39. Hadhi ya Tuzo katika ngazi ya Uamuzi

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu  ya athari zinazokumba pande zile ambazo haziudhurii katika hatua ya usuluhishi au uamuzi. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Hadhi ya Tuzo katika ngazi ya Uamuzi.

Maana ya Tuzo

Tuzo ni uamuzi unaofikiwa na mwamuzi katika mgogoro wa kazi kwenye ngazi ya uamuzi. Kwa lugha ya kiingereza inaitwa ‘Award’. Kama tulivyoeleza kwenye makala za utangulizi kuwa mgogoro wa kazi mbele ya Tume una ngazi mbili muhimu yaani usuluhishi na uamuzi. Tumechambua kwa kirefu juu ya usuluhisi na kuonesha mchakato wake. Vivyo hivyo katika mchakato wa uamuzi zipo ngazi na hatua za kufuata ambazo tulizijadili.

Ili tuzo iwe kamili kwa mujibu wa sheria za kazi inapaswa kuwa au kuonekana na vitu vifuatavyo;

  • Majina ya wadaawa na nafasi zao
  • Viini vya mgogoro baina ya pande mbili
  • Maelezo ya awali ambayo pande zote zinakubalina
  • Muhtasari wa pande zote mbili juu ya ushahidi na hoja zao
  • Sababu za uamuzi
  • Amri ya mwamuzi katika Tuzo

Tuzo ya Tume katika ngazi ya uamuzi ina nguvu ya kisheria ya kuzibana pande zote mbili kama ulivyo uamuzi wa mahakama nyingine yoyote.

Mara baada ya Tuzo kutolewa, mwamuzi anatoa amri ya kutekeleza yale yaliyo ndani ya Tuzo kwa upande ulioshindwa shauri ndani ya muda fulani. Endapo amri iliyo ndani ya Tuzo haijatekelezwa, basi upande ulioshinda unaweza kuchukua hatua za ziada kwa kufungua shauri la kukazia Tuzo mbele ya Mahakama Kuu ya Kazi ili kumlazimisha aliyeshindwa kutekeleza matakwa ya Tuzo.

Nini kifanyike endapo hujaridhishwa na Tuzo?

Endapo mdaawa katika shauri la kazi mbele ya Tume hajaridhika na Tuzo ya Mwamuzi anaweza kuchukua hatua ya kuomba marejeo mbele ya Mahakama Kuu ya Kazi. Ieleweke kuwa hakuna utaratibu wa rufaa kutoka maamuzi ya Tume kwenda Mahakama Kuu ya Kazi bali kuna haki ya Marejeo.

Mdaawa ambaye hajaridhika na uamuzi husika anapaswa kuchukua hatua za kuomba marejeo ndani ya wiki 6 mara baada ya kupata Tuzo husika.

 

Hitimisho

Tuzo katika ngazi ya uamuzi ni hatua muhimu sana katika kukamilisha mchakato wa mgogoro wa kiajira mbele ya Tume. Hatahivyo, kuwa na Tuzo mkononi hakumaanishi tayari umepata haki yao au amri imetekelezwa inapobidi utahusika kufungua shauri mbele ya Mahakama ya Kazi kwa ajili ya utelekelezaji zaidi. Ni muhimu kwa pande zote mara baada ya kupata Tuzo, kuitekeleza ndani ya muda au kama hujaridhika kufanya mchakato wa marejeo ili kuepuka usumbufu usio wa lazima kwa Tume na Mahakama ya Kazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.