja na mizania ya sheria za kazi. Hapa unazingatia na mifano ya mashauri ambayo yalipita yanayofanana na mgogoro husika na kueleza Tume kwa nini inapaswa kuamua kutokana na upande wako.
- Uamuzi/ Tuzo
Hii ni ngazi ya mwisho mara baada ya kumalizika kwa hatua zote hapo juu. Hii ni sehemu ya kazi ya Mwamuzi kukaa chini na kuchambua maelezo, ushahidi, vielelezo na sheria za ajira zinavyoeleza juu ya mgogoro husika na kutoa maamuzi. Maamuzi ya Tume yanaitwa kwa lugha nyingine Tuzo ‘Award’. Tuzo hii inazifunga pande zote na ni lazima itekelezwe kama amri nyingine yoyote ya mahakama.
Hitimisho
Uamuzi wa Tume au Tuzo ni matokeo ya mwisho wa mchakato mzima wa utatuzi wa mgogoro kwa njia ya uamuzi. Hapa Tume lazima iweke bayana kuwa ni upande upi ni sahihi au upande upi umekiuka taratibu za sheria za kazi katika shauri husika. Kwa kawaida Tuzo hupaswa kutolewa ndani ya siku 30 mara baada ya kuwasilishwa kwa hoja za mwisho. Utatuzi wa mgogoro wa kazi kwa njia ya uamuzi ni mojawapo ya njia ambazo pande zote zinatoa ushahidi na kuleta vielelezo husika. Hapa ni kama mfumo mwengine kwani kuna kushindwa au kushinda toafuti na mfumo au ngazi ya usuluhishi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.