61. Je, ninaweza kudai Mwajiri wakati sina Mkataba wa Maandishi?


Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeweza kujibu swali ya kwamba nini mfanyakazi anaweza kufanya endapo atakatwa mshahara pasipo utaratibu. Leo tunakwenda kuangalia endapo mfanyakazi anaweza kuwa na madai kwa mwajiri wake pasipo kuwa na mkataba wa maandishi. Karibu tujifunze.

Hali ya Mahusiano ya Kiajira

Moja ya changamoto kubwa hasa inayowakuta wafanyakazi wengi ni kuwa katika ajira pasipo mikataba ya maandishi. Waajiri kwa sababu moja ama nyingine wamekuwa wazito kutoa mkataba wa maandishi kwa wafanyakazi wao. Hii ni hali ya wafanyakazi wengi. Upatikanaji wa mkataba baina ya pande mbili inakuwa kama vita ambayo mfanyakazi anakuwa mnyonge akihofia kufukuzwa kazi na huku mwajiri akihofia endapo atatoa mkataba basi mfanyakazi atakuwa msumbufu na anaweza kumchukulia hatua za kisheria.

Hali hii imekuwa ikiwakuta watu wengi katika ajira ya kwamba wamefanya kwa muda mrefu lakini hakuna mkataba wa maandishi kuhusiana na haki zao za kiajira.

Hivyo swali muhimu ambalo tunapenda kulijibu katika makala hii ni iwapo mfanyakazi anaweza kufungua madai ya haki zake za kiajira dhidi ya mwajiri hatakama hana mkataba wa maandishi?

Hatua ya 1

Dhana ya Uwepo wa mahusiano ya Kiajira

Sheria ya Kazi na Ajira inatambua mazingira ya mahusiano ya kiajira baina ya mfanyakazi na mwajiri hata pale unapokosekana mkataba wa maandishi. Dhana hii ya kisheria imewekwa mahsusi kuwalinda wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwa waajiri ambao hawako tayari kutoa mkataba wa maandishi.

Vipo vigezo ambavyo sheria inavizingatia ili kuonesha uhusiano wa kiajira inapaswa kuzingatiwa. Uwepo wa kigezo kimojawapo au vyote vitathibitisha uwepo wa uhusiano wa kiajira.

Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;

  • Iwapo namna ya ufanyaji kazi wako ulikuwa unasimamiwa na kupata maelekezo kutoka kwa mtu mwingine, au
  • Saa zako za kazi zinasimamiwa na kwa maelekezo ya mtu mwingine, au
  • Kwa mtu anayefanya kazi katika Shirika, mtu huyo ni sehemu ya Shirika, au
  • Umefanya kazi kwa mtu mwingine kwa wastani wa saa 45 kwa mwezi katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, au
  • Unamtegemea kiuchumi mtu anayemfanyia kazi au kumtolea huduma, au
  • Katika utendaji wako wa kazi unapatiwa vitendea kazi na mtu mwingine, au
  • Umekuwa  ukifanya kazi au kutoa huduma kwa mtu mmoja tu.

Kama tulivyoeleza ya kwamba hivi ni vigezo vya kisheria kwa ajili ya kuibua dhana ya uwepo wa uhusiano wa kiajira baina ya mtu na mwajiri wake katika mazingira ambayo hakuna mkataba wa maandishi. Kama umefanya kazi au kutoa huduma kwa mtu au shirika lakini huna uthibitisho wa kimaandishi basi ni muhimu kukagua vigezo hivi ili uweze kujua nafasi yako ikiwa ni mwajiriwa au la.

Endapo una kigezo kimojawapo kati ya hivi basi unayo haki na sababu ya kuwasilisha madai yoyote juu ya haki za kiajira dhidi ya mwajiri wako.

Wapo waajiri kwa makusudi hawatoi mkataba wala kitambulisho ili siku wakitaka kuachana na wewe kiajira basi wanakuondoa pasipo maandishi wala kumbukumbu yoyote. Hali hii huwakatisha sana tamaa wafanyakazi wakijua kuwa hawana namna ya kuweza kudai chochote au kupinga kusitishwa kwao ajira.

Ndugu msomaji hii ni hatua ya kwanza na muhimu sana kwako kutambua juu ya uhusiano wako wa kiajira baina yako na mwajiri hata kama hakuna mkataba wa maandishi.

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala za kujibu swali hili katika makala zijazo.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com