40. Nafuu kwa Mfanyakazi aliyeachishwa kazi kinyume na Sheria.

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu  ya Tuzo tukijufunza maana yake, uandishi wake na athari zake kwa pande zote. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Nafuu mbalimbali anazopata mfanyakazi aliyeachishwa kazi kinyume na sheria.

Maana ya Nafuu

Nafuu ni neno la kisheria lililotafsiriwa kutoka neno la kiingereza ‘relief au remedy’ ikiwa na maana ya malipo au stahiki anazopata mtu kutokana na kudhibitishwa kwa madai yake kisheria.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukiangalia juu ya mchakato mzima wa kuajiri na mahusiano baina ya mwajiri na mfanyakazi. Pia tumeona namna mbalimbali ambazo mfanyakazi anaweza kuachishwa kazi na hatua anazopaswa kuchukua endapo ataona kuachishwa huko hapakuwa na uhalali wa kisheria.

Tatizo kubwa ambalo wanalo wafanyakazi wengi ni kutokufahamu haki zao pindi wanapoingia katika mikataba ya ajira, wanapokuwa kwenye ajira na hata pale ajira inapokoma. Hii inasababisha dhuluma kubwa sana dhidi yao kwa kutokujua. Kama msemo wetu wa kila siku kutokujua sheria sio utetezi, wafanyakazi wamekuwa wahanga wakubwa kwa kutokuijua sheria.

Ndugu msomaji ikiwa ni mfanyakazi na leo hii ajira yako imesitishwa na mwajiri wako, je haki zako ni zipi? Je, utaenda Tume kufungua shauri dhidi ya mwajiri ukidai nini? Kwa uzoefu wangu ni wafanyakazi wachache sana wanaojua haki zao endapo suala kama hili litajitokeza. Katika makala hii tutakwenda kujifunza juu ya nafuu au stahiki za mfanyakazi anazoweza kudai na kupata endapo atakuwa amesitishwa ajira kinyume cha sheria.

Nafuu za kisheria

Sheria ya Ajira na mahusiano Kazini zinaeleza wazi juu ya nafuu anazoweza kupata mfanyakazi endapo Tume au Mahakama imeona na kudhibitisha kuwa usitishaji wa ajira haukuwa halali.

Kifungu cha 40 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004 kinaeleza kwa ufasaha juu ya aina za nafuu ambazo mfanyakazi anaweza kupata endapo itadhibitika kuwa aliachishwa kazi isivyo halali. Tume au Mahakama Kuu inaweza kuamua mojawapo ya nafuu zifuatazo;-

  1. Kumrejesha Kazini Mfanyakazi

Endapo Tume au Mahakama imebaini baada ya ushahidi kuwa ajira ilisitishwa isivyo halali basi inaweza kumwamuru mwajiri kumrejesha mfanyakazi katika kazi yake tangu siku ile ambayo ajira yake ilisitishwa isivyo halali. Hii ina maana kuwa mwajiri atawajibika kumlipa mfanyakazi mishahara yote tangu siku ile aliyomwachisha kazi mpaka siku Tume au Mahakama inatoa uamuzi. Amri hii haijailishi shauri limechukua miaka mingapi, ikiwa ni la miaka 2 basi atalipwa mishahara yote kwa kipindi hicho alichokuwa nje ya ajira. Kwamba mwajiri anapaswa kumrudisha kazini mfanyakazi huyo kuendelea na majukumu yake.

  1. Kumwajiri upya mfanyakazi kwa masharti

Tume au Mahakama kulingana na ushahidi uliotolewa inaweza kuamuru mfanyakazi husika kuajiriwa upya na mwajiri kulingana na masharti ambayo Tume au Mahakama inaona yanafaa.

  1. Kumlipa mfanyakazi fidia

Pia Tume au Mahakama ina uhuru wa kuagiza mwajiri kumlipa mfanyakazi fidia ya madhara aliyopata kutokana na kusitishiwa ajira kinyume cha sheria. Sheria imeweka kiwango cha chini cha fidia hiyo ni angalau mishahara ya miezi 12 ya mfanyakazi.

Hizi ndizo nafuu ambazo sheria ya Ajira imeziweka wazi endapo Tume au Mahakama itaona kuwa usitishaji wa ajira haukuwa halali. Hatahivyo ieleweke kuwa amri ya kulipa fidia si mbadala wa malipo au madai mengine ambayo mwajiriwa anastahili kwa masharti yoyote ya sheria au makubaliano. Mfano Tume imetoa fidia ya miezi 12 na katika mkataba wa ajira kuna kipengele kuwa endapo mwajiri atasitisha ajira ya mfanyakazi basi atamlipa kiasi cha kadhaa kama mkono wa heri basi kiasi hicho pia lazima kitalipwa na mwajiri.

Nini kinatokea endapo mwajiri hataki kumrejesha mfanyakazi kama amri ya Tume au Mahakama inavyotaka?

Sheria ya Ajira kama ilivyo sheria zingine na mahusiano mengine ya kimkataba ni suala la hiyari. Inawezekana Tume au Mahakama kutoa amri ya mfanyakazi kurejeshwa kazini au kuajiriwa upya kazini lakini mahusiano yake na mwajiri yasiwe mazuri na mwajiri hataki kuendeleza mahusiano hayo, sheria imeweka utaratibu ambao utamtaka mwajiri kufanya yafuatayo;

  • Kulipa mishahara yote tangu mfanyakazi asitishwe ajira isivyo halali mpaka siku ya kutekeleza amri ya Tume
  • Kulipa marupurupu yote ya mfanyakazi husika tangu siku ya kusitisha ajira mpaka siku ya kutekeleza amri ya Tume

 

  • Kumlipa mfanyakazi fidia ya miezi 12

 

Hitimisho

Ndugu msomaji natumai leo umejifunza juu ya nafuu ambazo mfanyakazi anaweza kupata endapo itabainika kuwa amesitishwa ajira isivyo halali. Pamoja kwamba nafuu hizi zipo ndani ya sheria si suala la Tume au Mahakama kukupatia tu bali unapaswa kuzijua na kuomba wakati unafungua shauri lako. Tume haiwezi kukurudisha kazini wakati maombi yako ni kulipwa fidia ni muhimu kujua ni aina ipi ya nafuu ambayo ina maslahi mazuri kwako. Pata ushauri wa wanasheria ili kufahamu namna bora ya kufungua shauri ambalo litaleta tija baada ya kumalizika

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.