Biashara Sheria.8. Aina za Kampuni

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Katika makala iliyopita tumeona mfumo wa uendeshaji biashara na mamlaka inayohusika na usajili wa biashara hizo. Tumeanza kuchambua juu ya makundi ya kampuni katika makala iliyopita ambapo tumeona mgawanyo wa makundi ya aina kuu tatu. Leo tunaenda kuangalia kwa ufafanuzi zaidi aina za kampuni zinazopatikana katika makundi hayo. Karibu tujifunze.

Makundi ya Kampuni

Katika makala ya utangulizi wa makundi ya kampuni tuliweza kueleza kwa uchache juu ya makundi matatu ambayo kampuni zinaweza kugawanywa. Mgawanyo huu unatokana na mtazawo wa makampuni kwa mujibu wa

  • Mgawanyo wa kampuni kwa asili; hapa tuna kampuni zilizosajiliwa ndani ya Tanzania na zile ambazo zimesajiliwa nje ya Tanzania.

 

  • Mgawanyo wa kampuni kwa ukomo wa madeni; hapa tuna mgawanyo wa ukomo wa madeni ndani ya kampuni na ukomo nje ya kampuni

 

 

  • Mgawanyo wa kampuni kwa umiliki; hapa tuna mgawanyo wa kampuni binafsi na zile za umma.

Katika kuendelea kufafanua dhana hii ya mgawanyo wa makampuni, katika makala ya leo tutaanza kuzichambua kila aina ya kampuni inayopatikana kwenye makundi haya ya kampuni.

Kampuni Binafsi

Kampuni binafsi ‘private company’ ni aina ya kampuni inayomilikiwa na idadi ndogo ya wamiliki kuanzia 2 na wasiozidi 50. Msingi wa kampuni binafsi ni aina ya biashara inayoendeshwa na watu ambao wana mahusiano ya karibu kama mke na mume, au wazazi na watoto au jamaa wa karibu wenye taaluma moja.

Sifa za msingi za kampuni binafsi

Zipo sifa au asili ya uundwaji wa kampuni binafsi ambazo zinatofautisha na mfumo wa kampuni nyingine. Zifuatazo ni baadhi ya sifa husika;

  • Kampuni binafsi kwa kawaida huundwa na watu walio na mahusiano ya karibu ikiwa ya kifamilia au kindugu au urafiki au taaluma.
  • Kampuni binafsi inaweza kuanzishwa na wanahisa angalau 2 na wasiozidi 50

 

  • Hisa za kampuni binafsi si rahisi kuhamishwa kwenda kwa wengine wasio wa kampuni husika

 

  • Kampuni binafsi haiweki hisa zake katika soko la hisa

 

  • Kampuni binafsi mitaji yake inaishia kuchangiwa na wanahisa tu walio ndani ya kampuni na si umma kwa kuchangia kununua hisa.

 

  • Kampuni binafsi ili kufanya kazi inapaswa kuwa na idadi ya wakurugenzi wasiopungua 2.

 

  • Kama ilivyo kwenye kampuni nyingine, kampuni binafsi ni tofauti na wamiliki wake yaani inajitegemea katika uendeshaji wake.

 

Hitimisho

Leo tumeangalia kwa sehemu juu ya aina ya kampuni binafsi. Mfumo huu au aina hii ni nzuri sana kwa wale wanaoanza biashara na wenye malengo yanayofanana. Ni vyema kwa watu kufanya uchaguzi sahihi na kuanzisha kampuni za aina hii kwani uanzishwaji wake una gharama nafuu.

Kumbuka kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema.

Wako

Isaack Zake, Wakili