Sheria Jinai.4. Mambo ya Kuzingatia ili Wananchi watoe taarifa kwa Uhuru

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wetu na mfuatiliaji wa makala mbali mbali za mtandao wa uliza sheria. Katika makala iliyopita tuliangalia wajibu wa kutoa taarifa juu ya makosa ya jinai pamoja na kwa nini watu hawatoi taarifa za uhalifu. Leo tunaangalia mambo ya kuzingatia ili wananchi watoe taarifa kwa uhuru. Karibu ndugu msomaji tujufunze.

Wajibu wa kutoa taarifa juu ya uhalifu ni wa kila mmoja wetu ambaye anajua au amesikia kuhusiana na tukio lolote la kijinai.

Tumeona katika makala iliyopita juu ya changamoto zinazowafanya watu au wananchi kutokuwa wepesi kutoa taarifa za uhalifu katika maeneo yao. Leo tunaangalia juu ya mambo ya msingi yanayoweza kufanywa ili watu kuwa na utayari wa kutoa taarifa za uhalifu mapema kwa vyombo husika.

  1. Mfumo wa utoaji taarifa

Kama tulivyoona kwa mujibu wa sheria mtoa taarifa anapaswa kuwasilisha taarifa za uhalifu kwa kituo kilicho karibu yake. Hatahivyo uzoefu unaonesha mazingira ya uwasilishwaji wa taarifa hizi si rafiki sana kwa watoa taarifa. Kutokana na maendeleo ya kisayansi na teknolojia, mamlaka zinapaswa kuanza kutumia mbinu nyingine za ukusanyaji wa taarifa za kihalifu ambazo watoa taarifa wataona wapo salama zaidi. Mfano taarifa zinaweza kutolewa kwa njia ya simu, au ujumbe mfupi au barua pepe au barua pasipo kudhihirisha utambulisho wa mtoa taarifa. Ni kazi ya mamlaka kuchunguza endapo taarifa hizo zinaweza kuwa za ukweli na kuzuia uhalifu kujitokeza mahali.

2. Usiri wa mtoa taarifa

Hofu kubwa kwa watoa taarifa ni hali ya usiri wa taarifa wanazotoa. Ni muhimu sana kwa mamlaka zinazopokea taarifa za uhalifu au matukio kujua namna ya kutunza siri za watoa taarifa zao. Ni lazima watu wanaohusika na uchunguzi wa taarifa hizo wawe waaminifu kuhakikisha kuwa mtoa taarifa analindwa kutokana na taarifa alizotoa endapo zitasaidia kuzuia uhalifu au kuwakamata wahalifu.

3. Ushirikiano na watoa taarifa

Watoa taarifa wamekuwa na malalamiko juu ya wao kusumbuliwa na mamlaka kwa taarifa wanazotoa. Ni muhimu watoa taarifa kupewa ushirikiano kama wasaidizi wa kuzuia uhalifu na si kama wahalifu wenyewe. Zipo harakati na juhudi zinazofanywa na mamlaka kuweka ukaribu zaidi na jamii ili kusaidia jamii kuona wajibu wa kuzuia uhalifu kwani waathiriwa wakuu ni jamii husika.

4.Ulinzi wa kisheria kwa watoa taarifa

Kwa muda mrefu kumekuwa na jitihada za uundwaji wa sheria maalum ya ulinzi juu ya watoa taarifa. Jitihada hizi zimefanikiwa na Bungu limetunga sheria hii maalum kwa ajili ya ulinzi wa kisheria kwa watoa taarifa mbalimbali zinazoweza kuzuia uhalifu au kubaini wahalifu.

Hitimisho

Kama tulivyoona ya kwamba suala la utoaji wa taarifa za uhalifu ni jukumu la kila mmoja wetu mwenye kujua taarifa husika. Ni muhimu sana kwa wananchi kuwa na imani na vyombo vya uchunguzi ili taarifa zinazotolewe zilete tija na kuzuia uhalifu katika jamii. Pia vyombo vinavyohusika na uchunguzi vinapaswa kuchukua taarifa za uhalifu kwa umakini na usiri huku wakizifanyia kazi kwa weledi wote.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040