53. Uzembe unaoathiri utendaji wa kazi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeona juu ya Utoro Uliokithiri au Kutelekeza Kazi. Leo tunaangalia juu kosa la Uzembe unaoathiri utendaji wa kazi. Karibu tujifunze.

Utendaji wa Kazi Usioridhisha

Sheria ya Kazi na Ajira inatambua kuwa mfanyakazi anaweza kuachishwa kazi kwa utendaji usioridhisha ‘poor work perfomance’.

Utendaji wa mfanyakazi usioridhisha ni hali ya kiwango cha utendaji chini ya viwango vya kazi vilivyowekwa na mwajiri. Sheria ya ajira inatambua haki ya mwajiri kuweka viwango vya kazi, hivi ni viwango ambavyo wafanyakazi wanapaswa kuvizingatia katika utendaji wao.

Uzembe kazini au tabia ya uzembe inayosababisha kiwango cha kazi kutokufikiwa linaweza kuwa kosa linalosababisha kusitishwa kwa ajira ya mfanyakazi.

Ni lazima kufahamu kuwa, mwajiri anapomwajiri mfanyakazi kuna mambo anatarajia kutoka kwa mfanyakazi, jambo la msingi sana kwa mwajiri ni utendaji wa kazi kwa viwango vinavyotarajiwa ili kuleta tija na manufaa kwa mwajiri. Hakuna mwajiri anayeweza kuvumilia suala la uzembe ambao utasababisha hasara au kuharibika kwa kazi yake.

Sheria ya Kazi na Ajira kupitia Kanuni za Utendaji Bora ‘Employment and Labour Relations (Code of Good Prictice)’ inaeleza kuwa mfanyakazi anaweza kuachishwa kazi kwa kosa la utendaji mbovu wa kazi kutokana na uzembe.

‘Habitual, substantial or wilful negligence in the performance of work’

Maana yake mfanyakazi anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa vitendo vya kitabia vya uzembe ulikithiri unaothiri utendaji wa kazi

Vigezo vya kuchukua hatua dhidi ya mfanyakazi kwa Uzembe unaoathiri utendaji

Vipo vigezo vya kisheria vinavyopaswa kuzingatiwa na mwajiri ili kuweza kuchukua hatua dhidi ya mfanyakazi. Waajiri wengi wanashindwa kufahamu ni makosa ya aina gani yanaweza kuonesha kuna uzembe ulikithiri ambao unaathiri kazi. Mahakama imeweka vigezo vya msingi vya kuzingatia ili kuthibitisha suala la uzembe unaathiri kazi. Vigezo hivi vilianishwa katika kesi maarufu ya Donoghue v Stevenson (1932) A.C.562, ambayo ilinukuliwa katika kesi ya Twiga Bancorp Limited v. Zuhura Zidadu na Mwajuma Ally, Marejeo Na.206 ya 2014, mbele ya Mhe. Jaji Aboud wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi;

  1. Uwepo wa wajibu

Kwamba lazima kuwe kuna wajibu ambao mfanyakazi anapaswa kuuzingatia ‘duty of care’. Ili kosa la uzembe linaloathiri kazi liweze kuthibitika dhidi ya mfanyakazi husika ni lazima kuwepo na wajibu aliopewa mfanyakazi husika. Huwezi kumchukulia hatua mfanyakazi kwa kosa ambalo hawajibiki nalo.

  1. Ukiukwaji wa wajibu

Kwamba wajibu huo umekiukwa na mfanyakazi yaani hakuuzingatia kama alivyopaswa ‘breach of duty of care’. Mfanyakazi anapaswa kuwa ameshindwa kuzingatia wajibu huo kwa uzembe. Mfanyakazi anaacha kufanya anachopaswa kufanya kwa mujibu wa wajibu aliopewa na mwajiri.

  1. Ukiukwaji wa wajibu huo kupelekea madhara

Kwamba kukiukwa huko kwa wajibu huo kumesababisha madhara kwa mwajiri au kazi husika ‘the breach caused damage’. Madhara ni lazima yawe matokeo ya kutotimizwa kwa wajibu huo na mfanyakazi. Mwajiri ni lazima ajiridhishe kuwa yapo madhara ambayo ni matokeo ya mfanyakazi kutokutimiza wajibu wake.

  1. Madhara yawe dhahiri

Kwamba madhara hayo ni dhahiri na yalitarajiwa kutokea endapo mfanyakazi ameshindwa kutekeleza wajibu ‘the damage was foreseeable’. Ni muhimu kuzingatia kuwa madhara yanayotokea kutokana na ukiukwaji wa wajibu ni lazima yawe dhahiri au yaliyotarajiwa kutokea sio yaliyojificha au yasiyohusiana na uzembe wa mfanyakazi.

Hivi ndivyo vigezo vinavyotumika katika kuthibitisha uzembe wa mfanyakazi unaoathiri utendaji wa kazi.

Hitimisho

Uzembe kazini ni moja ya kosa kubwa linaloweza kusababisha kusitishwa kwa ajira hata kama limejitokeza mara moja au kwa kujirudiarudia. Ni dhahiri kuwa kitu kinachowaunganisha mfanyakazi na mwajiri ni kazi, na kazi hiyo inapaswa kufanywa kwa uadilifu na umakini mkubwa ili mfanyakazi alete tija kwa mwajiri na mwajiri aweze kumlipa mfanyakazi ipasavyo. Kosa la uzembe halivumiliki kwa mwajiri, mfanyakazi anapaswa awe makini azingatie maelekezo na viwango vya utendaji vilivyowekwa na mwajiri. Ni muhimu pia kwa mwajiri kuhakikisha kazi anayoitoa inaeleweka vizuri kwa mfanyakazi na wajibu unaopaswa kuzingatiwa unafanywa vizuri.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com