47.A. Madai Mengine Muhimu katika Usitishaji wa Ajira

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeanza kuchambua hoja na swali linalohusu aina na dai au madai ambayo mfanyakazi anaweza kudai endapo ataachishwa kazi isivyo kihalali. Tumeona juu ya ufafanuzi katika Dai la Fidia. Leo tunaenda kuangalia juu ya madai mengine muhimu. Tunaendelea kujibu swali la msingi

Nini unaweza kudai endapo umeachishwa kazi isivyo kihalali?

Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

Msingi wa Madai

Mfanyakazi aliyeathiriwa na kuondolewa kazini isivyo halali kwa kawaida anakuwa katika hali ya kutokuwa vizuri. Hivyo anapofuatilia haki zake za kiajira ni muhimu kufahamu madai anayopaswa kudai kisheria au nafuu zilizotolewa ndani ya sheria ya ajira.

Nimeshuhudia mara kwa mara kwenye mashauri ya kazi, mfanyakazi anaulizwa ni kitu gani au haki gani anataka Tume imsaidie kumpatia, wengi hujibu tu kama Tume inavyoona inafaa. Hili si jibu zuri au mwafaka unahitaji kujipanga na kufahamu kwa ufasaha ni kitu au haki gani za kisheria unastahili endapo itadhibitika kuwa usitishwaji wa ajira haukuwa halali.

Madai Mengine

Katika makala hii tunaenda kuangalia nafuu nyingine ambazo mfanyakazi ana haki ya kuzidai mbele ya Tume pale anapopinga usitishwaji usio halali wa ajira.

  1. Malimbikizo ya mishahara (Accrued salaries)

Mfanyakazi ni muhimu kueleza katika Fomu Na.1 ya CMA endapo kuna malimbikizo ya mishahara ambayo alikuwa anamdai mwajiri. Kuacha kuainisha madai anayomdai mwajiri kutasababisha kupunjwa malipo haya au Tume kutoyazingatia katika maamuzi yake. Hivyo kama mfanyakazi ana madai ya mishahara aliyofanyia kazi kabla ya kusitishwa ajira isivyo halali basi anapaswa kudai.

Mfano

Mfanyakazi anaachishwa kazi mwezi Mei lakini kipindi anachoachishwa mwajiri hakuwa amemlipa mishahara ya mwezi Machi na April, basi katika Fomu ya Madai ni lazima aeleze kuwa anadai na malimbikizo ya mishahara ya mwezi Machi na April.

  1. Mshahara badala ya notisi (Remuneration in lieu of notice)

Endapo mwajiri alisitisha ajira ya mfanyakazi pasipo notisi kama sheria inavyoeleza alipaswa kumlipa kiasi cha fedha badala ya notisi. Waajiri wengi huwa hawalipi kiasi cha fedha na pia hawatoi notisi. Endapo mfanyakazi atasitishiwa ajira yake pasipo notisi au kiasi cha fedha kulingana na notisi basi ni lazima aeleze kwenye Fomu Na.1 juu ya dai lake la malipo ya kiasi cha fedha badala ya notisi.

Mfano

Sheria inamtaka mwajiri kutoa notisi ya siku 28 kwa mfanyakazi anayelipwa mshahara kwa mwezi kama haitaendelea na mfanyakazi huyo au badala ya notisi mwajiri alipaswa kulipa kiasi cha mshahara wa mwezi kwa mfanyakazi huyo. Endapo mwajira hayafaya haya yote basi mfanyakazi katika madai yake atadai kiasi cha mshahara wa mwezi mmoja badala ya notisi.

  1. Kiinua Mgongo (Severance Pay)

Hii pia ni haki ya mfanyakazi endapo itadhibitika kuwa aliachishwa kazi isivyo halali. Haki ya kiinua mgongo inaanza kupatikana pale mfanyakazi anapokuwa amekamilisha mwaka yaani miezi 12 na mwajiri wake. Mfanyakazi aliyefanya kazi chini ya kipindi cha miezi 12 kwa mwajiri mmoja hawezi kudai kiinua mgongo.

Kiinua mgongo ni mishahara ya siku 7 kwa kila mwaka wa mfanyakazi aliofanya kwa mwajiri mmoja hadi kipindi kisichozidi miaka 10. Hivyo ni muhimu kufanya hesabu za kupata mshahara wa siku kisha unazidisha kwa saba kwa kipindi kisichozidi miaka 10.

Mfano

Alex amefanya kazi kampuni ya ABC ambapo amekuwa akilipwa mshahara wa Tsh.100,000/- na amefanya kazi katika kampuni hiyo kwa miaka 9. Je, atalipwa kiasi gani?

100,000  = 3846.15 (mshahara wa siku)

26 (siku za kazi katika mwezi)

3846.15 x siku 7 x miaka 9 = Tsh.242,307.45

Hivyo dai la kiinua mgongo la Alex ni kiasi cha Tsh.242.307.45.

Ni muhimu kukumbuka kigezo cha kupata dai hili ni kufanya kazi kwa mwajiri mmoja kwa kipindi kisichopungua mwaka 1 na kitalipwa kwa kipindi kisichozidi miaka 10 hata kama mfanyakazi amefanya kazi kwa kipindi zaidi ya miaka 10.

Hitimisho

Haya ni baadhi ya madai mengine muhimu ambayo sheria ya ajira inayatambua pia ni wajibu wa mwajiri na mfanyakazi kuyatambua. Wafanyakazi wengi wanapokuwa katika kudai haki zao hawana ufahamu juu ya madai haya ni hivyo kuyakosa au kushindwa kuyazungumzia kwenye maelezo yao au Fomu Na.1 ya CMA. Katika makala nyingine tutaendelea kujifunza juu ya madai mengine ya kisheri ambayo ni muhimu kwa mfanyakazi kuyazingatia.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.