38. Madhara ya Kutokuudhuria Usuluhishi na Uamuzi

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu ya mchakato wa utatuzi wa mgogoro kwa njia ya uamuzi. Tuliona juu ya hatua za Uamuzi. Leo tunaenda kuangalia juu ya athari zinazokumba pande zile ambazo haziudhurii katika hatua ya usuluhishi au uamuzi.

 

Sheria ya Ajira na kanuni zake zimewekwa kwa lengo la kusaidia pande zote kufuata mchakato wa haki katika kutatua mgogoro wa kiajira ikiwa ni usuluhisi au uamuzi.

Yapo mazingira ambayo yanajitokeza kwa upande uliowasilisha mgogoro au upande ambao unalalamikiwa kushindwa kuudhuria kwenye usuluhishi au uamuzi pasipo kuwa na sababu za msingi. Kanuni zinazohusiana na kuendesha mashauri ngazi ya usuluhishi na uamuzi zinaeleza utaratibu unaopaswa kuchukuliwa na msuluhishi au mwamuzi endapo hali hii itajitokeza.

  1. Athari za kutokuudhuria usuluhishi

Sheria ya Ajira kupitia kanuni zinazoongoza masuala ya usuluhishi zinaeleza juu ya athari zinazojitokeza kwa upande kutokuudhuria shauri wakati wa usuluhishi.

Athari za kutokuudhuria usuluhisi zinatokana na aina ya mgogoro uliopo mbele ya Msuluhishi.

Endapo mgogoro ulio mbele ya msuluhishi ni mgogoro wa maslahi basi kanuni zinamtaka msuluhishi kufanya ifuatavyo

  • Iwapo aliyeshindwa kuudhuria ni mlalamikaji, msuluhishi anaweza kuongeza siku 30 zaidi ya zile ambazo zinatakiwa kutumika katika usuluhishi

 

  • Iwapo aliyeshindwa kuudhuria ni mlalamikiwa, msuluhishi anaweza kupunguza siku za usuluhishi.

Endapo mgogoro ulio mbele ya msuluhishi ni lalamiko au mgogoro wa haki, msuluhishi anapaswa kufanya yafuatayo;

  • Iwapo aliyeshindwa kuudhuria ni mlalamikaji, msuluhishi anaweza kuutupilia mbali mgogoro husika

 

  • Iwapo aliyeshindwa kuudhuria ni mlalamikiwa, msuluhishi anaweza kusikiliza shauri upande mmoja.

 

  1. Athari za kutokuudhuria uamuzi

Sheria ya Ajira na kanuni zake inaeleza pia athari za pande za mgogoro wa kiajira kwenye ngazi ya uamuzi kwa kutokuudhuria kwenye shauri.

  • Iwapo aliyeshindwa kuudhuria ni mlalamikaji, mwamuzi anaweza kuutupilia mbali mgogoro husika

 

  • Iwapo aliyeshindwa kuudhuria ni mlalamikiwa, mwamuzi anaweza kusikiliza shauri upande mmoja.

Hatahivyo katika kufanya maamuzi haya Tume ni muhimu kujiridhisha wakati wote kuwa kila upande umepata taarifa sahihi juu ya uwepo wa shauri na siku ambayo wanapaswa kuudhuria.

Endapo itatokea mdaawa akaumizwa na maamuzi ya Tume ya kutupilia mbali mgogoro kwa kutokuudhuria au kuusikiliza upande mmoja, yule aliyeathiriwa na maamuzi hayo anayo nafasi ya kuleta maombi mbele ya Tume katika siku 14 baada ya uamuzi husika, na iwapo ataonesha sababu za msingi Tume inaweza kutengua maamuzi yake.

 

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa kazi kuwa makini na kufuata mwongozo wa kuudhuria mashauri kama wanavyotakiwa. Kumekuwa na tabia ambayo hasa inafanywa na waajiri ya kutokuzingatia wito mbele ya Tume. Hii inasababisha usumbufu mkubwa sana na kuleta mlolongo mrefu wa utatuzi wa migogoro ya ajira.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.