43. Haki ya Marejeo au Mapitio ya Tuzo
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia juu mamlaka ya mahakama ya kazi. Leo tunakwenda kuangalia juu ya Mamlaka ya Mahakama ya Kazi kufanya Marejeo au Mapitio ya Maamuzi ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.
Maamuzi ya Tume
Kama tulivyoangalia katika makala zilizotangulia tumeona njia za utatuzi wa migogoro ya kazi. Njia kuu tulizoona ni usuluhishi na uamuzi ambazo tayari tumeziangalia katika makala zilizopita.
Mara baada ya maamuzi ya Tume kutoka hasa katika ngazi ya Uamuzi ni lazima kuna upande utakaokuwa umeshinda yaani kupata Tuzo na upande ule ambao umeshindwa kwenye shauri husika.
Sheria ya Ajira inatoa fursa kwa upande usioridhika na maamuzi ya Tume kupata nafasi ya marejeo ya uamuzi wa Tume.
Haki ya Marejeo au Mapitio juu ya Tuzo ya Tume
Sheria ya ajira imetoa haki kwa upande wowote wa mgogoro wa kazi ambao haujaridhika na maamuzi au Tuzo ya Tume kuomba marejeo au mapitio ya uamuzi husika mbele ya Mahakama ya Kazi.
Kwa kawaida na kwa mujibu wa sheria uamuzi wa Tume haukatiwi rufaa bali unaweza kufanyiwa marejeo au mapitio na Mahakama ya Kazi.
Sheria inatoa kipindi kisichozidi wiki 6 tangu uamuzi wa Tume kutolewa kwa upande usioridhika kuchukua hatua ya kuomba marejeo au mapitio ya Tuzo hiyo mbele ya Mahakama ya Kazi.
Nyaraka Muhimu wakati wa kuomba Marejeo au Mapitio
Upande usioridhika na maamuzi ya Tume unaweza kuomba marejeo au mapitio kwa kuandaa nyaraka za kisheria kwa mujibu wa Kanuni za Mahakama Kuu ya Kazi toleo la 2007 ambazo zitahusisha;
- Notisi kwa Msajili wa Mahakama ya Kazi (Notice)
- Maombi ya Faragha (Chamber summons)
- Hati ya Kiapo (Affidavit)
Katika uandaaji wa nyaraka hizi, upande usioridhika utajieleza sababu za kutoridhika na Tuzo ya Mwamuzi wa Tume na maombi yake mbele ya Mahakama ya Kazi.
Mahakama ya Kazi itasikiliza marejeo au mapitio yaliyoombwa mbele ya Jaji wa Mahakama kuu na atakuwa na mamlaka ya kutengua maamuzi ya Tume endapo sababu za msingi zitadhibitishwa au atayadhibitisha maamuzi ya Tume endapo mwombaji atashindwa kudhibitisha juu ya sababu za msingi.
Hitimisho
Kwa uzoefu wa mashauri ya kazi ni rahisi kufanya mashauri ngazi ya Tume kwani hata lugha inayotumika na nyaraka zinazoandaliwa zinaweza kuandaliwa kwa lugha ya Kiswahili, hatahivyo mbele ya Mahakama kuu mara nyingi lugha inayotumika kuandaa nyaraka ni lugha ya kiingereza hivyo kuwa ngumu sana kwa wadaawa kuendesha mashauri yao pasipo msaada wa wataalamu wa kisheria. Hivyo ni muhimu kupata ushauri wa kisheria juu ya uendeshaji wa shauri mbele ya Mahakama ya Kazi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.