Biashara Sheria.7. Makundi ya Kampuni

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Katika makala iliyopita tumeona mfumo wa uendeshaji biashara na mamlaka inayohusika na usajili wa biashara hizo. Tumeona juu ya makundi makuu 3 ya uendeshaji wa biashara kisheria na usajili wake. Pia tumeangalia juu ya uchambuzi wa mifumo ya biashara binafsi na ile ya ubia na hata mfumo wa kampuni. Leo tunakwenda kuchambua juu ya makundi ya kampuni .Karibu tujifunze.

Biashara ya Kampuni

Kama tulivyoweza kueleza katika makala zilizotangulia juu ya mfumo wa biashara au kuendesha shughuli kupitia kampuni kwamba huu ni mfumo wa hali ya juu zaidi kuliko mifumo mingine. Kampuni inabeba jila lake, malengo yake na namna ya utendaji wake ambao ni tofauti na wamiliki wake.

Katika kuelewa namna kampuni zinavyofanya kazi, yapo makundi ya kampuni ambayo yanaweza kuelezwa na kutofautisha juu ya asili na utendaji wa kampuni husika. Tanzania kama nchi nyingine inayo mamlaka maalum ya usajili wa kampuni ambapo zinasajiliwa kampuni za aina mbalimbali.

Katika makala hii tunakwenda kuagalia juu ya mgawanyo wa kampuni katika makundi yake.

Makundi ya Kampuni

Zipo namna mbalimbali za kugawanya au kuanisha aina za makundi ya kampuni. Kwa mujibu wa makala hii na utaratibu wa usajili wa kampuni nchini Tanzania, kampuni zinaweza kugawanywa katika makundi yafuatayo;

  1. Mgawanyo wa kampuni kwa asili

Kundi hili linazungumzia juu ya usajili wa kampuni. Hii ina maana ni wapi kampuni husika imesajiliwa kwa mara ya kwanza. Hapa tuna aina mbili za kampuni

  • Kampuni iliyosajiliwa ndani ya nchi ya Tanzania. Hii inajulikana kama ‘local company’. Hili ni kundi la kampuni ambalo kuanzishwa kwake na kusajiliwa hufanyika ndani ya Tanzania.

 

  • Kampuni iliyosajiliwa nje ya nchi ya Tanzania. Hii pia inajulikana kama ‘foreign company’ yaani kampuni ambayo kwa mara ya kwanza imesajiliwa nchi nyingine. Kampuni za aina hii zina mfumo wa kusajiliwa au kutambuliwa kwa shughuli zake katika nchi ile ambayo inaenda kupanua shughuli zake.

 

  1. Mgawanyo wa kampuni kwa ukomo wa madeni

Hili ni kundi la pili katika mgawanyo wa kampuni zinazosajiliwa Tanzania. Kama tulivyoeleza kuwa moja ya sifa ya kampuni ni hali ya ukomo wa madeni kuishia kwenye kampuni husika na kutokuwaathiri wamiliki wa kampuni. Katika kundi hili tunapata tena aina mbili ya kampuni

  • Ukomo wa madeni ndani ya kampuni

Aina hii ya kampuni ni ile ambayo madeni yanapojitokeza yataishia kulipwa na kampuni husika kupitia mali zake na kiasi cha umiliki cha wamiliki wake na si vinginevyo. Hizi ni kampuni ambazo zinajulikana kama ‘limited companies’. Hapa kampuni ikifilisika basi ni kiasi kile cha fedha au mtaji au mali za kampuni ndicho kitahusika na ulipaji wa madai au madeni yoyote ya kampuni.

  • Ukomo wa madeni kwa wamiliki wa kampuni

Aina hii ya kampuni ni ile ambapo madeni yakijitokeza basi kampuni itahusika kulipa pamoja na wamiliki wake pia. Endapo kampuni itafilisika basi hata wamiliki wake watachangia kwa mali zao kulipa madai yote ya kampuni. Aina hii zinajulikana kama ‘unlimited companies’

  1. Mgawanyo wa kampuni kwa umiliki

Kundi hili linazungumzia juu ya aina ya umiliki wa kampuni. Katika kundi hili tunapata aina mbili za umiliki wa kampuni yaani kampuni binafsi na kampuni za umma.

  • Kampuni binafsi

Endapo kampuni itasajiliwa na kuonesha idadi ya manahisa ni 2-50 basi kampuni hiyo itahesabika kama ni kampuni binafsi. Kwa kawaida sheria ya makampuni inaeleza kuwa namba ya chini kabisa ya kuweza kuanzisha kampuni ni angalau watu 2. Kampuni binafsi inakuwa na wanahisa wasiopungua 2 na wasiozidi 50.

  • Kampuni za umma

Kampuni ya umma ni aina ya kampuni ambayo wanahisa wanazidi idadi ya watu 50. Tumeona mifano mingi ya aina za makampuni ambayo yalikuwa binafsi na kubadilishwa kuwa kampuni za umma kwa kuongeza idadi ya wanahisa.

 

Hitimisho

Leo tumeendelea kujifunza zaidi juu ya makundi ya kampuni na namna zinavyogawanywa kwa minajili ya usajili. Kwa kupata ufahamu huu utakusaidia ndugu msomaji kujua ni aina gani au kundi gani la kampuni ungependa kuwa nalo kulingana na matarajio yako ya kibiashara. Usiache kufuatilia zaidi makala hizi tuendelee kujifunza zaidi juu ya makampuni.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili