46. Dai la Fidia

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeanza kuchambua hoja na swali linalohusu aina na dai au madai ambayo mfanyakazi anaweza kudai endapo ataachishwa kazi isivyo kihalali. Tumeona juu ya ufafanuzi katika Dai la Kurudishwa Kazini. Leo tunaenda kuangalia juu ya Dai la Fidia huku tukiendelea kujibu swali letu la msingi linalouliza;

Nini unaweza kudai endapo umeachishwa kazi isivyo kihalali?

Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

Dai la Fidia

Sheria ya ajira inatoa nafuu au kuruhusu mfanyakazi kuomba Fidia. Fidia ni aina ya nafuu ambayo inatolewa ili kumpunguzia maumivu ya kiuchumi aliyopata mfanyakazi kutokana na kusitishwa ajira.

Sheria inaeleza kuwa endapo itadhibitika kuwa mfanyakazi ameachishwa kazi pasipo uhalali basi Tume inaweza kutoa fidia ya angalau mishahara ya miezi 12 kwa mfanyakazi. Hii itamsaidia mfanyakazi kujipanga wakati akiangalia utaratibu mwengine wa kuendesha maisha yake au kutafuta kazi nyingine.

Unapoomba dai la fidia huwezi wakati huo huo ukaomba dai la kurudishwa kazini, huwezi kupata vyote kwa wakati mmoja ni ama urudishwe kazini au ulipwe fidia.

Mara nyingi wafanyakazi kwa hofu ya kutokutaka kurudi kazini wanaomba walipwe fidia. Hatahivyo kulingana na muda unaoweza kuchukua kesi kuendeshwa unajikuta muda mwingi umeisha na hatimaye unalipwa fidia ya miezi 12 tu pasipo muda ule ambao ulikuwa unaendesha shauri hata kama ni zaidi ya miaka 2.

Jambo lingine ambalo ni muhimu wafanyakazi kufahamu ni kuwa fidia inaweza kutolewa hata zaidi ya miezi 12. Sheria imeweka ukomo wa chini wa kiwango cha miezi 12 lakini haijaweka kiwango cha juu. Hivyo itategemea hoja za mfanyakazi zinaweza kuonesha ni kiasi gani ameathiriwa na kuachishwa huko kazi. Ipo mifano ya mashauri ambayo watu wamelipwa fidia hadi miezi 36.

Faida za Dai la Fidia

  • Kulipwa fidia na kuachana na mwajiri husika pasipo kuwa na mazingira ya mwajiri kukuchukulia hatua kwani hautakuwa kazini kwake.

 

Hasara za Dai la Fidia

Kutekelezwa kwa dai hili kunaweza kuleta hasara kadhaa kwa mfanyakazi ambazo anapaswa kuzifahamu

  • Dai la fidia linaweza kukukosesha mishahara ambayo ulipaswa kuipata kipindi kizima wakati kesi inaendelea kama halitafafanuliwa vizuri.
  • Unaweza kulipwa fidia lakini ukapata changamoto ya kupata ajira nyingine

 

Hitimisho

Ni muhimu kufahamu ya kuwa juu ya dai la fidia kwani lina faida zake na hasara zake. Kulinganisha na dai la kurudishwa kazini ambalo lina faida zaidi na ni mbadala endapo mwajiri hataki kumrudisha kazini basi anapaswa kumlipa mishahara yote pamoja na fidia. Hivyo ninasisitiza juu ya kupata ushauri mapema kabla ya kudai au kuandaa madai yako kwenye fomu Na.1 ya CMA kwani kili kinachodiwa ndicho Tume au Mahakama itatoa.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.