42. Mamlaka ya Mahakama ya Kazi

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala zilizopita tulikua tukichambua masuala ya nafuu za kisheria endapo Tume itaamua kuwa usitishwaji wa ajira haukua halali. Leo tunaangalia mchakato wa utatuzi wa migogoro ya kazi ngazi ya Mahakama ya Kazi.Karibu tujifunze.

Utatuzi wa Migogoro ya Kazi

Katika makala ya utatuzi wa migogoro ya kazi tulieleza juu ya njia ambazo zimewekwa kisheria kuhusika na utatuzi wa migogoro ya kazi. Vyombo vilivyoanishwa kisheria ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na Mahakama ya Kazi. Vyombo hivi ndivyo vimepewa jukumu la msingi la utatuzi wa migogoro ya kazi. Tumeeleza madhara ya wadau kutokutumia vyombo hivi katika kushughulikia migogoro ya kazi ni hatimaye kupoteza haki zao. Tumeangalia kwa kirefu mchakato unaohusika na utatuzi wa migogoro kwenye ngazi ya Tume ikuhusisha Usuluhishi na Uamuzi. Katika makala hii tutaangalia kwa kirefu juu ya mchakato wa utatuzi katika Mahakama ya Kazi

Mahakama ya Kazi

Mahakama ya Kazi ni sehemu ya kitengo cha Mahakama Kuu kama mahakama nyingine yenye kushughulikia tu migogoro ya kazi. Migogoro ya kazi ina mfumo wake ya utatuzi ambapo huanzia kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kisha Mahakama ya Kazi na endapo upande wowote haujaridhika basi unaweza kufika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambacho ndicho chombo cha juu kabisa kwenye utatuzi wa migogoro yote.

Mahakama ya Kazi inayo mamlaka ya kipekee kuhusiana masuala ya matumizi, tafsiri na utekelezaji wa Sheria ya Ajira na sheria nyingine za kazi pamoja na kutoa maamuzi juu ya;-

  • Rufaa kutokana na maamuzi ya Msajili wa vyama vya wafanyakazi na waajiri
  • Mapitio na marejeo ya
  • Tuzo ya Mwamuzi
  • Maamuzi ya Kamati ya Huduma Muhimu
  • Mapitio ya maamuzi, kanuni na miongozo itolewayo na waziri
  • Malalamiko yanayopaswa kusikilizwa na mahakama ya Kazi
  • Migogoro inayopaswa kusikilizwa na kutolewa maamuzi na Mahakama ya Kazi
  • Maombi ikiwemo;-
  • Amri ya tamko au
  • Amri ya zuio

Haya ni maeneo ambayo mahakama ya Kazi ina mamlaka ya kuyashughulikia kwa kusikiliza na kutoa maamuzi.

 

Hitimisho

Ndugu msomaji, leo tumejifunza juu ya mamlaka ya mahakama ya Kazi katika utatuzi wa masuala mbalimbali yanayohusiana na kazi. Ni muhimu sana kwa wadau wa kazi kufahamu mamlaka hii ya mahakama ya Kazi. Zimekuwepo changamoto za wadau kutokuitumia mahakama ya Kazi katika ufumbuzi wa matatizo ya kazi bali wanatumia njia nyingine au mamlaka nyingine ambazo kisheria hazina uhalali wa kusikiliza au kutoa maamuzi yanayohusiana na utatuzi wa mgogoro wa kazi. Iwapo huna ufahamu wa kutosha juu ya kuwasilisha malalamiko au mgogoro wako katika mahakama hii ni vyema kuwasiliana na wanasheria wenye ufahamu juu ya utendaji wa mahakama hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.