41.Malipo ya Kisheria kwa Mfanyakazi aliyeachishwa kazi kihalali.

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu  ya nafuu anazostahili mfanyakazi aliyeachishwa kazi pasipo kufuata utaratibu wa kisheria. Leo tunakwenda kuangalia juu ya malipo au stahili anazopaswa kupewa mfanyakazi endapo anaachishwa kazi kwa kufuata taratibu za kisheria.

 

Usitishwaji wa Ajira Kihalali

Kama tunavyofahamu kuwa mahusiano ya kiajira ni mahusiano ya kimkataba ambayo yana muda maalum. Hivyo yapo mazingira ambayo yanaweza kupelekea mkataba kumalizika kwa pande zote pasipo kuwa na mgogoro wa aina yoyote.

Endapo mwajiri atazingatia taratibu zote za usitishaji wa ajiri basi usitishaji huo utakuwa halali. Tumeangalia namna za usitishaji wa ajira ulio halali katika makala za mwazo.

Malipo ya kisheria

Sheria ya Ajira na mahusiano Kazini zinaeleza wazi kuhusu malipo ya kisheria ambayo anastahili mfanyakazi kulipwa pindi ajira yake itakapofikia ukomo. Malipo haya ni muhimu yafahamike kwa mwajiri na pia kwa mfanyakazi. Waajiri wengi kama walivyo wafanyakazi hawana ufahamu ni vitu gani wanapaswa kulipa pindi mahusiano ya kiajira yanapofikia mwisho. Pande zote zinaingia mgogoro kwa kutokujua stahiki zinazopaswa kulipwa.

Vifungu vya 41 – 44 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004 vinaeleza mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa kusitisha ajira.  Malipo haya ni kama ifuatavyo

  1. Mshahara badala ya taarifa

Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri kutoa taarifa kwa mfanyakazi juu ya kusudio lake ya kusitisha ajira. Hii inampa mfanyakazi nafasi ya kujiandaa kuondoka kazini mara baada ya taarifa ile kutolewa. Kwa kazi ambayo mfanyakazi analipwa kwa mwezi basi taarifa inapaswa kutolewa mwezi mmoja kabla ya siku ya kusitisha ajira, na kwa mfanyakazi anayelipwa kwa siku au wiki basi taarifa isiwe chini ya siku nne. Hatahivyo inaweza kujitokeza hali ya mwajiri kutokutoa taarifa ndani ya muda husika, sheria inamwelekeza kulipa mshahara huo badala ya taarifa. Mfano mwajiri anakusudia kusitisha ajira mwisho wa mwezi Machi 2018 ingawa hakutoa taarifa mapema basi anapaswa kulipa mshahara wa mwezi Machi 2018 ambao mfanyakazi amefanya kazi na ule wa mwezi April 2018 ambao utakuwa ni mbadala wa taarifa.

  1. Mshahara kwa kazi iliyofanywa na mfanyakazi

Mwajiri anatakiwa ahakikishe kuwa anamlipa mfanyakazi mishahara au mshahara kwa kazi ambazo mfanyakazi amefanya. Kunatokea kuwa wapo waajiri ambao wanalimbikiza mishahara ya wafanyakazi. Hivyo pindi mwajiri anamwachisha mfanyakazi anapaswa kulipa malimbikizo yote ya madai ya mishahara na marupurupo mengine.

  1. Likizo ambazo mfanyakazi hajaenda

Ifahamike kuwa likizo ni haki ya mfanyakazi ambaye anafanya kazi kwa mfululizo wa miezi 12 kwa mwajiri mmoja. Yapo mazingira yanayojitokeza mahali pa kazi mfanyakazi anakosa muda wa kwenda likizo. Ni muhimu kwa mwajiri wakati wa kusitisha ajira kuhakikisha mfanyakazi analipwa kiasi cha likizo alizopaswa kwenda. Hatahivyo, mfanyakazi atapata haki ya likizo isiyozidi likizo 3 kwa miaka 3. Mfanyakazi asiyekwenda likizo hata zaidi ya 3 hatolipwa hizo nyingine. Pia mwajiri anapaswa kumlipa mfanyakazi siku za likizo ambazo bado hazijakamilika.

  1. Kiinua Mgongo

Mwajiri anapaswa kumlipa mfanyakazi kiinua mgongo mara baada ya kusitisha ajira. Haki ya kiinua mgongo inalipwa kwa mfanyakazi endapo atakuwa amefanya kazi mfululizo kwa mwajiri kwa kipindi cha miezi 12. Ukomo wa kiinua mgongo anachostahili kulipwa mfanyakazi ni miaka 10 ya kazi kwa mwajiri. Kiinua mgongo hakitalipwa endapo mfanyakazi ameondolewa kwa utovu wa nidhamu.

 

  1. Nauli na usafirishaji wa mizigo

Yapo mazingira ambayo mfanyakazi anafanya kazi mahali tofauti na pale alipajiriwa. Endapo mazingira haya yatajitokeza ni wajibu wa mwajiri kumlipa mfanyakazi nauli na kusafirisha familia yake na mizigo yake mpaka sehemu aliyomwajiri.

Pia ni muhimu kuzingatia cheti cha Utumishi pale ambapo ajira inasitishwa ambacho mwajiri anapaswa kumpatia mfanyakazi.

 

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa pande zote kwenye mahusiano ya kiajira kufahamu haki na wajibu wao katika mkataba husika. Ufahamu huu utasaidia sana kupunguza idadi kubwa ya migogoro inayowasilishwa Tume kwa kigezo tu cha kutokujua shahili za wafanyakazi na wajibu wa waajiri. Tunatoa rai kwa wafanyakazi na waajiri pia na wadau wa sekta ya ajira kama vyama vya waajiri na wafanyakazi kutoa elimu ya kutosha kwa wadau wao mara kwa mara. Wafanyakazi ni lazima wafahamu kuwa ipo siku ajira hiyo itakoma na lazima wawe na ufahamu wa haki zao.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.